Tuesday 11 October 2016

CCM Z'BAR YAJIBU MAPIGO YA CUF




Na Is-haka Omar, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimesema hakina mpango wa kufanya mazungumzo au makubaliano na Chama Cha Wananchi (CUF), kuhusiana na suala la uchaguzi uliopita.
Msimamo huo ulitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alipokuwa akijibu hoja zilizotolewa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, juzi.
“Uchaguzi umekwisha na kazi iliyopo mbele ya CCM ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama ya mwaka 2015/2020, ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi mkuu na viongozi wa CCM zinatekelezwa kwa vitendo,” alisema.
Vuai alieleza kupitia gazeti moja kuwa, Jussa alinukuliwa akisema  CUF inaangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo na CCM, kuhusiana na suala la uchaguzi.
Hata hivyo, alisema  CCM haipo tayari kukaa meza moja na chama hicho kujadili jambo, ambalo lilishafanyiwa uamuzi halali kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za nchi.
Alisema CCM inaweza kukikaribisha chama chochote cha upinzani kufanya mazungumzo juu ya namna gani ya kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM,
siyo suala la uchaguzi mkuu kwa kuwa  umeshapita kisheria na serikali zinaendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Vuai alisema kitendo cha kujadili  serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa ni kwenda kinyume na sheria za nchi kwa kuwa  serikali hizo zimetokana na uamuzi halali wa wananchi kupitia mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia.
Aliwataka wafuasi wa CUF na wananchi kwa ujumla, kupuuza  madai yaliyotolewa na kiongozi huyo, hususan kuhusu mantiki ya kuundwa kwa serikali ya mpito Zanzibar, hatua ambayo haiwezekani na inaashiria kuvunja Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.
“CCM hatuna mpango wa kukaa meza moja na chama chochote cha upinzani, siyo CUF tu, kujadili uchaguzi kwa kuwa tayari umeshapita kwa vigezo vyote vya uhalali wa kisheria.
“Hoja na ajenda  ya kufanyika kwa uchaguzi wa mpito Zanzibar, kwa sasa ni ndoto za mchana ama kujifurahisha kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa usiokuwa na uzani wala  mafanikio kwa wafuasi wa chama kinachojenga hoja hizo hapa nchini,” alisema.
Vuai alisema CCM inaamini uchaguzi umekwisha na sasa inajipanga na maandalizi ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Alisema CUF kwa sasa imekosa mwelekeo ndiyo maana viongozi wake wanafikia hatua ya kuwadanganya wafuasi wao kwa mambo, ambayo kiuhalisia wanajua hayawezi kufanyika katika historia ya uwanja wa kisiasa Zanzibar.
Vuai alisema chama chochote cha siasa pamoja  na kuwa na jukumu la kushinda na kusimamisha dola katika uchaguzi mkuu, bado kinatakiwa kuwa na miongozo imara ya kusimamia ukweli, haki na uwazi kwa wafuasi na wananchi, vigezo ambavyo vimekosekana ndani ya CUF tangua kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2015.
Alisisitiza kuwa kazi iliyopo mbele ya CCM ni kujiandaa kwa mambo mbalimbali, yakiwemo uchaguzi wa ndani wa Chama wa mwaka 2017, kwa ajili ya kupata viongozi makini na hodari, ambao watakuwa na jukumu la kusimamia maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Naibu Katibu Mkuu alitaja jukumu la msingi linalotekelezwa na CCM  kuwa ni uhakiki wa mali za Chama, ili kujiridhisha zaidi ikiwa ni mkakati wa uimarishaji wa hali ya siasa na uchumi ndani ya CCM.
Aliwasihi wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla, kuendelea kuwa watulivu na kushirikiana kikamilifu na serikali zote mbili.
Aidha, aliwataka wananchi kuwafichua baadhi ya wanasiasa wanaojihusisha na vitendo vya kuharibu amani na utulivu wa nchi.                                           

No comments:

Post a Comment