Wednesday, 16 November 2016
WALIOISALITI CCM WASIGOMBEE TENA UONGOZI
NA JOSEPH MANYONYI, BUNDA
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Mkoa wa Mara, Amueli Magabe, amewataka waliokisaliti Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu uliopita, wasichukue fomu za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Chama unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Magabe, alisema hayo juzi, wakati akizungumza katika kikao cha ndani cha viongozi wa matawi na kata ya Nyamanguta, wilayani Bunda, mkoani Mara.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa, Jeremia Wambura, ambaye yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mara kwa lengo la kuimarisha uhai wa CCM na jumuia zake.
Alisema wanachama waliokisaliti Chama hawakuwa waaminifu, wamevunja kanuni, maadili na katiba ya CCM, hivyo hawafai kuwa viongozi kwa kuwa walichangia kupunguza kura za Chama katika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Wambura, alisema CCM ni Chama kilicholeta uhuru kwa amani na utuluvu, hivyo hakuna budi utaratibu huo uenziwe kwa ajili ya maslahi ya taifa.
Aidha, mjumbe huyo alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Aliwataka viongozi wa jumuia hiyo, kusimamia maadili na malezi bora ya watoto, sambamba na kuwapeleka shule, kukuza elimu, kutunza na kuhifadhi mazingira ya nchi ili kutekeleza kazi za jumuia ya wazazi kama ilivyoainishwa kwenye kanuni.
Katibu wa jumuia hiyo mkoani Mara, Robert Manjebe, aliipongeza serikali kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kununua ndege, ambazo zitachochea kasi ya maendeleo ya uchumi wa taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment