Thursday, 14 April 2016

OLE SENDEKA: OLE WENU VIONGOZI WAZEMBE CCM, MAGUFULI ANAKUJA


VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi zote, wametakiwa kutanguliza uadilifu na uwajibikaji katika kutimiza majukumu yao.
Wametakiwa kufanya hivyo ili kuwezesha kasi ya utendaji kazi serikalini kuwa mara mbili baada ya Rais Dk. John Magufuli, kukabidhiwa uenyekiti wa CCM, Juni, mwaka huu.
Aidha, viongozi hao wametakiwa kufanyakazi kwa kujituma na kuwatumikia wananchi bila kujali tofauti ya kiitikadi, ili CCM iendelee kupendwa na wananchi kote nchini.
"CCM ni Chama cha ukombozi, ni chama kimbilio la wote, ni chama cha wakulima na wafanyakazi je, viogozi wote tunalifahamu hili? Tujitambue, hali itakuwa tete sana ninawaambia, msijemkashangaa," alisema Christopher Ole Sendeka, Msemaji wa Chama, alipozungumza na viongozi wa CCM wilayani Hanang jana.
Aidha, alisema viongozi hao hawapaswi kufanya kazi kwa woga, bali kwa moyo ili ofisi za CCM ziwe mahali salama wakati wote, na si kama vituo vya polisi au hospitali, ambako watu huenda kwa hofu wakiwa na shida.
Pamoja na hayo, Ole Sendeka aliwapongeza viongozi hao kwa juhudi kubwa walizozionyesha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kufanikiwa kuwa wilaya ya kwanza kutoa kura nyingi za urais ndani ya mkoa wa Manyara.
Alisema anaamini haikuwa kazi rahisi, ikizingatiwa eneo hilo liliwahi kuongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye pia alikuwa Kamanda wa Vijana wa CCM, lakini akahamia upinzani.
Awali, katika hotuba ya makaribisho, Katibu wa CCM wilaya hiyo, Kajoro Vyohoroka, alisema licha ya changamoto kadhaa, hali ya kisiasa ni nzuri na kwamba wanaendelea kuchapa kazi wakati wote.
Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita, walifanikiwa kupata madiwani 21 wa kuchaguliwa, kati ya 33 hivyo kuunda halmashauri.


No comments:

Post a Comment