Friday, 1 July 2016
WABUNGE WATATU CHADEMA WAFUNGIWA
WABUNGE watatu wa CHADEMA wamefungiwa kutohudhuria vikao vya bunge, akiwemo Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini-CHADEMA), ambaye alitoa ishara ya matusi bungeni kwa kuonyesha kidole cha kati cha mkono wa kulia.
Uamuzi huo ulifikiwa jana, ambapo Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alitangaza kumfungia kuhudhuria vikao vitano, James Millya (Simanjiro – CCM) kwa kusema uongo bungeni.
Millya alidaiwa kusema uongo kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi na Walemavu, Jenista Mhangama ni shemeji wa mmoja wa wabia wa kampuni iliyonunua Kampuni ya Tanzanite One, aliyodai ilikuwa ikinyanyasa wananchi.
Hata hivyo, Millya alishindwa kuthibitisha madai hayo licha ya kuwasilisha maandishi kuhusu suala hilo.
Kwa upande wa Kubenea, Naibu Spika, Dk. Tulia alisema anafungiwa kuhudhuria vikao vitano vya bunge kuanzia jana, kwa kusema uongo bungeni.
Alisema Kubenea alidai kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, aliingia mkataba wa ujenzi wa nyumba za makazi ya wanajeshi na kuwa waziri huyo angenufaika.
Dk. Tulia alisema mchango huo alioutoa Mei 10, mwaka huu, ulitoa tuhuma dhidi ya jeshi hilo na kwa waziri, ambaye aliwasilisha malalamiko kwake akitaka Kubenea athibitishe kauli hiyo.
Mei 13, mwaka huu, Kubenea alitakiwa kuthibitisha, ambapo alishindwa,hivyo bunge liliamua kumfungia kutokuhudhuria vikao hivyo.
“Kubenea kashindwa kuthibitisha maneno aliyoyasema bungeni na kwa mamlaka niliyonayo chini ya Kanuni ya 63(8), namsimamisha kuhudhuria vikao vitano vya bunge kuanzia tarehe ya leo (jana),”alisema Naibu Spika.
Kuhusu suala la Mbilinyi, maarufu Sugu, amefungiwa kuhudhuria vikao 10 kwa kusema uongo bungeni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika, alisema hayo wakati akisoma taarifa ya kamati hiyo kuhusu suala la Mbilinyi kutoa ishara ya matusi bungeni.
Alisema kitendo kilichofanywa na mbunge huyo Juni 6, mwaka huu, kimelifedhehesha bunge, wabunge na jamii ya Watanzania na kilifanywa na mbunge mzoefu wa bunge hilo.
Aliongeza kuwa kutokana na vitendo hivyo, mbunge huyo asimamishwe asihudhurie vikao 10 vya bunge la 11, kuanzia jana.
Mkuchika alisema Naibu Spika, Dk. Tulia alipeleka malalamiko dhidi ya mbunge huyo kudharau mamlaka ya Spika kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Alisema kamati hiyo ilikaa Juni 19, mwaka huu na kufanya uchunguzi wa shauri hilo, ulioiwezesha kamati kubaini kuwa mbunge huyo alikiuka taratibu.
Awali, malalamiko hayo yaliwasilishwa kwenye kamati na Jacqueline Msongozi (Viti Maalumu-CCM), ambaye aliomba muongozo kwa Naibu Spika na kuungwa mkono na Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini-CCM), wakilalamikia kitendo hicho cha Sugu.
Hata hivyo, kamati hiyo iliwaita wabunge hao na kutoa ushahidi wao kuhusu suala hilo na Mbilinyi alitoa ushahidi wake na kusema lugha ya alama haina maelezo ya moja kwa moja na kwa uelewa wake ni kwamba, ishara hiyo si tusi bali ni alama ya kupinga jambo lilitokea.
Mbilinyi katika utetezi wake, alikiri kuwa alionyesha kidole hicho kwa kuwa alikasirishwa na mbunge wa CCM, aliyemtukania mama yake matusi ya nguoni, ndio maana alichukua uamuzi huo.
Mkuchika alisema kamati ilitafakari kuhusu utetezi wake na kwamba mbunge huyo hakulalamika kuhusu suala alilolilalamikia na alipohojiwa kuhusu jina la aliyemtukana, hakuweza kulitaja.
Hata hivyo, kamati iliridhika kuwa mbunge huyo alionyesha kidole chake cha kati kwa juu huku akiwa amekunja vidole vingine vilivyobaki.
Alisema kamati ilizingatia mazoea na utamaduni wa mataifa mbalimbali na mazoea na utamaduni wa jamii ya Kitanzania kuhusu ishara iliyolalamikiwa, ambapo jamii hizo hutambua kuwa ishara hiyo ni tusi, hivyo ilimpa adhabu hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment