Tuesday, 1 September 2015
DK. SLAA AIBUKA NA KUMMALIZA LOWASSA
MWANASIASA mwenye ushawishi mkubwa katika upinzani, Dk. Wilbrood Slaa ameibuka hadharani na kusema mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, hafai kuwa kiongozi wa nchi kutokana na kashfa mbalimbali ikiwemo ya ufisadi.
Ametangaza rasmi kuondoka CHADEMA na kustaafu siasa za vyama huku akiahidi kuendelea kuwatumikia Watanzania kutokana na vipawa alivyonavyo.
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kujitokeza hadharani tangu akatae ukiukwaji wa demokrasia ndani ya CHADEMA kwa ajili ya kumbeba mgombea urais wao, Dk. Slaa amesema amechukua uamuzi huo kwa kuwa siku zote huwa hapendi kuburuzwa, kununuliwa wala kujidharaulisha kwa ajili ya kumnufaisha mtu fulani.
Dk. Slaa alitangaza uamuzi wake huo jana, katika Hoteli ya Serena Dar es Salaam, ikiwa ni karibu miezi miwili tangu aliposusia hatua za uteuzi wa mgombea urais wa CHADEMA.
Dk. Slaa alisema Lowassa hastahili kuwa rais wa nchi kwa kuwa ni mchafu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo ufisadi ambao mara nyingi amemkabili bayana na kumweleza msimamo wake huo.
“Nimeamua kujitokeza hadharani kueleza ukweli kuhusu mambo mbalimbali yaliyokuwa yakipotoshwa ikiwemo kuelezwa kuwa eti nimechukua likizo.
“Sikuchukua likizo, niliamua kujiweka kando baada ya kutokubaliana na mambo ya hovyohovyo yaliyokuwa yakiendelea ndani ya CHADEMA kwa ajili ya kumpa nafasi Lowassa agombee urais,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, aliyekuwa akizungumza kwa mifano huku akirudia kumtaka Lowassa na maswahiba zake kujitokeza hadharani kupinga anayoyaeleza, mgombea huyo aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kwa kashfa ya Richmond, hana uwezo wa kutatua kero za Watanzania
Dk. Slaa amesema moja ya sababu zilizomfanya aukatae uamuzi wa kumteua Lowassa kuwa mgombea urais kupitia UKAWA ni kushindwa kwake kutimiza makubaliano waliyofikia.
Alisema mwanzoni alielezwa kuwa Lowassa angejiunga na CHADEMA akiwa na watu makini, wakiwemo wabunge 50, wenyeviti 22 wa CCM wa mikoa na wenyeviti 88 wa CCM wa wilaya.
Hata hivyo, alisema ili kuwatambua watu hao, alitaka apatiwe majina yao ili aweze kujua nafasi watakazogombea katika uchaguzi mkuu ujao, lakini hilo halikufanyika.
"Huwezi kupokea idadi tu ya watu bila kujua majina yao na nafasi watakazogombea katika chama. Hilo halikufanyika hadi Julai 25 nilipotakiwa kuitisha kikao cha dharula cha kamati kuu kilichofanyika Julai 27,"alisema Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, saa chache kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, alipigiwa simu na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na kumuuliza iwapo hajaridhika na uamuzi wa kumpitisha Lowassa kuwa mgombea urais wa UKAWA.
Alisema tangu alipojiunga na CHADEMA, hakuwahi kutofautiana na Mbowe na kuongeza kuwa, ilitokea hivyo wakati wa ujio wa Lowassa ndani ya CHADEMA.
Dk. Slaa alisema kabla ya kufanyika kwa kikao cha kamati kuu, kiliitishwa kikao cha kamati ndogo, kilichomuhusisha yeye, Mbowe, Tundu Lissu na mshenga wa Lowassa, Askofu wa Kanisa la Ufufuo, Gwajima.
Mwanasiasa huyo alisema kikao hicho kilifanyika kuanzia saa tatu hadi saa tisa usiku, lakini kilimalizika bila ya kufikiwa kwa mwafaka kuhusu Lowassa.
