Monday, 25 April 2016
AMINA SALUM ALI ATEMA CHECHE KWA WATUMISHI ZANZIBAR
WAZIRI wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amewataka watendaji wa Wizara hiyo kuleta mabadiliko katika utendaji wa kazi, ili kuifanya Zanzibar iweze kufikia katika uchumi wa kati.
Alisema kuwa, Wizara imeandaa sera mbali mbali ambazo zinaweza kuifanya Zanzibar kufikia uchumi wa kati, ikiwa ni pamoja na sera ya biashara, viwanda na sera ya mpangokazi ambao utekelezaji wake utaanza leo (jana).
Akizuzungumza na watendaji wa Wizara hiyo pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo tofauti katika ukumbi wa Makonyo Chake Chake, alisema ipo haja kwa watendaji wake kujibadilisha kwa kuwa na sera madhubuti ya kuwa na viwanda vikubwa, ambavyo vitaifanya Zanzibar kufikia uchumi wa kati.
Alieleza suala la kukuza viwanda Zanzibar kuwa, Wizara inataka kukiendeleza kiwanada cha sukari Mahonda, kujenga kiwanda cha maziwa, kiwanda cha Zanzibar Milin na kiwanda cha makonyo ambacho hutoa mafuta ya karafuu, makonyo na mafuta mengine ya mimea.
”Kuna mambo lazima tuyabadilishe, kwanza utendaji wa kazi wa silka ya kawaida ambapo wanataraji matokeo yatakayobadilisha maisha ya wananchi, utendaji utakaotuletea mapato na maendeleo, hii ndio itakayoifanya Zanzibar kufikia uchumi wa kati”, alisema Balozi huyo.
Balozi Amina aliwataka watendaji hao kufanya kazi ya ziada katika kubadilisha Zanzibar na kuwa ya maendeleo zaidi kwa kutumia bidhaa zinazotokana na kilimo.
Alisema kuwa, asilimia 85 ya viwanda Zanzibar ni vya wananchi, hivyo ni vyema juhudi zikatendeka katika kuvibadilisha na kufikia viwanda vikubwa, kwani Zanzibar inayo nafasi kubwa ya kuzalisha na kuuza bidhaa zinazotokana na kilimo.
”Tunatakiwa tufanye kazi ya kuibadilisha Zanzibar kwa kutumia bidhaa zinazotokana na mimea, kwani uzalishaji unataka bidii kubwa, hivyo ipo haja ya kuwashirikisha wa Zanzibar na nje yake kwa kutembeleanaili kuona wenzetu wanafanya nini na sisi tuweze kufuata”, alieleza Waziri huyo.
Waziri huyo alisema, ipo haja ya kutolewa elimu kwa wajasiriamali na kuwezeshwa kwa kupitia sehemu za nje zenye maeneo ya kiuchumi ili kujifunza mambo mbali mbali ambayo wataiga kutoka huko.
”Ili tufikie huo uchumi wa kati ni lazima Serikali ijipange kuwawezesha wajasiriamali na wawekeze kupitia sehemu za wenzao ka kuwatembeza, kupatiwa elimu na soko, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwetu”, alieleza.
Akizungumzia suala la karafuu alieleza kuwa, Zanzibar imefanya vizuri kwa miaka mitano iliyopita kwa uzalishali wa zao hilo, ambapo Serikali imenunua tani elfu 20 kutoka kwa wananchi, ikiwa na thamani ya shilingi billioni 285.89.
”Serikali imejiandaa vizuri na bei itaendelea kuwa ile ile kama alivyoahidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, lengo ni kuivusha Zanzibar kwenda katika uchumi wa kati”, alisema.
Alisema bei ya ununuzi wa zao la karafuu haijashushwa kama baadhi ya wananchi wanavyodai, kwani hiyo ni ahadi ya serikali katika kustawisha maisha ya wakulima wa zao hilo.
Aliwataka wananchi kuacha kabisa uuzaji wa karafuu kwa njia ya magendo na waendelee kuuza hapa Zanzibar, kwani fedha zinapoingia serikalini huwafaa wananchi wenyewe kutokana na huduma za kijamii.
”Pia tufanye biashara inayokubalika kimataifa, karafuu zetu tusuzichanganye na makonyo kwa sababu kuna ushindani mkubwa wa soko, hivyo ni vyema tukazianika sehemu sahihi na kuwa kavu kabisa”, alifahamisha.
Aidha alisema kuwa, Wizara itakuwa na utaratibu wa kuangalia bei ya vyakula na kuhakikisha kwamba vyakula vinavyoingia vinakuwa na viwango vya kimataifa pamoja na usafi.
”Tuko tayari kuingia katika mapambano, kwa nini tusiwe na viwango vya vyakula vinavyoingia wakati nchi nyengine wanavyo, tutahakikisha zinaingia bidha zenye ubora na viwango”, alisisitiza.
Mwandishi wa habari Salim Ali Mselem kutoka redio Istiqama akiuliza swali, alisema serikali itapanga sera ipi ambayo itawawezesha wananchi wote wakati wanapoimarisha upande huu, wananchi hukwama kwa upande wapili.
”Zao la karafuu limeongezwa bei lakini na kodi inaongezeka kwa wafanyabiashara siku hadi siku, jambo ambalo wenye kipato cha chini wanaumia, kwa mfano wafanyabiashara wa sokoni hapa Chake Chake wanatozwa kodi elfu 60 badala ya elfu 30, kweli wananchi wanawezeshwa hivi”, alihoji Salim.
Nae Nasra Mohamedi kutoka ZBC televisheni akitoa hoja yake kuwa, kama iliyoelezwa wajasiriamali wapo asilimia 85, hivyo serikali itafute njia mbadala ya kuwawezesha ili kutumia njia ya digital katika kufanya kazi zao ili kufikia maendeleo zaidi.
Waziri Amina alikuwa kwenye ziara ya kutembelea vitengo mbali mbali vya Wizara, ambapo aliona jitihada mbali mbali zinazofanywa na wajsiriamali na kujionea mambo mbali mbali ambayo hufanywa katika kiwanda cha makonyo Wawi Chake Chake, ikiwa ni pamoja na mafuta yanayotengenezwa kwa karafuu na makonyo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment