Wednesday, 2 September 2015
DK. MAGUFULI: NITAIMARISHA UHUSIANO NA NCHI JIRANI
Na Selina Wilson, Namtumbo
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema akipata ridhaa ya Watanzania kuwa rais, ataimarisha uhusiano na nchi jirani na nchi wafadhili.
Dk. Magufuli alisema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, ulifanyika katika uwanja wa CCM, Wilaya ya Namtumbo.
Alisema serikali ya awamu ya nne imekuwa na uhusiano mzuri wa kimataifa na wadhili, hivyo kazi yake ni kukuza uhusiano huo.
"Nitaimarisha uhusiano na nchi jirani za Uganda, Zambia, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na zingine , ikiwemo pia wafadhili," alisema.
Aliwataka wananchi wachague kiongozi anayeaminiwa na wafadhili ambao wamekuwa wakifadhili miradi ya ujenzi wa barabara na kutumia fedha vizuri.
Alisema amekuwa waziri kwa miaka 20, amesimamia fedha nyingi za miradi ya barabara ambazo zimejengwa na zinaendelea kujengwa nchi nzima.
Akizungumzia raslimali za nchi, Dk. Magufuli alisema Namtumbo kuna madini ya uranium, hivyo atahakikisha anayaendeleza ili yawanufaishe wananchi wote.
Dk. Magufuli alisema kiu ya Watanzania siyo vyama, bali ni maendeleo, hivyo atatumia uwezo wake kuleta maendeleo bila ubaguzi, bila kujali itikadi za vyama.
Alisema ataendelea kujenga barabara za lami na kujenga reli ya kiwango cha kisasa kutoka Mtwara/ Namtumbo/ Songea hadi Mbambabay.
Katika hatua nyingine Dk. Magufuli alikagua ujenzi wa barabara Matemanga/Liuli katika Kijiji cha Ulia, inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Dk. Magufuli alionyesha uzoefu katika ujenzi wa barabara kwa kupanda na kuongoza mtambo wa kutengeneza barabara, ambapo wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya SRBG walimshangilia na kumwahidi kwamba watampigia kura.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Dk. Magufuli aliwataka wafanye kazi kwa uadilifu, bila kuiba mafuta na vipuri na kwamba mkandarasi ameshalipwa na wao watalipwa.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, barabara hiyo inajengwa kwa vipande na wakandarasi wanane na ujenzi wake utakamilika mwakani.
Akiwa katika eneo la Matemanga, aliwahakikishia wananchi kwamba serikali yake itajenga viwanda, ikiwemo cha kubangua korosho, ili kukuza uchumi.
Dk. Magufuli kwa nyakati tofauti aliwanadi wagombea ubunge, Injinia Edwin Ngonyani wa Namtumbo na Injinia Ramo Makani wa Tunduru wapigiwe kura, ili apate safu ya watu wa kufanya nao kazi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment