Friday, 1 July 2016

WATENDAJI MARUFUKU KUJIPA UWAKALA-MAJALIWA

SERIKALI imepiga marufuku watendaji wake, hasa katika halmashauri, kujipa uwakala wa kukusanya mapato kwani ni kinyume na taratibu za kiutumishi.

Mbali ya hilo, halmashauri zote nchini zinatakiwa kuanza kutumia mfumo wa kieletroniki katika kukusanya mapato na malipo kuanzia leo.

Waziri Mkuu, Kassim Mjaliwa, alisema hayo jana, alipokuwa akihitimisha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majaliwa alisema kwa kufanya hivyo, ni kosa kwani sheria zinakataza mtumishi kufanya biashara na taasisi yake.

Alisema hatua hiyo inachukuliwa ingawa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa sura 290, inazipa mamlaka serikali za mitaa kutoza na kukusanya kodi, ushuru na ada mbalimbali.

Alisema katika kufanya hivyo, halmashauri hutumia mawakala, ikiwa ni mikakati ya kuboresha  ukusanyaji wa mapato na kutoa muda mwingi kwa watumishi wa halmashauri kuhudumia wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imebaini kuwa wakati mwingine watumishi wenyewe wanajipa uwakala kinyume na taratibu zinaomzuia mtumishi kufanya biashara na taasisi yake.

Alisema si kila chanzo cha mapato ya halmashauri kitakusanywa  kwa kutumia mawakala, hivyo  halmashauri zitaelekezwa kwa waraka ni vyanzo vipi vinahitaji kutumia mawakala.

“Baadhi ya vyanzo vya mapato vitatakiwa kukusanywa na halmashauri yenyewe kwa kuzingatia miongozo itakayotolewa na serikali,’’ alisema.

Aliongeza kuwa moja ya miongozo hiyo ni kuwa, kuanzia sasa ama kwa kutumia mawakala au halmashauri zenyewe, ni lazima fedha zinazokusanywa ziwekwe kwenye akaunti ya halmashauri na kutumia mfumo wa kielektroniki ili kupunguza au kumaliza masuala ya ‘Cash Transaction’.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema halmashauri zikubaliane na wakala ni kiasi gani cha asilimia za makusanyo kitalipwa kwa wakala na malipo yafanyike baada ya kukusanya na kuingizwa kwenye akaunti. 

MAHAKAMA YA MAFISADI.

Kuhusu mahakama hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema inaanza kazi rasmi leo.

Alisema kuanza kwa mahakama  hiyo ni sehemu ya kupambana na rushwa na ufisadi, ikiwa ni ahadi ya Rais Dk. John Magufuli.

“Tulipoanza mapambano haya, baadhi ya watu walidhani kuwa ni nguvu ya soda tu, si kweli hata kidogo, zoezi hili ni endelevu,’’ alisema Majaliwa.

Aliongeza kuwa kupitia mahakama hiyo, mashitaka ya rushwa na ufisadi yatasikilizwa kwa muda mfupi.

Waziri Mkuu alisema majaji watakaosikiliza mashauri hayo watakuwa na uelewa mpana zaidi kuhusiana na sheria za kushughulikia masuala ya rushwa.

Alisema uwepo wa mahakama hiyo utaimarisha  zaidi taasisi za uwajibikaji nchini zinazoshughulikia mapambano dhidi ya rushwa kama vile TAKUKURU.

“Kuanzishwa kwa mahakama hii kutawafanya watu waliozoea rushwa na ufisadi kujiuliza mara mbili kabla ya kufanya uharifu huo,’’ alisema.

Aidha, alisema viongozi ni lazima waepuke vitendo vya rushwa, mgongano wa maslahi, unyanyasaji wa kijinsia, kuomba na kupokea rushwa, kushawishi na kujipatia maslahi ya kifedha yasiyostahili.

Alisema serikali ya awamu ya tano haitasita  kuchukua hatua stahiki kwa viongozi wa umma au watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma, hivyo kuzingatia maadili si suala la hiari bali ni lazima.

UPATIKANAJI WA SUKARI.

Akizungumzia upungufu wa sukari hapa nchini,  Waziri Mkuu Majaliwa alisema hadi kufikia Juni 9,  mwaka huu, tani 23, 874.6 za sukari zilikuwa zimeingizwa nchini.

Alisema hadi Juni 30, mwaka huu, tayari tani 63,000 za sukari zimeingizwa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali.

Alisema pamoja na kuingizwa kwa sukari hiyo nchini, bado soko la sukari limeendelea kuyumba kutokana na hisia tu kuwa sukari haitoshi.

Waziri Mkuu alisema serikali imejipanga kuondokana na tatizo hilo kwa kuweka mikakati mbalimbali, ikiwemo kufanya tathimini upya ili kujua mahitaji halisi ya sukari.

Pia, alisema kutaanzishwa viwanda vipya vya sukari, ambavyo ni viwanda vya kati vitatu katika wilaya ya Kilosa, Mvomero na Kilombero na viwanda vikubwa maeneo ya Bagamoyo, Rufiji, Kigoma na Kidunda.

UGONJWA HATARI USIOJULIKANA

Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imepeleka jopo la watalaamu wa afya kwenye maeneo ya wilaya ya Chemba yaliyoathirika ili kutambua kiini chake.

Alisema hadi juzi, wagonjwa walikuwa wamefikia 38, na vifo vilikuwa 10 na wengine 35, wamepatiwa huduma za matibabu katika Hospitali ya Dodoma.

Alisema sampuli zimekusanywa na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Maabara ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu  na Maabara ya Hospitali ya KCMC.

Waziri Mkuu alisema hadi sasa sampuli ya aina moja tu ya nafaka ambayo matokeo yake yanaonyesha kuwepo kwa uchafu wa sumukuvu.

Alisema uchunguzi wa samapuli za aina nyingine unaendeleana na serikali inatarajia kuzipeleka Marekani kwa uchunguzi zaidi.

Bunge limeahirishwa hadi Septemba 6, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment