Tuesday 11 October 2016

MALI ZA WAHALIFU LAZIMA ZITAIFISHWE- PROFESA MCHOME



NA FURAHA OMARY

KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome amesema serikali inataka kuhakikisha mali iliyopatikana kwa njia ya uhalifu, haibaki kwa mhalifu kwa sababu uhalifu haulipi.

Kutokana na hilo, wizara hiyo imewataka wadau wa sheria wanaokutana kwa siku tatu, kuangalia sheria zinazohusiana na urejeshaji wa mali zinazotokana na uhalifu, kuhakikisha mwisho wa mkutano huo wanatoka na majibu ya changamoto zote zinazowakabili.

Profesa Mchome aliyasema hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipokuwa akifungua warsha hiyo, ambayo imewakutanisha maofisa kutoka ofisi mbalimbali, ikiwemo ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), ambapo mkurugenzi wake, Biswalo Mganga na Msaidizi wake, Oswald Tibabyekomya walihudhuria.

Wadau wengine ni Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wizara ya Fedha, Polisi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

“Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo yenye dhamana ya kusimania sheria, ikiwemo kama mtu unapatikana na makosa yanayohusisha mali, basi zikamatwe, zinaweza kutaifishwa au kuwekwa chini ya ulinzi fulani.

“Wadau wanaohusika na eneo hilo wapo wengi, hivyo kazi ya wizara ni kuhakikisha wanakaa na kuangalia namna gani wanatupeleka mbele,” alisisitiza.

Profesa Mchome alisema mali inayopatikana kwa njia ya uhalifu inatakiwa isibaki kwa mhalifu kwa sababu uhalifu haulipi.

Alisema  katika kukabiliana na uhalifu, serikali iliandaa sheria mbalimbali, zikiwemo za utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambazo ni sheria mama.

Profesa Mchome alisema sheria hizo siyo kwamba hazina changamoto, hivyo wadau hao waliokutana wanatakiwa kuzijadili na kuja na majibu ya changamoto zilizoko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Mganga alisema lengo la kukutana ni kuhakikisha wanaweka sheria vizuri kwa kuwa kuna watu wanakamatwa wakiwa na mali zilizopatikana kwa njia za uhalifu na nyingine zinatokana na uhalifu.

“Tunataka kuhakikisha uhalifu haulipi, kama unapata mali kutokana na uhalifu, basi tunataka irudi na ubaki sifuri. Tunakuja katika kauli ya Rais Dk. John Magufuli kwamba, kila mtu lazima afanye kazi na mtu ale kwa ajili ya jasho lake, umepata kwa njia zisizo halali basi zirudi ili isije familia  zikajitapa kwa kupitia mali hizo,”  alisema.

Aidha, Biswalo alisema lazima kuwe na utaratibu mzuri wa jinsi ya kutunza mali hizo, hivyo watahakikisha wanaweka utaratibu ambao utaiweka serikali wakati wote kuwa salama.

“Kwa mfano, gari la mtu liko polisi, tutaamua kuliuza na baadaye fedha kuwekwa katika akaunti na siku ya mwisho kwa aliyeshinda kesi anapatiwa fedha zake,” alisema Biswalo na kuongeza kuwa, lengo la kufanya hivyo ni serikali isipate malalamiko na hasara.

Biswalo alisema wanataka kuhakikisha uhalifu haulipi na nchi inakuwa sehemu salama ya binadamu na viumbe hai kuishi.

Alisema kwa kufanya hivyo, kutawezesha Tanzania isiwe sehemu ya wahalifu kukimbilia na kujificha.

No comments:

Post a Comment