Friday, 1 July 2016

UPINZANI TANZANIA BADO SANA-MAJALIWA

SERIKALI imesema kumekuwa na taswira potofu iliyojaribiwa kufanywa na kambi ya wapinzani kwa wananchi katika  bunge lililomalizika jana.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema pamoja na taswira iliyotolewa na kambi hiyo kwa wananchi, haikuweza kufanikiwa.

Alisema taswira hiyo ilitaka kuonyesha kama vile kuna kuminywa kwa demokrasia ndani ya bunge.

“Kwa bahati nzuri wananchi wetu na wadau wa maendeleo wamebaini kuwa  upinzani katika taifa letu bado haujakomaa kisiasa kwa sababu si jambo la kawaida kwa mbunge kuzitoa hoja za bungeni na kuzipeleka mitaani na kisha kujadiliwa huko. Iwapo hilo linawezekana, basi kusingekuwa na umuhimu wa kuwa na bunge,’’ alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kutokana na sintofahamu hiyo kuhusu nafasi ya bunge katika kutunga sheria na kusimamia serikali, alitoa ufafanuzi  kwa wabunge.

Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa ibara ya 100 na 101 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, imetoa haki na kinga kwa wabunge.

Alisema nia ya haki na kinga hiyo ni kuwapa nafasi wabunge kujadili na kuhoji utendaji wa serikali kwa uhuru bila mashaka yoyote ya kuweza kushitakiwa wanapomaliza wajibu wao.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kinga ya aina hiyo haijatolewa kwa mwananchi yeyote nchini na kwa mantiki hiyo, wabunge wamepewa heshima kubwa.

Alisema kitendo cha baadhi ya wabunge kususia vikao vya bunge hakitoi picha nzuri kwa wananchi waliowachagua kuwasilisha  matatizo yao bungeni.

"Hivyo natoa rai kwa waheshimiwa wabunge hao, kutafakari upya uamuzi wao na nawasihi kwa busara zao, waingine bungeni ili kwa pamoja  tuweze kutoa ushauri kwa serikali," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema bunge linaongozwa na Katiba, Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge, hivyo ni vyema zikafuatwa.
 

No comments:

Post a Comment