Wednesday 2 September 2015

SAMIA APATA MAPOKEZI MAKUBWA DODOMA






NA EPSON LUHWAGO, MPWAPWA 

MGOMBEA mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, jana alipata mapokezi makubwa katika Wilaya za Chilonwa, Kongwa  na Mpwapwa akiwa katika kampeni mkoani Dodoma.
Katika mikutano yake hiyo iliyofanyika jana kwenye vijiji vya Nzali (Chilonwa), Chigwingwili (Kongwa) na Mazae wilayani Mpwapwa, melfu ya wananchi walijitokeza, hivyo kuonyesha dhahiri kwamba Dodoma ni ngome ya CCM.
Wakati wote wa mikutano wananchi walikuwa wakishangilia, huku vikundi mbalimbali vya ngoma na kwaya vikitumbuiza kwa ngoma za kabila la Kigogo na nyimbo ambazo zilikuwa zikihamasisha Watanzania kuichagua CCM.
Licha ya kukusanya maelfu ya watu, pia imevunja rekodi za mikutano yote aliyoifanya tangu kuanza kwa kampeni zake kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na Dodoma.
Kadhalika, wananchi waliofika kwenye mikutano hiyo walikuwa wakishangilia na kuonyesha kuwa wako tayari kuichagua CCM katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Mbali na utayari huo, hata viongozi wa maeneo hayo waliopata nafasi ya kutoa neno, walieleza bayana kuwa CCM itaibuka na ushindi wa kimbunga kwa zaidi ya asilimia 95.
Viongozi hao walitanabahisha kwamba CCM itashinda katika nafasi zote za urais, ubunge na udiwani kutokana na kufanya kazi nzuri katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Pamoja na utekelezaji wa Ilani, walisema CCM imeteua wagombea wanaokubalika katika nafasi zote na huo ndio mtaji wa kupata kuta nyingi.
Katika kijiji cha Nzali, Mbunge Mstaafu wa Chilonwa, Hezekiah Chibulunje, alisema katika miaka mitano iliyopita, utekelezaji wa ilani umefanyika kwa asilimia 90, hivyo kuendelea kuleta imani kwa wananchi kuichagua CCM.
Naye Mbunge wa Kongwa alisema serikali ya CCM imetekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi zake katika kilimo, maji, elimu, afya, umeme na kilimo licha ya kuwepo changamoto chache ambazo zinashughulikiwa.
AWAKONGA NYOYO WANANCHI
Hotuba za mgombea mwenza huyo katika mikutano yake yote zilikuwa na hamasa kubwa kiasi kwamba wananchi walilazimika kushangilia kutokana na kugusa maeneo muhimu.
Kubwa zaidi, aliwagusa zaidi pale alipoeleza kuwa hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa mkoani Dodoma kwa kuwa serikali imejipanga kuhakikisha chakula kinapatikana kwa wingi.
“Tunajua Dodoma ilikumbwa na ukame katika maeneo mengi hivyo kupata mazao kidogo. Lakini nawahakikishia kuwa serikali ina chakula cha kutosha katika maghala yake, hivyo tutahakikisha wananchi wanakipata kwa bei nafuu ili wasipate matatizo kwa sababu ya njaa,” alisema.
Sambamba na hilo, alisema serikali ijayo ya CCM itapambana na watumishi wasio waaminifu katika sekta ya afya ambao wamekuwa wakiuza dawa na vifaa tiba.
Alisema kazi kubwa ya serikali ijayo ni kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za afya hivyo kuwaondolea wananchi adha ya kwenda kununua kwenye maduka binafsi.
“Ninasikitika sana pale mwanamke anakwenda na mtoto hospitalini na anaandikiwa dawa na daktari lakini anaambiwa hazipo kwa hiyo aende akanunue kwenye duka la dawa. Hii hatutakubaliana hata kidogo iwapo mtatuchagua kuingia madarakani,” alisema. 
Akizungumza katika kijiji cha Nzali, Samia alipongeza kzi nzuri iliyofanywa na wilaya kwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi zilizotolewa kwenye ilani iliyopita.
Hata hivyo alisema kero au changamoto zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi katika miaka mitano ijayo. Moja ya mambo aliyoahidi ni usambazaji wa umeme katika vijiji vyote.
Kero nyingine aliyoahidi kuipatia ufumbuzi ni mgogoro wa mpaka kati ya wilaya ya Chilonwa na Kongwa. Alisema serikali itapima mpaka wa wilaya hizo ili kumaliza tatizo hilo.
Pia alisema tatizo la upatikanaji hafifu wa mawasiliano ya simu litafanyiwa kazi kwa kujenga minara katika maeneo ambayo yamekuwa na changamoto hiyo.
Katika jimbo la Kongwa, alisema kero sugu ya maji inayovikabili vijiji vya ukanda wa juu, itapatiwa suluhu ili wananchi wasiendelee kupata adha ya kutafuta maji kwa kutembea umbali mrefu.
Alisema hayo baada ya Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai, kuwa maeneo hayo hayana maji licha ya kwamba yako karibu ardhini hivyo kinachotakiwa ni kuyachimba na kusambaza kwenye vijiji.
ABOMOA UPINZANI
Katika wilaya ya Mpwapwa, Samia alibomoa kambi ya upinzani baada ya wanachama wanane, wakiwemo waliokuwa wakiisumbua CCM katika baadhi ya maeneo, kujiunga na Chama.
Miongoni mwa wanachama hao walisema wameamua kurejea CCM baada ya kubaini kuwa upinzani hakuna nia ya dhati ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Akizungumza baada ya kuwapokea, Samia alisema hata walev waliobaki wanapaswa kujua kuwa huko waliko ni sawa na nyumba ya kupanga ambako hakuna uhakika wa maisha yao ya kesho.
“Ndugu zangu huko mmechepuka rudini njia kuu CCM ndiko mpango mzima. Wenzenu wanasema sera yao ni kuing’oa CCM. Hivi kuing’oa CCM ni mahitaji muhumu kwa Watanzania? Hawana kitu hao achaneni nao mje CCM ndiko kwenye ahadi za kweli.
00000

No comments:

Post a Comment