RAIS Dk. John Magufuli amemwelezea Dk. Ramadhan Dau, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kuwa ni kiongozi aliyetoa mchango mkubwa kufanikishwa kujengwa kwa daraja hilo.
Dk. Magufuli alisema hayo jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Daraja la Nyerere, uliofanyika katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.
Alisema kumekuwa na mtindo wa kutowatambua watendaji waliofanikisha kutekelezwa kwa miradi mikubwa, hivyo katika kuvunja mwiko huo, Dk. Magufuli alimtaka Dk. Dau kusimama na kueleza machache kuhusu mradi huo.
“Kabla sijazungumza chochote naomba kumkaribisha mtu aliyetoa mchango mkubwa kwenye daraja hilo ambaye ni Dk. Dau. Nimefanya hivi kutokana na kutokuweko kwa utaratibu wa kuwatambua watu waliotoa mchango mkubwa kufanikisha ujenzi wa miradi mikubwa kama hii,” alisisitiza Rais Magufuli.
Akizungumza na wananchi Dk. Dau ambaye hivi karibu aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Balozi, alisema wazo la kujengwa kwa daraja hilo lilitokea Rufiji mkoani Pwani akiwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Alisema ni furaha kushuhudia serikali inatimiza ndoto ya miaka mingi kwa kukamilika kwa daraja hilo na yeye akishuhudia ambalo litasaidia kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
Dk. Dau aliitaka mifuko mingine ya hifadhi za jamii kushindana kwenye uwekezaji wa miradi inayolenga kutatua kero za wananchi.
No comments:
Post a Comment