"Taarifa zilizotolewa kwamba awali nilikubali jambo hilo, hazikuwa za kweli. Zilikuwa habari za kupotosha na ninawaomba wawe na hofu ya Mungu,"alisema.
Dk. Slaa alisema wakati wa kikao hicho, Mbowe na Lissu walimuomba aende nyumbani kwa Lowassa ili wakajadili na kufikia muafaka juu ya suala hilo, lakini alikataa.
Alisema asingeweza kwenda nyumbani kwa Lowassa, ambaye alikuwa bado mwanachama wa CCM na kuongeza kuwa hiyo ndio sababu ya kikao hicho kuvunjika bila ya kufikia muafaka.
Dk. Slaa alisema kutokana na msimamo wake huo, aliamua kuandika barua ya kujiuzulu uongozi Agosti 10, mwaka huu na kumkabidhi Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara, Profesa Award Safari, ambaye aliichukua na kuichana.
Alisema baadaye alimuandikia barua Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar, ambaye alimweleza wazi kwamba alichokuwa akikifanya ni kujisumbua kwa vile mambo hayo yalishapangwa kipindi kirefu kilichopita.
"Watu wanasema siasa ni mchezo mchafu, lakini kwa mimi niliyesomea mambo haya nasema siasa ni sayansi, haitaki uongo, ulaghai na udanganyifu. Vitu vidogo vidogo vinaondoa uaminifu katika siasa,"alisema.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisema hakuhitaji kuandika barua kuthibitisha kwamba amejiuzulu uongozi CHADEMA kwa vile angeweza kufanya hivyo kwa mdomo kupitia mkutanoni.
Alisema madai kwamba alifungiwa nyumbani na kuzuiwa kutoka na mkewe, Josephine Mushumbuzi hayakuwa na ukweli kwa sababu huo ulikuwa ni uamuzi wake binafsi.
Alimtetea Josephine kuwa ni mwanaharakati mzuri katika masuala ya kisiasa na kwamba ana uchungu na nchi, anazo haki zake na ndio sababu aliwahi kutokwa damu baada ya kukumbana na kipigo kutoka kwa polisi wakati wa maandamano yaliyofanyika mjini Arusha.
Dk. Slaa alisema pia kuwa si kweli kwamba mkewe alikuwa akilipwa na CHADEMA na kwamba tangu mwaka 2010, amekuwa akizunguka naye nchi nzima kukipigia debe chama hicho.
Aidha, Dk. Slaa alisema hakuwa akilipwa mshahara wa shilingi milioni saba na CHADEMA kila mwezi kama ilivyowahi kuripotiwa na vyombo vya habari na kwamba familia yake imekuwa ikiishi kwa kula mihogo na maharage.
"Nina uchungu kama Slaa na familia yangu. Sikuwa nataka hadhi ya chama ichafuliwe. Pia sikuwa nataka jina langu lichafuliwe,"alisema.
Kiongozi huyo wa zamani wa CHADEMA alisema kitendo cha chama hicho kupokea wanachama walioshindwa kura za maoni kutoka CCM hakikuwemo kwenye makubaliano kati yao.
"Hatukuwa tumekubaliana kwamba mbunge aliyeshindwa kura za maoni kama Mahanga (Makongoro-mbunge wa zamani wa Segerea) aje Chadema. Kuna watu wamepata vilema, wametumia fedha zao kwa sababu ya Chadema, halafu waje wengine wapewe nafasi za juu,"alisisitiza.
Alimshangaa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kwa kujitokeza hadharani kumsafisha Lowassa kwa madai kuwa ni mtu safi na mchapakazi.
Alisema binafsi alikuwa hazungumzi na Sumaye baada ya kumshutumu bungeni kutokana na kumiliki shamba kubwa eneo la Kibaigwa mkoani Dodoma na kuwaacha wananchi wakiwa hawana ardhi.
