Thursday 24 March 2016

POLISI WATATU WASIMAMISHWA KAZI KWA WIZI WA MAFUTA


SERIKALI imewasimamisha kazi askari watatu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa tuhuma za wizi wa mafuta ya ndege aina ya jet-A1, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Saalam.

Pia, imetoa siku 14 kwa uongozi wa kikosi hicho kuhakikisha tuhuma dhidi yao zinachunguzwa na iwapo itabainika ni kweli, wafikishwe mahakamani.

Aidha, imeonya kwamba serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya askari wanaofanya makosa kulindwa kwa kuhamishwa vituo vya kazi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alitangaza uamuzi huo jana, baada ya kufanya ziara katika uwanja huo wa ndege ulioko Dar es Salaam, kwa lengo la kubaini ukweli wa kushamiri vitendo vya wizi wa mafuta ya ndege, ambavyo vinafanywa na askari.

Masauni aliwataja askari aliowasimamisha kazi kuwa ni Musa Mandauli mwenye namba TAA 01066, Khalfani Kisana mwenye namba TAA 01117 na Abias Mwanza.

“Kuna baadhi ya askari ambao si waaminifu, wanalichafua Jeshi la Polisi kwa vitendo vya wizi wa mafuta ya ndege, kwa hiyo wanahatarisha maisha ya abiria kwani rubani anaweza kuingia ndani ya ndege akijua mafuta yapo, kumbe hayapo, hivyo ndege inaweza kwenda juu na kulipuka,” alisema.

Aliongeza: “Watu kama hao serikali haiwezi kuwavumilia, badala yake inachukua uamuzi wa kuwasimamisha askari watatu kutokana na matukio ya hivi karibuni yaliyotokea ya wizi wa mafuta.”

Masauni alionyesha kushangazwa na kitendo cha kuwalinda askari hao, ambao baada ya kubainika kuhusika na vitendo hivyo, waliachwa na kuhamishiwa makao makuu bila ya kuchukuliwa hatua.

Naibu waziri huyo alisema askari hao wanakataa kukaguliwa katika uwanja wa ndege, wakidai wao ni askari, kumbe wanatumika kusafirisha magendo.

Akielezea matukio wanayotuhumiwa kuyatenda askari hao, Masauni alisema Oktoba 7, mwaka jana, saa mbili asubuhi, Mandauli na Kisana, walitumia gari la mkuu wa kikosi hicho katika uwanja huo, lenye namba STJ 2948, ambapo walikutwa wakiwa wamebeba madumu 10 yenye mafuta ya ndege yenye ujazo wa lita 20.  

“Askari hao walipitia geti la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) 603 KJ na walipokaguliwa, walikutwa na madumu hayo,”alisema.

Masauni alisema tukio lingine lilitokea Agosti 26, 2014, saa nane usiku, ambapo askari Mwanza alinaswa na kamera za usalama katika uwanja huo, akishirikiana na mfanyakazi wa kampuni ya usafirishaji mizigo ya SWISSPORT, Lucas Meganda akiiba mizigo ya abiria.

“Hata hivyo, askari hao baada ya kubainika na kukamatwa kwa kosa hilo, bado waliendelea kulindwa kwa kuhamishwa kwenda makao makuu na kupandishwa cheo na kuwa inspekta badala ya kuchukuliwa hatua,” alisema.

Mbali na matukio hayo yaliyofanywa na askari, Masauni aliagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kuwatafuta wamiliki wa magari mawili kwa kosa la kutaka kuiba mafuta ya ndege kwenye uwanja huo.

Alisema Januari 13, mwaka huu, gari lenye namba T 225 AWN, aina ya Saloon GX, lilikutwa na madumu 10 yakiwa tupu, ambapo walipitia katika geti namba sita na lilipokaguliwa, yalikutwa madumu hayo ambapo dereva alitoroka na gari hilo.

Masauni alisema tukio lingine lilitokea Januari 8,mwaka huu, saa nane usiku, ambapo  gari lenye namba T 786 AWZ, lilibeba madumu 30, ambayo yalikuwa tupu na lilipita geti namba nane.

Alisema gari hilo lilipokaguliwa, yalikutwa madumu hayo, lakini dereva wa gari hilo alitoroka na chombo chake, baada ya kubainika lilikuwa na lengo la kutaka kuiba mafuta hayo.

Masauni alisema kilichobainika ni kwamba askari hao huwa na tabia ya kukataa kukaguliwa kwenye kizuizi cha kuingia uwanjani na wanatumika kupitishia magendo.

No comments:

Post a Comment