Friday, 1 July 2016

HUJUMA NZITO ULIPAJI KODI, KIGOGO ATAJWA, KAMPUNI HEWA 30 ZABAINIKA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imezibaini kampuni kubwa nne zinazojihusisha hujuma ya  ukwepaji wa kodi wa takribani sh. bilioni 30.

Aidha, mfanyabiashara Mohamed Mustapher Yussufali, anashikiliwa na kuhojiwa na TAKUKURU kwa kujihusisha na ukwepaji huo wa kodi.

Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alisema jana kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana TAKUKURU wamebaini kuwepo kwa baadhi ya kampuni na watu binafsi ambao wanajihusisha na ukwerpaji kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi ya mapato kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFD) ambazo hazijasajiliwa na TRA na hutoa risiti bandia.

Alisema kampuni hizo zimekuwa zikinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za EFDs ambazo hazijasaliwa na huzitumia risiti hizo kudai marejesho ya VAT bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa.

Kidata alisema kitendo hicho kinainyima mapato serikali kwa mujibu wa sheria na kwamba TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili kubaini kampuni zinazojihusisha na udanganyifu huo.

Alisema kampuni nne, zimebainika kujihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huo kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2014, ambapo sh. bilioni 29.2 zimebaianika kutolipwa serikalini na kampouni hizo.

Kidata alizitaja kampuni hizo kuwa ni Skol Building Material Ltd ambayo tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2013 haikulipa VAT ya sh. bilioni 5.4 na kodi ya mapato yenye thamani ya sh. bilioni  10.9 na kwamba kodi anayodaiwa ni sh. bilioni 16.4.

Alisema kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Limited, ambayo tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikulipa VAT ya sh. bilioni 5.9 na kodi ya mapato yenye thamani ya sh. bilioni 4.9 ambayo kodi inayodaiwa ni sh. bilioni 10.8.

Kampuni ya A.M.Steel @ Iron Millis Limited kuanzia mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa VAT ya sh. milioni 79.01 na kodi ya mapato yenye thamani ya sh. milioni 113.6 ambayo jumla ya kodi anayodaiwa ni sh. milioni 210.

Kampuni nyinge ni A.M. Trailer Manufacturers Limited ambayo toka mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa VAT sh. milioni 638.2 na kodi ya mapato sh. bilioni 1 ambapo jumla ya kodi anayodaiwa ni sh. bilioni 1.7.

Aliwataka wafanyabiashara kutojihusisha na ununuzi wa risiti za bandia na kudai marejesho ya VAT yasiyostahiki kwa kuwa mamlaka imejithibiti kuendelea na zoezi la kuwabaini wafanyabiashara wanaokwepa kodi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna Valentino Mlowola, alisema uchunguzi wa hujuma hizo unaendelea na kwamba hadi sasa wamebaini kampuni hewa 300.

Alisema kampuni hizo zimepewa siku tatu zilipe kodi inayotakiwa na iwapo hazitalipa zitachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Mlowola alisema taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi wa kuwabaini wafanyabiashara wasiolipa kodi ya serikali akiwemo huyo wanayemshikilia.

No comments:

Post a Comment