"Leo (Sumaye) anasema Lowassa msafi. Dhambi haiwezi kuhalalishwa kwa dhambi nyingine. Na kama mnakumbuka vizuri, Watanzania walikuwa wakimwita Sumaye ziro. Mnajua ni kwa nini?" Alihoji Sumaye.
Dk. Slaa alisema akiwa kiongozi wa CHADEMA, alitegemea Lowassa angeingia kwenye chama hicho akiwa na viongozi makini na wanaokubalika, lakini kinyume chake waliletewa makapi.
Alisema akiwa kiongozi wa chama hicho, aliwahi kuapa kwamba mwaka huu wasingepokea makapi kutoka CCM, lakini badala yake wamekula matapishi yao wenyewe.
Alimponda aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, aliyejiunga na CHADEMA, Mgana Msindai kwamba ni mzigo na anaufahamu vyema uwezo wake.
"Msindai ni mzigo,namjua A to Z, alikuwa mwenyekitiwangu wa serikali za mitaa bungeni, akijibu nitasema,"alisema Dk. Slaa na kukiri kwamba hafahamu lolote kuhusu mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja.
Akimzungumzia Matson Chizzi, ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi wa uchaguzi wa CCM, Dk. Slaa alisema sifa pekee aliyopelekewa ni kwamba alikuwa mwizi wa kura hivyo akaona amekosa sifa.
Dk. Slaa pia alimponda John Guninita, ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa CHADEMA kabla ya kurejea CCM kwamba, hana uwezo hata wa kuandika ripoti.
"Siitetei CCM, nasema ukweli. Viongozi wangu wamepata kigugumizi. Siongelei CCM, naongelea Chadema,"alisisitiza mwanasiasa huyo.
Dk. Slaa alisema haiwezekani kuiondoa CCM madarakani kwa kuingia mkataba na shetani, kwamba baada ya kukiondoa, mengine yatafuata baadaye.
Alisema kuiondoa CCM kwa staili hiyo hakuwezi kuleta nafuu yoyote kwa vijana na wazee, ambao maisha yao bado ni duni. Alisema kuiondoa CCM madarakani kunataka kuwa na watu makini, wenye uwezo na wanaokubalika.
"Wananchi waliikubali Chadema kwa sababu ilikuwa na misingi isiyoyumba. Leo hii hakuna uadilifu.Mramba (Basil) na Yona (Daniel) walihukumiwa kwenda jela kwa sababu Chadema tulipiga kelele kuhusu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.
"Leo Lowassa anasimama kwenye majukwaa na kuhoji mwenye ushahidi kuhusu tuhuma za Richmond autoe hadharani kwa vile hajafikishwa mahakamani. Kama hawajui siasa ni bora wanyamaze,"alisema.
Dk. Slaa alisema yeyote aliyeshiriki kumpitisha Lowassa kugombea urais kwa tiketi ya UKAWA hana tofauti na mtu anayehalalisha dhambi kwa dhambi nyingine na kwamba anapaswa kufungwa jiwe na kutoswa baharini.
Mwanasiasa huyo alisema kumsafisha Lowassa hivi sasa ni sawa na kuondoa uchafu chooni na kuuhamishia kwenye chumba cha kulala, ambacho hakiwezi kulalika.
"Neno choo ni baya sana, lakini kwa Marekani na Japan ni pazuri kwa sababu ni mahali pa starehe na unaweza kula hata chakula.
"Lakini kwa sisi waafrika, choo ni mahali pa uchafu. Huwezi kujitia ujasiri wa kupakua uchafu wa chooni na kuupeleka chumba cha kulala kwa sababu nacho kitakuwa choo, huwezi kulala, kitakuwa kinanuka,"alisema Dk. Slaa.
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Karatu alisema ajenda ya ufisadi ilikuwa ikikipa nguvu chama hicho, lakini sasa imehamishwa upande mwingine.
