Wednesday, 20 April 2016
UWANJA WA NDEGE WA ZAMANI WA MBEYA WAUZWA
ULIOKUWA uwanja wa ndege wa zamani wa Mbeya, unaokadiriwa kuwa na urefu wa kilometa 2.7, uliopo kata ya Iyela, jijini Mbeya, unadaiwa kuuzwa kinyemela kwa wananchi wa eneo hilo.
Hata hivyo, inadaiwa wakati hayo yakifanyika, serikali ya mkoa Mbeya ilikuwa na taarifa kuhusu suala hilo.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha idadi ya viwanja vilivyouzwa ndani ya uwanja huo wa ndege ni kati ya 60 hadi 70, ambapo jopo la waandishi kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji (TAJATI), lilitembelea uwanja huo na kukuta mawe yaliyopimwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi.
Habari zaidi zilisema viwanja hivyo vyenye thamani ya kuanzia sh. milioni 20 hadi sh.milioni 50, kila kimoja vimegawiwa kwa wananchi, huku ikielezwa mmoja wa wakazi wa eneo hilo, aliyefahamika kwa jina la Mwanguku, kuwa ndiye anayemiliki eneo hilo kabla ya kuanzishwa kwa uwanja huo zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Airport, Enock Mwampagama, alisema ameona uwanja huo umevamiwa huku kukiwa na baadhi ya viwanja vilivyopimwa na baadhi ya watu wakiendelea kulima katika eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pambogo, ambao umepakana na mtaa wa Airport, Esia Edward, alisema mara baada ya kuona eneo hilo linavamiwa, alitoa taarifa serikalini ambako hakupata mrejesho.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Block T, Adrian Majembe, alisema ameona uvamizi mkubwa ukiendelea eneo hilo, lakini hakushirikishwa kwa lolote.
“Nimesikia eneo hilo la viwanja lilikuwa ni la familia ya mtu aliyetambulika kwa jina la Mwanguku, ambaye inadaiwa eneo hilo ni mali ya familia hiyo,” alidai.
Alisema wakazi wa eneo hilo walidai wamegawiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipokuja Mbeya.
‘’Nilisikia watu wakisema wananchi wamegaiwa viwanja na wameruhusiwa kujenga eneo hilo na Waziri Lukuvi,’’alisema Majembe, ambaye aliwahi kuwa Meya wa Manispaa ya Mbeya kati ya mwaka 1994-2000.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iyela, Henry Shipela, alisema alipopata taarifa za uvamizi wa eneo hilo, alifuatilia na kukuta watu wakiwa wanalima na baada ya kuulizia kwa baadhi yao, aliambiwa ni la familia ya watumishi wa uwanja wa ndege.
Alisema atafuatilia kujua sababu zaidi juu ya uvamizi wa uwanja huo.
Akizungumzia suala la uvamizi wa uwanja huo, Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA), Hamis Amir, alisema amesikia suala hilo na kuwa ulikuwa ukitumika awali kabla ya kuanzishwa kwa uwanja wa SIA mwaka 2012.
Hata hivyo, alisema hajui vyema mipaka ya uwanja huo.
Mmoja wa maofisa wa Halmashauri ya Jiji Mbeya, aliyehusika katika upimaji huo, aliyetambulika kwa jina la Ben Mponzi, alisema uwanja huo ulipimwa na Ofisa Mpima Ardhi wa Jiji la Mbeya, Athuman Maugo, ambaye naye alidai eneo hilo lilipimwa kwa idhini ya serikali na si Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Dk. Samwel Lazaro alisema Halmashauri ya Jiji la Mbeya haihusiki na jambo lolote kuhusu uwanja huo wa ndege.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment