Friday, 1 July 2016

SERIKALI YAFUTA MAADHIMISHO WIKI YA ELIMU

WAZIRI  wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, amesema kwa mwaka huu, hakutakuwepo na sherehe za maadhimisho ya wiki ya elimu.

Profesa Ndalichako amesema badala yake, fedha ambazo zingetumika kwenye maadhimisho hayo, zitatumika kuboresha miundombinu ya shule.

Waziri huyo alisema  hayo juzi,  mjini Morogoro,wakati akizundua mpango wa ukarabati wa shule kongwe nchini.

Alisema jumla ya sh. bilioni 1.2, zilizotengwa kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho hayo,  sasa zitatumika kukarabati miundombinu ya shule hizo ili kutengeneza mazingira mazuri ya kujifunzia.

Alisema kama hadi mwakani mazingira ya miundombinu ya shule mbalimbali zilizopo nchini yataendelea kuwa katika hali isiyoridhisha, maadhimisho hayo pia yanaweza yasipewe nafasi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMU), Mwalimu Juma Kakonda, aliwataka maofisa elimu mikoa na wilaya watakaopokea fedha hizo, kuhakikisha zinatumiwa katika maeneo yaliyokusudiwa na si vinginevyo

Kwa mara ya kwanza, Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI, iliadhimisha wiki ya elimu Mei 3, hadi 10, 2014, ambapo yaliendelea kufanyika kila mwaka kwa lengo la  kutoa motisha na zawadi kwa shule na wanafunzi wanaofanya vizuri.

No comments:

Post a Comment