Thursday 24 March 2016

TAKUKURU YATINGA SAKATA LA RUSHWA KWA WABUNGE

SAKATA la baadhi ya wenyeviti wa kamati za kudumu za bunge na makamu wenyeviti  kudaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, linazidi kuchukua sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuanza rasmi kuwachunguza.

Taarifa  iliyotolewa na TAKUKURU, jijini Dar es Salaam jana,
ilisema  taasisi hiyo  ndiyo yenye dhamana  ya kuchunguza  tuhuma zote zinazohusu rushwa  kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa  Namba 11 ya mwaka 2007.

“Suala la Kamati za Bunge kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, tayari TAKUKURU imeanza kulishughulikia na uchunguzi unaendelea,” ilisema taarifa hiyo, iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano ya TAKUKURU Makao Makuu.

TAKUKURU ilitoa maelezo hayo baada ya Uhuru kutaka kujiridhisha juu ya hatua, ambazo taasisi hiyo imechukua baada ya  baadhi ya wabunge kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kutokana na tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma, Maendeleo ya Jamii, Zitto Kabwe, aliamua kuachia ngazi.

Sambamba na Zitto, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, naye alitangaza kuandika barua kwa Spika ili kujivua ujumbe wa kamati hiyo kwa sababu kama aliyoitoa Zitto.

Wakati TAKUKURU ikithibitisha kuanza kufanya uchunguzi huo, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, Dar es Salaam, kilitoa ufafanuzi juu ya hatua ya Spika Ndugai  kufanya  mabadiliko katika Kamati za Bunge, Machi 22, mwaka huu.

Taarifa hiyo imekanusha kwamba, mabadiliko hayo yaliyofanywa na Spika Ndugai, hayatokani na kashfa ya rushwa kwa wabunge.

“Mabadiliko yaliyofanywa na Spika ni ya kawaida na wala hayakuanisha dosari zozote katika utendaji wa Kamati za Kudumu za Bunge.

“Msingi wa mabadiliko ya wajumbe kwenye kamati, umelenga kuzingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda kamati hizo, Januari 2016, ambapo alikuwa ameanza kufanyiakazi mabadiliko hayo tangu mapema mwezi huu,”ilisema taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa wabunge wanaosakamwa kwa uvunjifu wa maadili kupitia mitandao ya kijamii na magazeti, watendewe haki kwa sababu Spika anazingatia utawala wa sheria.

“Na kama kuna mbunge yeyote anayetuhumiwa kwa makosa ya jinai, mamlaka za kiuchunguzi zina wajibu wa kutekeleza majukumu yao na pale inapobidi, Bunge lenyewe kupitia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, inaweza kufanya uchunguzi kwa Mamlaka ya Spika,”ilibainisha taarifa hiyo.

"Ifahamike vema kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 116 (3), mamlaka ya kufanya mabadiliko kwenye Kamati za Kudumu za Bunge ni ya Spika na anaweza kufanya hivyo wakati wowote kama alivyofanya mapema mwezi huu, ambapo alizingatia maombi ya baadhi ya wajumbe 15 kuhamia kamati nyingine kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kiafya na kuboresha utendaji wa kamati hizo kama ilivyojitokeza juzi kwa wajumbe 27 kuhamishiwa kamati zingine,”ilieleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment