Friday, 18 November 2016

MREMA BADO SANA, AENDELEA KUSOTA RUMANDE HADI JUMANNE



MBUNGE  wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), ameendelea kusota rumande baada ya Mwanasheria wa Serikali Mwandamizi, Paul Kadushi, akisaidiwa na Mwanasheria wa Mkoa wa Arusha, Maternus Marandu, kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kuwasilisha hoja za awali za kisheria, kabla ya kusikilizwa kwa maombi ya upande wa utetezi.

Baada ya maombi hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sekela Moshi, alikubali ombi hilo na kuileza mahakama kuwa, kisheria ni lazima hoja hizo zisikilizwe kabla maombi ya barua yaliyowasilishwa mahakamani hapo  na upande wa utetezi, Novemba 14, mwaka huu.

Aidha, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala, akisaidiwa na John Malya, Adamu Jabiri, Charles Adiel, Sheck Mfinanga na Faraji Mangula, walikubaliana na ombi hilo .

Akiwasilisha hoja hizo, Kadushi aliieleza mahakama kuwa, ana hoja mbili za kisheria na kwamba, ya kwanza uamuzi unaopingwa ni mdogo, hivyo hauna tija ya kuomba Mahakama Kuu kupitia majalada ya kesi za jinai.

Kadushi alijenga hoja kwa mifano kadhaa na kuongeza kuwa, mahakama inafungwa mikono kupitia maombi madogo katika kesi za jinai.

Hoja ya pili ni kuwa maombi hayo hayakidhi matakwa ya kisheria kulingana na sheria namba 359(i), kifungu kidogo cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura (20), kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kadushi alidai sheria hiyo inaelekeza kuwa, mtu asiporidhishwa na mahakama za chini, anatakiwa kukata rufani mahakama kuu.
Kulingana na hoja hiyo, upande wa utetezi kama haukuridhishwa na maamuzi ya mahakama, walitakiwa kukata rufani badala ya kuandika barua.

“Kama upande wa waleta maombi hawakuridhishwa na maamuzi ya mahakama ya hakimu mkazi juu ya upande wa Jamhuri kutia nia ya kukata rufani dhidi ya dhamana ya mteja wao, walitakiwa kuomba rufani na si kuandika barua ya maombi,”alidai.

Kadushi alitumia fursa hiyo kuukumbusha upande wa utetezi kuwa, katika sheria, hakuna mbadala wa kusema kuwa unataka kukata rufani au kupeleka maombi na kwamba, katika barua yao ya maombi, hakuna sehemu hata mstari mmoja walipoomba rufani.

“Upande wa utetezi ulitakiwa kukata rufani na pia wangeweza kuleta kiapo cha kukata rufani mahakamani, lakini mpaka sasa hawajaonyesha nia ya kufanya hivyo, lakini napenda kuwakumbusha kuwa bado milango iko wazi,”alidai Kadushi.

Baada ya hoja hizo, Jaji Sekela alitoa nafasi kwa upande wa utetezi ili kujibu hoja za upande wa Jamhuri, ambapo Kibatala aliiomba mahakama kupata tafsiri ya pingamizi la awali na kusema hoja za upande wa Jamhuri hazikidhi pingamizi la kisheria.

Kibatala alidai kifungu namba 372  cha sheria ya uendeshaji wa mashauri ya jinai (CPA), kinaeleza bayana mamlaka ya mahakama kuu ya kuitisha jalada na kuangalia mwenendo, hukumu na maamuzi yanayofanywa na mahakama za chini.

Aliongeza kuwa sheria hiyo pia katika kifungu cha 373, kinaleza ni namna gani mahakama kuu inaweza kupata taarifa za mapungufu ya maamuzi katika mahakama za chini.

“Leo tumekutana hapa kwa ajili ya kusikiliza maombi yetu tuliyowasilisha mahakama kuu na kupokewa, lakini cha ajabu kabla maombi hajasilizwa, upande wa Jamhuri unaiwekea hadi mahakama pingamizi la kusikiliza maombi kwa madai wana hoja za awali.

“Hayo siyo mapingamizi ya hoja za awali, ni sawa na mwananchi yeyote kulalamika kuhusu maamuzi ya mahakama za chini, halafu akamwandikia jaji mfawidhi  barua, halafu jaji akaitisha faili hilo na kupitia maamuzi hayo na sisi ndicho tulichokifanya,”alidai Kibatala.

Aidha, alidai mahakama ilishindwa kusimamia kikamilifu sheria kwa kuwa mtuhumiwa alikuwa ameshapewa dhamana, lakini kabla ya kutoa masharti ya dhamana, upande wa Jamhuri ulisimama na kuileza mahakama kuwa, una nia ya kukata rufaa ya mdomo, jambo ambalo siyo sahihi.

“Kutokana na hoja hizo, mahakama ikitoa dhamana, lazima uweke masharti na hoja yangu hapa ni kwamba, mahakama kuu ina mamlaka ya kuingilia na kurekebisha kasoro hizo.

“Hapa hatuviziani ili tushinde, marejeo ya majalada hayawezi kuombwa kama haikuwa haki pamoja na marejeo. Ni tuhuma nzito kwa mahakama ya chini kushindwa kusimamia mamlaka yake. Hapa ni zoezi, kuna zoezi linafanywa na mahakama kuangalia mapungufu ya kisheria,” alisema.

Baada ya hoja hiyo, Kibatala aliiomba mahakama kutupa hoja hizo mbili za awali kwani hazina mashiko ili maombi yao yaweze kusikilizwa,  ikiwa ni pamoja na upande wa Jamhuri kulipa fidia ya gharama leo.

Kufuatia hoja hizo, Jaji Sekela alitoa nafsi tena kwa upande wa Jamhuri kujibu hoja zilizowasilishwa na Kibata, ambapo Kadushi aliendelea kusisitiza kuwa, upande wa utetezi bado una nafasi ya kukata rufaa dhidi ya pingamizi la dhamana ya mateja .

Aidha, alisema mifano yote ya kesi za mahakama ya rufaa aliyoitoa mahakamani hapo, ina mashiko, ambapo alisoma vifungu mbalimbali vya kisheria kutetea hoja zake .

Pia, alitumia fursa hiyo kuileza mahakama kuwa, endapo itapokea maombi ya barua kwa ajili ya kufanya mapitio ya majalada ya kesi za mahakama ya chini, ni dhahiri kuwa kutakuwa hakuna rufaa zitakazokuwa zinakatwa na kwamba, watu watakuwa wanaandika maombi ya barua pekee.

Aidha, aliendelea kuisisitiza mahakama kutupilia maombi ya barua ya upande wa utetezi na kuendela kuumbusha kukata rufaa kama hawajaridhika na pingamizi la dhamana dhidi ya mteja wao.

Hoja za pande zote mbili zilimalizika saa 7;25 mchana,  ambapo Jaji Sekela aliuleza upande wa Jamhuri na utetezi kuwa, hoja za kisheria walizowasilisha mbele ya mahakama hiyo ni nyingi na kwamba, anahitaji muda kuzipitia kwa makini, ambapo aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 22,  mwaka huu, ambapo ataamua kama maombi ya upande wa utetezi yatatupwa au yatasikilizwa.

“Hoja ni nyingi za sheria mlizowasilisha mbele ya mahakama hii  pande zote mbili naomba muda kuzipitia ambapo Jumanne ya Novemba 22, mwaka huu, nitatoa maamuzi ya hoja mbili zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri,"alieleza.

Awali, Lema alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha, Novemba 6, mwaka huu, akituhumiwa kwa kesi mbili za uchochezi namba 440 na 441 za mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment