WANACHAMA wa CCM wenye malengo ya kugombea nafasi za uongozi wa Chama mwakani, kwa kutumia nguvu ya fedha, wametakiwa kutojaribu kuchukua fomu hizo kwa sababu hakuna nafasi yao CCM.
CCM imesema kwenye uchaguzi wake mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani, maadili na miiko ya Chama itazingatiwa kwa kiwango cha juu ili kutotoa nafasi kwa bora viongozi kushika wadhifa.
Imesema kama misingi yake ilivyo, CCM haina nafasi kwa fisadi, mla rushwa na anayetumia fedha kupata madaraka, kwa sababu safu ya uongozi inayotumia fedha haina uadilifu na uwajibikaji.
Aidha, imesema inachokiamini ni kwamba, safu yoyote ya uongozi iliyotumia fedha kupata madaraka, ina chanzo cha fedha hizo na mwisho wa siku itakitumikia chanzo hicho na si kuwatumikia walio wengi.
Kauli hiyo ilitolewa jana, mjini Babati mkoani Manyara na Msemaji wa CCM Taifa, Christopher Ole Sendeka, wakati akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Manyara.
Alisema kiapo cha CCM kinakataa rushwa ndio sababu Chama hakitamsaidia kwa namna yoyote mwanachama au kiongozi atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
"Mwanachama au kiongozi wa CCM atakayebainika kujihusisha na rushwa kwa namna yoyote, Chama hakitamsaidia wala kumtetea.
"Sana sana tutaziomba mamlaka zinazohusika zimpe mhusika adhabu kali kwa sababu kakiuka sheria za nchi na maagizo ya Chama chake," alisema.
Ole Sendeka alimaliza ziara yake mkoani Manyara kwa kutembelea wilaya za Babati Mjini na Vijijini, ambako alifanya mikutano miwili mikubwa ya hadhara na leo anaendelea na ziara hiyo mkoani Singida.
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Manyara, wamekitaka Chama kumwajibisha yeyote atakayebainika kuhusika na hujuma ya kuchoma moto jengo la ofisi za CCM mkoa huo, lililoko mjini Babati na kusababisha hasara za mamilioni ya fedha.
Wakizungumza juzi mjini Babati, kwenye mkutano wa ndani, uliofuatiwa na mkutano
wa hadhara, uliofanyika eneo la Mji Mpya, wajumbe hao walimsihi Msemaji wa CCM
Taifa, Christopher Ole Sendeka, kupeleka ujumbe Taifa kuwa moto ule ni hujuma.
Kauli hiyo inakuja wakati tayari kumeundwa kamati maalumu ya ujenzi iliyopewa
majukumu ya kufanya ukarabati wa jengo hilo lenye ghorofa moja, ikiongozwa na
Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa mkoa wa Manyara, Amaan Hivji.
Moto huo uliozuka kwenye jengo hilo la Makao Makuu Mkoa Machi 7, mwaka huu,
ambapo kwa mujibu wa Katibu wa CCM mkoa, Ndeng’aso Ndekubali, uliunguza nyaraka
na mali zingine za CCM, ambazo thamani yake bado haijajulikana.
“Kiongozi wetu umekuja umeona majanga yaliyotupata, tunasema hivi, hii haikuwa
ajali, ukawaambie makao makuu ni mwendelezo wa chuki za uchaguzi mkuu, tena
baadhi ya viongozi wetu wa CCM wamehusika, wawajibishwe,” alisema mmoja wa
wajumbe.
Aidha, walisema licha ya kwamba vyombo vya usalama vinaendelea na uchunguzi,
CCM ni vyema ikaanza upelelezi wa chini chini, ikisaidiana na polisi ili
kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa sababu
hawavumiliki.
Wajumbe hao waliokuwa wakizungumza kwa hisia kali, walisema CCM Babati ina
majipu lukuki, ambayo yalichangia kushurutisha wananchi kutokuwapigia wagombea
wa CCM kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana, kwa madai kuwa hawafai kuongoza.
Walisema ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi wa Chama anaendekeza fedha na
ahadi alizoahidiwa na upinzani, ikiwemo cheo endapo wangeshinda, ikiwemo ukuu
wa wilaya na mkoa na kusahau wajibu wake kwa CCM na Watanzania.
“Mwaka jana tulitaabika sana, tunakesha kuomba kura nyumba kwa nyumba, mwisho
wa siku tunaambiwa mbona nyie mnahangaika wakati kuna baadhi ya viongozi wenu
wanatuambia tusiwape kura kwa kuwa watu mliosimamisha kugombea hawafai.
Inaumiza sana,” alisema Chrispin Msacky.
Wajumbe hao walisema hakuna haja ya kuficha na kuleana kwa sababu madhara
waliyoyapata ni makubwa, ikiwemo kupoteza jimbo la Babati Mjini, hivyo endapo
Chama kitahitaji msaada kutoka kwao, ikiwemo kuwapa majina ya wasaliti, watatoa
ushirikiano.
"Majina mbona tunayo, tutawataja mkituhitaji kufanya hivyo kwa sababu kanuni ni
kwamba Chama kwanza, mtu baadaye. Wamechangia sisi kushindwa kiti cha ubunge na
tumepoteza halmashauri ya mji.
“Kama
vile haitoshi wanatuchomea ofisi na bado wako ndani ya CCM, hapana haikubaliki,
utumbuaji majipu uhamie Chamani, kwaniniunacheleweshwa? Hatutaki unafiki,
tumeamua kujijenga upya, tunahitaji
watu safi,” alisema mmoja wa wajumbe.
Walitumia nafasi hiyo kumweleza Ole Sendeka, ambaye alikamilisha ziara yake
mkoani humo juzi, kuwa Babati ina tatizo la mpasuko ndani ya CCM, ambao
ulitokana na vita za uchaguzi uliopita, hivyo ni lazima lifanyike jambo
kurudisha uhai.
Akijibu michango ya wajumbe hao, Ole Sendeka, ambaye kabla ya kikao hicho
alitembelea jengo hilo kuona hasara za tukio hilo, alisema ni tukio la
kusikitisha ambalo Chama kinatoa onyo kwa atakayebainika.
“CCM inawapa pole Wana Manyara kwa kuunguliwa na jengo hili. Ni tukio baya sana,
nimepita, nimeona sasa tuwaachie wenzetu wa ulinzi na usalama, lakini tunatoa
onyo kwa yeyote atakayebainika kuhusika na
hujuma hii,” alisema.
hujuma hii,” alisema.
Alisema kuhusu mpasuko, CCM inaendelea na mchakato wake kikatiba kufanya
tathmini ya uchaguzi uliopita kwenye mikoa mbalimbali, ambapo kwa Manyara zamu
yake ikifika maamuzi yatatolewa kwa mujibu wa katiba ya Chama.
“Tunawapa pole kwa hali hii inasikitisha, Chama kinaendelea na taratibu zake,
lakini nyie kwa kutumia kamati zetu za siasa, ambazo ndio injini ya Chama ngazi
za mikoa na wilaya, fanyeni upembuzi kwa uadilifu wa hali ya juu na asionewe
mtu,” alisema.
Aliwataka wajumbe hao kushikamana kwa umoja wao katika kukirudisha Chama kwenye
misingi yake ya kuwa kimbilio la wanyonge na kushirikiana kutafuta namna ya kukamilisha
ukarabati wa jengo la ofisi za mkoa, kama ulivyo mkakati wa CCM kufanya ofisi
za mikoa na wilaya kujitegemea kiuchumi.
No comments:
Post a Comment