Aliwalaumu waandishi wa habari kwa kuandika habari bila kuzifanyia utafiti na hivyo kupotosha ukweli kuhusu suala zima na kashfa ya Kampuni ya Richmond, iliyokuwa ikimkabili Lowassa na kumfanya ajiuzulu.
Alisema akiwa mbunge mwaka 2008, aliwahi kumtaka Lowassa aache kungung'unika, badala yake ajitokeze hadharani na kuwaambia ukweli Watanzania kuhusu kashfa hiyo, lakini alishindwa kufanya hivyo.
Alisema pia kuwa Lowassa aliwahi kumtisha kwamba anaharibu sifa ya serikali, lakini hakuwa tayari kutishika kwa vile aliona afadhali kuharibu sifa hiyo kuliko kuikana dhamira yake.
Dk. Slaa alisema siku ambayo ripoti ya kamati ya bunge iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza kashfa hiyo ilipokuwa ikiiwasilisha bungeni, alifuatwa mapema asubuhi na mtu mmoja na kumshawishi akubali kupokea hongo ya shilingi milioni 500 ili kuzuia ripoti hiyo isisomwe. Hata hivyo, hakumtaja mtu huyo.
"Nilichofanya nilimuuliza kama wewe umepewa milioni 500 uniletee mimi, wewe unazo ngapi? Niliwaambia Lowassa na Sumaye, rushwa ni dhambi inayoanzia kichwani,"alisisitiza.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, Lowassa hawezi kukwepa kashfa hiyo kwa sababu ripoti ya kamati ya bunge, iliyokuwa chini ya Dk. Harrison Mwakyembe, ilimtaka aidha ajipime kama anastahili kuendelea katika wadhifa huo au akubali bunge liijadili na kutoa uamuzi.
Alisema kitendo cha Lowassa kukubali kujiuzulu, kilidhihirisha wazi kuwa alikwepa aibu ya kutimuliwa madarakani na bunge.
"Lowassa anagombea urais, hawezi kwa sababu ni muongo na haaminiki,"alisisitiza Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa kuna wakati aliwahi kumwita kwenye ofisi ya spika akiwa bungeni na kumtolea kauli ya kitisho kuhusu taarifa ya Richomond, lakini alimsisitizia msimamo wake wa kumwita fisadi wa moyo na kichwa.
Akirejea ripoti ya Dk. Mwakyembe, alisema kampuni ya Richmond, iliyoshinda tenda ya kuiuzia TANESCO umeme, haikuwa imesajiliwa mahali popote na kwamba usajili wake ulikuwa wa kitapeli.
"Waziri mkuu alikuwa anajua yote haya, na kama hajui basi ni mzembe na hafai kuwa rais,"alisema Dk. Slaa.
Alisema tumaini jipya kwa Watanzania haliwezi kujengeka kwa ahadi za uongo na kuwataka vijana kuepuka siasa za ushabiki.
"Tuache ushabiki. Nina uchungu mkubwa. Chadema ninavyoiona, niliyoshiriki kuijenga, leo inatumia mabasi kuwapeleka watu kwenye mikutano na watu kutamba kwamba mafuriki hayazuiliki. Siko tayari na siwezi kuwa zezeta,"alisema Dk. Slaa.
Alisema ajenda kubwa ya CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka huu ilikuwa rushwa na uadilifu, lakini hayo yote kwa sasa hayawezekani kutokana na uamuzi wa kumteua Lowassa kuwa mgombea urais.
"Rushwa ndiyo iliyotufanya tufike hapa tulipo, tuna njaa na fedha iliyopo inaingia mifukoni mwa wachache. Wananchi walituamini, lakini leo agenda hiyo tuna kigugumizi cha kuizungumza,"alisema.
Alisisitiza kuwa Lowassa hawezi kuizungumzia Ilani ya CHADEMA kwa vile hakushiriki kuiandaa kwa vile iliandaliwa miezi kati ya 10 na 12 iliyopita.
