Na Chibura Makorongo, Shinyanga
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, vifaa
vinavyotumika kuhakiki vyeti kwa watumishi wa umma na kuandikisha vitambulisho
vya taifa (NIDA), vinadaiwa kuibwa na
watu wasiojulikana kwenye jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu,
mkoani Shinyanga.
Vifaa hivyo, zikiwemo kamera mbili na viegesho
vyake, vimebainika kupotea jana, asubuhi
wakati wa kujiandaa kuendelea na uhakiki wa vyeti na kuandikisha vitambulisho
vya taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani, Nyabaganga Talaba, alithibitisha upotevu
wa kamera mbili za NIDA.
“Leo asubuhi (jana), ofisa wa NIDA alibaini
kamera mbili na viegesha vyake
havionekani. Tunaendelea kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili
kuwabaini wahusika na kupata vifaa hivyo,” alisema.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga, alikiri
kupotea kwa kamera mbili na viegesha vyake vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye
ofisi ya halmashauri yake kwa ajili ya kupigia picha za NIDA.
Hata hivyo, alisema bado hajawapata taarifa zaidi
kuhusu upotevu wa vifaa hivyo na kuahidi kutoa taarifa zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Muliro
Muliro, alithibitisha kutokea kwa tukio la upotevu wa vifaa hivyo na kusema
kuwa uchunguzi unaendelea.
“Vifaa hivyo vilikuwa vimehifadhiwa katika jengo la
halmashauri, ambalo lina ulinzi, lakini vimekutwa havipo.
Nilichoagiza uchunguzi ufanyike ili tujue kamera
mbili na viegesha vyake viko wapi,” alisema.
Alisema vifaa hivyo vinatumika kwa kuandikisha
vitambulisho vya taifa, sambamba na uhakiki wa yeti kwa watumishi wa umma.
Alisema wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo
ili kujua kama kuna wizi au la na kwamba, mpaka sasa kuna baadhi ya watu
wanahojiwa.
No comments:
Post a Comment