Thursday, 30 June 2016

TUNDU LISSU MBARONI TENA


JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limemtia mbaroni  Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za uchochezi.

Lissu alitiwa mbaroni jana  majira ya saa sita mchana na kufikishwa katika Kituo Kikuu cha Kati cha Polisi majira ya saa 7:38, akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokua wamevaa kiraia.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa kituoni hapo akiwa kwenye gari binafsi  lenye namba za usajili T 549 DHH aina ya BMW,  lilokuwa ikiendeshwa na mwanasheria wa CHADEMA, John Malya.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi hilo, zilidai kuwa chanzo cha mwanasiasa huyo kutiwa mbaroni  ni kutokana na kauli za uchochezi alizozitoa juzi  wakati akiongea na waandishi wa habari katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini hapa.

Wakati akifikishwa kituoni hapo,  Lissu alionekana kunywea kwa kuwa mpole huku akimung’unya maneno yasiyoeleweka, tofauti na alivyozoeleka kuwa na purukushani na makeke mengi.

Kabla ya kufikishwa kituo hapo, waandishi wote wa habari waliondolewa na kutakiwa kutoingia ndani ya eneo la kituo hicho.

Amri hiyo ilitolewa na Mkuu wa Operesheni Maalum, Kanda ya Dar es Salaam, Lucas Mkondwa.

Hata hivyo, polisi waliendelea kuzuia waandishi wa habari  kuingia eneo la kituo cha polisi na kutakiwa kubaki nje ya lango kuu hata baada ya  gari ya Lissu kuwasili.

Mtuhumiwa huyo alionekana kutoswa na wana CHADEMA, kutokana na kutoonekana eneo hilo tofauti na ilivyozoeleka ambapo kiongozi akikamatwa, viongozi na wafuasi wa chama hicho hufurika.

Mbunge  Godbless Lema (Arusha Mjini - CHADDEMA)  ndiye pekee aliyeonekana akihaha kumhangaikia kumuandalia chakula bosi wake huyo baada ya kudai kuwa na njaa.

“Nimewauliza polisi, kwamba watamhoji kwa muda gani, wamenijibu kuwa inaweza kuchukua hata saa tatu, hivyo ninaenda kumtafutia chakula,”alisema Lema.

Pamoja na masuala mengine, Lema alikiri Lissu, kutiwa mbaroni  huku akijitetea kwamba kitendo hicho kilikuwa ni cha uonevu.

“Ni kweli   Lissu aliitwa polisi kwa sababu ya kauli alizotoa juzi wakati akitoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusilikiza shauri la kesi ya  gazeti la Mawio,”alisema Lema.

Alitaja sababu zingine zilizomfanya Lissu kuangukia mikononi mwa vyombo vya dola kuwa ni kauli za uchochezi anazodaiwa kuandika kupitia mtandao wa kijamii.

Alijinasibu kuwa baada ya Lissu kutiwa mbaroni  atakayefuata ni yeye.

Hadi majira ya saa 12:00 jioni, Lissu alikuwa bado anashikiliwa kituoni hapo na taarifa zilidai alikuwa ametupwa mahabusu.

Jitihada za kumpata Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda.

No comments:

Post a Comment