Friday, 1 July 2016

SAMIA: VITUO 'FEKI' VYA YATIMA KUFUNGWA


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema serikali inaendelea kuvisimamia kwa ukaribu vituo vyote vya kulelea watoto yatima nchini na vile vitakavyobainika kuwa vinanufaisha wamiliki na  vinaendeshwa bila ubora, vitafungiwa mara moja.

Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Ssalaam, juzi, katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Kampuni ya Chocolate Princess, inayoandaa kipindi cha televisheni cha The Mboni Show, hafla iliyojumuisha watoto yatima 283, kutoka vituo vitano vya mkoa wa Dar es Salaam.

Makamu wa Rais alisema azma ya serikali ni kuona vituo vyote vya kulelea watoto yatima nchini vinatoa huduma bora na inayokidhi mahitaji ya watoto hao na si vinginevyo.

Kuhusu malezi ya yatima, Makamu wa Rais alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwasaidia yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kuwapa elimu bora, upendo na si kuiachia serikali mzigo huo au mashirika yasiyo ya kiserikali.

Aidha, Makamu wa Rais Samia aliiomba jamii kuweka mipango mizuri ya kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa yatima kwa kuwa nao wana haki ya kuishi vizuri kama watoto wengine.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais alikutana na kuzungumza na viongozi wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), ofisini kwake, Ikulu, jijini Dar es Salaam, kuhusu namna ya kuongeza kasi ya kuanzisha  majukwaa ya kuwawezesha wananchi kiuchumi hapa nchini.

No comments:

Post a Comment