Tuesday 11 October 2016

WATANZANIA 450,000 WANA MATATIZO YA AKILI




Na Happiness Mtweve, Dodoma
ZAIDI ya Watanzania 450,000 wana tatizo la akili kwa kujitambua ama kutojitambua.
Aidha, katika mkoa wa Dodoma, kila siku watu 12, wanapokelewa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Wagonjwa wa Akili ya Mirembe, kutokana na tatizo hilo.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Christina Mndeme, wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani, yaliyofanyika kitaifa mkoani humo.
Alisema tatizo la akili huathiri kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda na kwamba, limekuwa linaongezeka kwa kasi.
"Kutokana na takwimu hizi, ifikapo mwaka 2050, idadi ya wagonjwa wa akili duniani itaongezeka kufikia watu milioni 60," alisema.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya akili na dawa za kulevya ya mwaka 2013/2014, mkoa unaoongoza kuwa na wagonjwa wengi wa akili ni Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkoa huo una asilimia mbili ya wagonjwa wa akili, ukifuatiwa na Mwanza wenye asilimia 1.2 huku Rukwa ukiwa wa mwisho ukiwa na asilimia 0.2.
Christina alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, alisema kwa Dodoma, wagonjwa 1,256, walipatikana katika kipindi cha mwaka 2015.
Alisema kila siku wanapokea wagonjwa 12, ambao wana ugonjwa wa akili, wanaotoka katika maeneo mbalimbali.
Dk. Kiologwe alisema idadi hiyo ya wagonjwa kwa mkoa wa Dodoma ni kutoka katika vituo 132, vilivyopo mkoani humo.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani ya Wagonjwa wa Akili Mirembe, Erasmus Mganga, alieleza sababu kuu mbili zinazosababisha ugonjwa wa akili, kuwa ni ile ya mtu kuzaliwa na vinasaba vya ugonjwa huo, ambapo vinakuwa ni vya kurithi.
Nyingine inatokana na magonjwa ambayo yanashambulia ubongo, ikiwemo mtu kuugua ugonjwa wa malaria, uti wa mgongo na mapafu, hivyo huathiri ubongo.
Alisema mgonjwa huyo akishatibiwa na kupona, anabaki na tatizo kwenye ubongo, hivyo kupatwa na ugonjwa wa kichaa.
Kupitia wizara, alisema serikali ina mpango wa kuanzisha kamati ya dawa za kulevya kila mtaa, ili zisaidie kuwatambua watumiaji wa dawa hizo.
Pia, alisema katika hopitali hiyo, wanapokea wagonjwa wa akili walioathirika kutokana na uvutaji bangi.
 Aliitaja sababu nyingine inayochangia hali hiyo kuwa ni  umasikini, unyanyapaa na unyanyasaji, ambapo mtu mwenye vinasaba vya ugonjwa huo, akikutana na mambo hayo hujikuta ugonjwa ukifumuka.
Alisema serikali imeingiza kwenye mitaala ya mafunzo elimu ya kuhusiana na dawa za kulevya.
Kutoka Zanzibar, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Juma Ali Khatib, amewataka madaktari wanaoshughulikia wagonjwa wa akili katika hospitali za Zanzibar, kujenga uzalendo wakati wakitoa huduma zao.
Alisema kwa kufanya hivyo, kutawezesha wagonjwa wa matatizo hayo kuwa na imani na tiba wanazozitoa.
Waziri Khatib, aliyasema hayo jana, wakati akitoa salamu zake katika maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa wa Akili Duniani, zilizofanyika katika Hospitali Kuu ya Kidongo Chekundu mjini Unguja, ambapo aliwafariji kwa kuwapatia matunda na vinywaji.
Waziri huyo alisema kazi ya kuwahudumia wagonjwa wa akili inahitaji kujitolea zaidi kwa vile wagonjwa wanaowahudumia tayari huwa ni wenye matatizo.
“Ni vyema kwa madaktari ambao wamechagua fani ya kutoa huduma katika eneo hilo, kuona wanakuwa wazalendo zaidi,” alisema.
Alisema tatizo la wagonjwa wa akili hapa nchini bado lipo na limekuwa likiongezeka siku hadi siku, hivyo serikali imeamua kuimarisha utoaji wa huduma katika sekta ya afya kwa kusomesha watoa huduma zaidi, ikiwa ni hatua itakayosaidia kupatikana wataalamu wenye uwezo mzuri wa fani ya tiba kwa visiwa vya Unguja na Pemba.
Akitoa mfano wa hilo, alisema mpango wa serikali ya Zanzibar kusomesha madaktari wa fani mbalimbali hapa nchini na kuja kwa ujenzi wa Hospitali Kuu ya Abdalla Mzee, Kisiwani Pemba na Hospitali ya Mnazi Mmoja na kuongeza vitengo vyake, ni ushahidi tosha wa dhamira ya serikali kukuza ustawi wa sekta hiyo ya afya.
Kutokana na hatua hizo za serikali, Waziri Khatib, aliwataka wanafunzi wanaochukua fani mbalimbali katika sekta ya afya, kuzingatia miiko ya utumishi wao watapomaliza masomo yao kwa kuacha kuwa na tabia ya kuwatolea matusi wagonjwa.
Aidha, aliwataka wanafunzi hao, kuwaona wagonjwa wa akili ni sawa na wagonjwa wengine wanaohitaji kupatiwa matibabu yaliyo sahihi.
Alisema serikali itajitahidi kuhakikisha inawaangalia katika maslahi yao kwa kuwapatia vifaa vya kufanyia kazi.
Waziri Khatib aliwaonya wafanyakazi hao kujiandaa kuvitunza vifaa na majengo mapya ya Hospitali ya Kwa Abdalla Mzee  na Mnazi Mmoja.
Awali, akitoa salamu zake kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Abdumalik Akili, Mkurugenzi wa Huduma za Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, Mohammed Dahoma, alisema serikali imeshajipanga kuona inashughulikia tatizo la wagonjwa wa akili.
Alisema hatua hiyo inatokana na idadi inayowapa huduma imeongezeka kutoka mwaka 2006, kwa kufikia zaidi ya wagonjwa 100,000.
Alitaja miongoni mwa changamoto zinazoikabili  hospitali hiyo kuwa ni uwepo wa dawa zisizotosheleza kwa mahitaji halisi ya wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo.
Alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano, ili kusaidia tiba za wagonjwa hao kwa kuwa ni sehemu ya matibabu yao.
Dk. Akili aliwataka wahudumu wa sekta hiyo, kukaa pamoja kuziangalia changamoto zilizomo katika matibabu ya afya ya akili, hususan sera na sheria zinazosimamia taasisi hiyo.
Mshauri wa Rais Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Abdalla Mwinyi Khamis, aliwataka wanafunzi wanaojifunza fani ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa akili, kuifahamu vyema historia ya kazi hiyo, ikiwa ni hatua itayowasaidia kutoa tiba bora kwa wanaougua maradhi hayo.

No comments:

Post a Comment