SERIKALI imesema
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), anafanya uhakiki wa
madeni ya serikali, ambapo amebaini kuna madudu mengi.
Imesema madai mengine
yameonyesha mashaka, ambapo amewataka wakurugenzi wa halmashauri na wakaguzi wa
ndani, kujiridhisha ukweli wa madai hayo kabla ya kuyafikisha serikalini kwa
ajili ya malipo.
Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa alisema hayo jana, wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Wilaya
ya Ruangwa mkoani Lindi, alipoitembelea wakati akiwa katika ziara ya kikazi,
iliyolenga kukabidhi msaada wa vifaa tiba alivyovitoa kwa ajili ya hospitali
hiyo.
“Madai mengine yanatia
mashaka, sisi hatuhitaji kuletewa madeni ya hovyo hovyo, ni vyema wakurugenzi
wa halmashauri na wakaguzi wa ndani wakajiridhisha kabla ya kuyapeleka
serikalini kwa ajili ya malipo.
“Madeni mengine ya
ajabu, mfano unakuta mtumishi mmoja anaidai serikali sh. milioni 30, jambo
ambalo ni gumu hata kama alihamishwa, haiwezekani kufikia kiwango hicho, pia
kuna baadhi ya majina yamejirudia mara nne,” alisema.
Majaliwa alisema
serikali italipa madeni yote inayodaiwa baada ya kumaliza kuyafanyia uhakiki,
hivyo aliwaomba watumishi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kuyahakiki
ili kuweza kulipa deni sahihi.
Awali, akisoma taarifa
ya idara ya afya kwa Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ruangwa, Dk. Japhet Simeo, alisema idara ya afya inakabiliwa na madeni ya
watumishi, ambayo ni sh. milioni 109.6.
Alisema madeni hayo yalitokana
na likizo, matibabu, uhamisho wa ndani na nje ya wilaya, gharama za mizigo kwa
watumishi waliostaafu, ambapo halmashauri imejipangia utaratibu wa kulipa
madeni hayo pindi inapopokea fedha kutoka serikali kuu.
Hata hivyo, alisema
kasi ya mtiririko wa fedha ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi ya
maslahi ya watumishi, ambapo halmashauri inawapongeza watumishi wa afya kwa
kuendelea kuwa wavumilivu na kuwahudumia wananchi.
Dk. Simeo alisema
halmashauri inawapongeza Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kwa
juhudi wanazozifanya za kuongeza mapato nchini na kuwa wana matumaini watumishi
nao wataboreshewa maslahi na stahiki zao ili kuchochea motisha kiutendaji.
Katika hatua nyingine,
Dk. Simeo alizungumzia upatikanaji wa dawa, ambao alisema umeongezeka kutoka
asilimia 30 mwaka jana, na kufikia asilimia 80 mwaka huu, na dawa muhimu katika
vituo vyote vya kutolea huduma ambavyo viko 32.
Wakati huo huo, serikali
imesema haitalipa
madeni, ambayo halmashauri zinadaiwa kwa kuwa mengi ni hewa.
Aidha, imesema
itazichukulia hatua halmashauri zote zilizoshindwa kujibu hoja, baada ya
kuwasilisha ripoti zao kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC).
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Utumishi na Utawala
Bora, George Simbachawene, alisema hayo jana, jijini Dar es Salaam, baada ya
kupokea ripoti kutoka LAAC.
"Madeni mengi
yanatokana na ukiukwaji wa kanuni na taratibu, hususani za manunuzi, ambapo
watendaji wamekuwa wakiandika idadi kubwa ya fedha tofauti na manunuzi halisi,
huu ni wizi, hatutavumilia," alisema.
Simbachawene alisema
serikali inaonekana inadaiwa fedha nyingi, ili hali ni madeni feki kwa kuwa
baadhi ya watu wamejitengenezea mianya ya kula fedha.
Alisema serikali haipo
tayari kulipa madeni yasiyoeleweka, isipokuwa yale tu yaliyo wazi na kuahidi
kuwachukulia hatua watumishi watakaobainika kufanya michezo hiyo michafu.
"Tutachukua
hatua na kuanzia sasa halmashauri zisizalishe madeni yasiyo ya lazima,
isipokuwa yale tu yanayojibu matatizo ya wananchi," aliagiza.
Hata hivyo, Waziri
Simbachawene alisema watazichukulia hatua halmashauri zilizoshindwa kujibu hoja
mbalimbali walizoulizwa na LAAC baada ya kupeleka ripoti zao.
Alisema kutojibu hoja
ni ukiukwaji mkubwa wa wajibu, ikiwemo kusababisha kupoteza hoja muhimu, ambazo
zingetatua changamoto na kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa.
"Takribani
halmashauri 30 ziliwasilisha ripoti kwa kamati hii na takribani zote
zimeshindwa kujibu hoja huku baadhi zikipuuza mapendekezo waliyopewa," alisema
Simbachawene.
Alizitaja halmashauri
zilizopuuza mapendekezo ya kamati kuwa ni Kigoma Mjini, Kasulu, Mbulu, Kiteto,
Kalambo, Longido na Kwimba.
Waziri Simbachawene alisema
kwa sasa TAMISEMI inasisitiza malipo kufanyika kielektroniki, ikiwemo watendaji
kuacha kuingia mikataba mibovu ya ukusanyaji mapato katika halmashauri zao, jambo linalosababisha upotevu wa fedha.
No comments:
Post a Comment