"Unajengaje maadili ukiwa na watu waliohusika na uchafu. Scotland Yard iliwahi kutuandikia tuchunguze dola milioni 400 Lowassa amezipata wapi. Leo tunamtetea. Mimi nina ushahidi wa yote ninayoyazungumza. Siwezi kuupeleka mahakamani kwa sababu kesi hupelekwa mahakamani na serikali. Kesi ya jinai haina mwisho,"alisema.
Dk. Slaa alisema hadi leo watanzania wanakamuliwa jasho lao kwa kuilipa mamilioni ya fedha Kampuni ya Dowans, iliyorithi deni la TANESCO kutoka Richmond, wakati kampuni hiyo haipo na haikuwahi kusajiliwa kokote duniani.
"Nitaendelea kubaki na msimamo huo na hata wajukuu zangu watakapokuja kuchimba kaburi langu, watasema nilikuwa sahihi,"alisema.
Dk. Slaa pia aliponda ahadi zilizotolewa na Lowassa kwenye mikutano yake ya kampeni ya kuwatoa jela mwanamuziki Nguza Vicking 'Babu Seya', aliyefungwa maisha baada ya kupatikana na hatia ya kuwabaka watoto wadogo na mashekhe wanaoshitakiwa kwa tuhuma za ugaidi.
Alisema kauli hiyo ya Lowassa inaonyesha wazi kuwa akili yake haiko sawa hivyo anahitaji kupimwa na madaktari kwa vile rais hana uwezo wa kufuta kesi ama kutoa msamaha kwa wafungwa waliohukumiwa kwa makosa ya ubakaji.
Pia alimshangaa Sumaye kwa kujitokeza hadharani kuwatetea mashehe hao wakati ni yeye aliyetoa amri kwa polisi kuingia kwenye msikiti wa Mwembechai wakiwa na mbwa kwa ajili ya kupambana na waislamu.
"Ukiumwa na nyota, ukiona jani ulikimbie. Tunapozungumzia utendaji uliotukuka, tunapaswa kuangalia kwa kufanya utafiti,"alisema na kuwataka wanahabari wasiwe makasuku wa kuripoti habari bila kuzifanyia utafiti.
Alisema Sumaye na Lowassa hawana sifa za kuwa viongozi wa nchi na kwamba Sumaye anashidwa kufika Mvomelo anakomiliki mashamba makubwa wakati hisa za Lowassa kwenye kampuni mbalimbali hazijaandikishwa kwenye Tume ya Maadili.
Dk. Slaa pia alieleza kusikitishwa kwake na uamuzi wa Kanisa la Kilutheri na baadhi ya mapadri wa Kanisa Katoliki kukubali kununuliwa kwa pesa ili wamuunge mkono Lowassa katika kampeni za kuwania urais.
Alisema kama ni kweli mapadri wa kanisa Katoliki wamehongwa ili kumuunga mkono Lowassa, wakae chini, wajitafakari na kujipima ili kuliokoa Taifa kwa vile linakwenda pabaya.
Alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa baadhi ya mapadri wamehongwa kati ya shilingi milioni 60 hadi 300 ili wamuunge mkono Lowassa na kwamba huko ni kulidhalilisha kanisa.
"Kama ni kweli, taifa letu limekwisha. Kaeni chini, pigeni magoti mtubu,"alisema.
Dk. Slaa amesema hayuko tayari kuona Tanzania inaongozwa na rais mwongo na asiye mwaminifu na kwamba ataendelea kupiga kelele ili jambo hilo lisitokee.
Alisema hajawahi kupata vitisho kama wakati huu, kuliko ilivyokuwa wakati wa sakata la Richmond, lakini hilo haliwezi kumfanya awe na woga wa kuwatetea wananchi na kuipigania nchi yake.
"Nimestaafu siasa, sina chama, lakini hii haina maana kwamba sina nchi. Mimi ni Mtanzania na nitaendelea kuwa mtetezi wa wananchi kwa kutumia vipawa nilivyojaliwa na Mungu,"alisema na kumshukuru Mungu kwa kumjalia vipawa hivyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment