Thursday 24 March 2016

SERA YA WAZEE KUWA SHERIA-UMMY

SERIKALI imesema imejipanga kuipa nguvu sera ya wazee nchini, kuwa sheria itakayowasaidia kujikwamua katika changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa sasa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema wazee wanakumbwa na changamoto nyingi katika maisha yao ya kila siku, hivyo azma ya serikali
ya awamu ya tano ni kuhakikisha wanapata mahitaji yao muhimu.

Aliyataja mahitaji hayo kuwa ni huduma ya afya, haki ya kuwezeshwa kiuchumi na uwakilishi katika vyombo vya maamuzi.

Ummy alikuwa akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, walipomtembelea ofisi kwake.

“Mimi mwenyewe nalichukua jukumu hili la kufanikisha kuandikwa kwa muswada wa sheria ya wazee nchini na kuupeleka Bungeni,
Septemba, mwaka huu, ili tuwe na sheria itakayowezesha kuwabana watu ambao watakaidi kutekeleza masuala yanayowahusu wazee,” alisema Ummy.

Aidha,Waziri Ummy ameziagiza halmashauri zote nchini, kuanzisha na kuboresha madirisha kwa ajili ya wazee kwenye hospitali zao.

Alisema huduma kwa wazee ni bure kuanzia kumwona daktari, vipimo na dawa, hivyo alihamasisha wazee kuungwa mkono kwenye Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF), ambao unatoa huduma za afya katika maeneo mengi zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, Hemed Mkali, akiwasilisha mada katika kikao hicho, alimpongeza Rais Dk. John Magufuli, kwa kuwajali na kuwapa kipaumbele wazee, kwa kuwapatia wizara, ambayo itawasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.

Alisema wana imani na Waziri Ummy kwamba watashirikiana naye ili kuwafanya wazee wa Tanzania waishi katika maisha mazuri.

No comments:

Post a Comment