Monday, 25 April 2016

UMAARUFU SI KIGEZO KUTEULIWA KUWA KIONGOZI CCM


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema sifa kuu inayozingatiwa katika kumteua kiongozi ndani ya Chama ni uanachama wake na si nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhwavi, alisema hayo juzi, alipofungua mafunzo elekezi kwa madiwani na watendaji wa kata katika Chama mkoa wa Morogoro,yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Usambara.

Alisema Chama katika kumteua mgombea yoyote, kigezo kikuu kinachotumika ni uanachama na sifa zake na si nyadhifa, ambazo aliwahi kuzoshika ndani ya CCM. Luhwavi alisema wakati wanamteua mgombea urais wa CCM, kuliibuka manung’uniko kutoka kwa watu mbalimbali kwamba, aliyeteuliwa hakuwahi kushika nyadhifa yoyote ndani ya Chama.

Kwa mujibu wa Luhwavi, Chama kinaangalia sifa na uwezo wa mwanachama inayemteua kugombea nafasi ya uongozi kama anakidhi vigezo vilivyowekwa na CCM.

“Hilo jambo linatakiwa lieleweke vizuri, lilisemwa sana alipoteuliwa John Magufuli, watu walikejeli, wakati aliwahi kuwa naibu waziri na waziri katika awamu ya nne ya uongozi na awamu ya tatu,”alisema.

Alisema katika awamu hizo za uongozi wake, Chama kilimuandaa vizuri kushika nafasi hizo, ambazo alizitumikia kwa ufanisi mkubwa na kuaminika kwa wananchi.

Akitoa mfano, alisema wakati akiwa Waziri wa Mifugo na Uvivu, Rais Magufuli alionyesha uwezo mkubwa, ikiwa ni pamoja na kutambua idadi ya samaki waliopo baharini, hivyo kuwaongoza Watanzania milioni 50 hakutamshinda.

“Nani ana shaka kuwa JPM ni mwanachama wa CCM, ambaye aliandaliwa na aliingia bungeni na kuteuliwa kuwa naibu waziri na kutokana na utendaji wake, aliweza kupanda na kuwa waziri kamili, lakini watu walikuwa wanauliza alikuwa wapi, kwani hawakumuona?” Alihoji.

Luhwavi alisema tangu Dk. Magufuli alipoingia madarakani, amekuwa akifanya mambo makubwa, ikiwemo utumbuaji wa majipu, kazi ambayo iliainishwa katika Ilani ya Chama ya kupambana na ufi sadi.

Alisema kazi anayoifanya ni kusimamia mapambano hayo, ambayo ni maazimio ya mkutano mkuu wa mwaka 2012, hivyo wapo watakaopona na kujeruhiwa. 


Hata hivyo, alisema Chama hakitamuacha katika mapambano hayo, hivyo ni lazima wamuunge mkono na mabadiliko ndani ya nchi yameandaliwa na wananchi wanatakiwa kutembea vifua mbele kwani kuna mambo mazuri yanakuja.

Alisema Watanzania wapo tayari kwa ajili ya mabadiliko hayo, hivyo Chama kibebe sura mpya kulingana na matakwa yaliyopo.

No comments:

Post a Comment