Friday, 1 July 2016

TUNDU LISSU APANDISHWA TENA KIZIMBANI

MBUNGE Tundu Lissu (Singida Mashariki - CHADEMA), amepandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi.

Wakati Lissu akipandishwa kizimbani jana, mahakamani hapo na kuachiwa kwa dhamana, polisi waliokuwa wamejaa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, waliwatia mbaroni wafuasi watatu wa CHADEMA, waliokuwa wamebeba mabango yakiwa na ujumbe ukiwemo wa ‘dikteta uchwara’.

Lissu (48), alifikishwa mahakamani hapo saa 6.54 mchana, akiwa katika gari la polisi lenye namba T 671 BEQ, aina ya Toyota Land Cruiser, akitokea Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, ambako alikuwa akishikiliwa tangu juzi, kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi.

Mtuhumiwa huyo, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, anadaiwa kutoa maneno hayo Jumanne wiki hii, akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Kisutu, alikokuwa amefikishwa kusomewa mashitaka ya kutoa chapisho la uchochezi kupitia gazeti la Mawio, lililokuwa na kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Jana, ilipotimu saa 7.29 mchana, Lissu alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Dk. Yohana Yongolo, ambapo Wakili wa Serikali Mkuu, Bernald Kongola kwa kushirikiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga na Salum Mohamed walimsomea shitaka hilo.

Wakili Kongola alidai Lissu anakabiliwa na shitaka la kutoa maneno ya uchochezi kinyume na Sheria ya Makosa ya Magazeti, ambalo anadaiwa kulitenda Jumanne wiki hii, katika Mahakama ya Kisutu, iliyoko wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Alidai mshitakiwa huyo kwa nia ya kushawishi na kudhalilisha wananchi wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali ya serikali, alitoa maneno ya uchochezi yasemayo; “Mamlaka ya serikali mbovu ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa kila Mtanzania kwa nguvu zote, huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi inaingia ndani ya giza nene.”

Baada ya kusomewa shitaka hilo, Lissu anayetetewa na jopo la mawakili 11, wakiongozwa na Michael Ngalo, alikana shitaka hilo na kutamka maneno hayo.

Wakili Kongola alidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliiomba mahakama kumpatia dhamana mshitakiwa kwa kuwa shitaka linalomkabili, linadhaminika kwa mujibu wa sheria na ana wadhamini wa kuaminika na pia ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na alienda kuripoti polisi mwenyewe.

Kwa upande wake, Wakili Kongola alidai hana pingamizi juu ya dhamana, lakini alitoa angalizo kwa mahakama kwamba izingatie mshitakiwa alishitakiwa Jumanne wiki hii, katika kesi ya jinai namba 208 ya mwaka huu, akiwa na wenzake watatu katika mahakama hiyo na akadhaminiwa.

Alidai akiwa ndani ya mahakama hiyo, mtuhumiwa huyo alitoa maneno ya uchochezi, hivyo kwa upande wao wanaona ni mtuhumiwa mzoefu hana hofu na mahakama.

Akijibu hoja hizo, Wakili Kibatala alidai cha msingi ni kwamba upande wa Jamhuri hauna pingamizi na dhamana, hivyo hoja nyingine zitupiliwe mbali.

Mahakama iliridhika na wadhamini wawili waliojitokeza kumdhamini Lissu, ambao ni Diwani wa Viti Maalumu, Rose Moshi na Mbunge mwenzake, Suzan Lyimo.

Hakimu Dk. Yongolo alitoa masharti ya dhamana, ambayo ni kila mdhamini kutia saini dhamana ya sh. milioni mbili na  mshitakiwa kutotoka nje ya nchi bila ya kibali cha mahakama.

Lissu aliachiwa kwa dhamana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Agosti 2, mwaka huu kwa usikilizwaji wa awali.

WAFUASI WAWILI WADAKWA

Baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, viongozi wa CHADEMA, akiwemo Mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe,  walikusanyika na wafuasi wao wakati Lissu alipotaka kuongea juu ya shauri hilo.

Wakati Lissu akizungumza, baadhi ya wanachama wa chama hicho waliamua kuonyesha mabango juu, jambo lililowalazimu polisi kuanza kuwakamata waliokuwa wameshika mabango hayo.

Polisi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia na wale waliokuwa wamevalia sare, walifanikiwa kuwatia mbaroni wanachama watatu na kuwapandisha katika moja ya magari yao sita yaliyokuwepo mahakamani hapo, lenye PT 1848 aina ya Toyota Land Cruiser na kuondoka nao Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Baada ya kuona hali hiyo, viongozi hao wa CHADEMA na wanachama wao wengine waliamua kuondoka huku magari ya polisi takriban nane yaliyokuwa na askari wengine wakiwa na silaha, yaliondoka na gari la maji ya kuwasha, ambalo lilikuwepo nje ya ukuta wa mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment