Thursday 24 March 2016

SADIKI AMTAKA MAKONDA AWE KARIBU NA VIONGOZI WA DINI




MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Sadiki amemtaka  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa karibu na kamati ya amani ya mkoa huo, ili kupata  ufumbuzi wa  changamoto mbalimbali.
Amemhakikishia kwamba kwa kufanya hivyo,  itamsaidia kufanyakazi zake kwa ufanisi na uhakika zaidi.
Akizungumza wakati  wa hafla  ya makabidhiano ya ofisi jana, Sadiki aliishukuru kamati hiyo kwa msaada mkubwa iliyompatia wakati wote wa uongozi wake.
Sadiki amehamishiwa mkoa wa Kilimanjaro, ambako amekwenda kuchukua nafasi ya mkuu wa zamani wa mkoa huo, Amos Makalla. Kabla ya uteuzi huo, Makonda alikuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni.
Sadiki alisema kamati hiyo  si ya kisiasa na kwamba, ipo kwa  lengo la kuleta amani Dar es Salaam na kuhahikisha  maendeleo yanapatikana.
“Chombo  hicho ni cha kuleta amani bila kujali itikadi za kidini  wala kisiasa. Pasipo kuitumia kamati hii kwa ushauri wa kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dar es Salaam, unaweza kupata wakati mgumu,”alisema.
Alisema  anatambua umuhimu wa kamati hiyo na kwamba ilikuwa mwongozo katika  kazi zake, hasa alipokutana na changamoto za mifarakano ya kidini.
Kwa mujibu wa Sadiki, kamati  hiyo  ina nia  njema  na serikali katika kuhakikisha mkazi wa Dar es Salaam, anapata mahitaji yake.
Kwa upande wake, Makonda  aliitaka kamati hiyo kumsaidia   katika kampeni ya usafi kwa kuwahamasisha waumini kufanya usafi.
“Ninawataka mawaziri  kupaka  rangi nyumba zao ili nami nipate nguvu ya kuwahamasisha wananchi  kwa lengo la kuliweka jiji la Dar es Salaam kuwa safi,”alisema.
Aliwahimiza viongozi hao wa dini  kuhakikisha  wanawahimiza waumini wao kwenye ibada, kupeleka silaha zao zikahahikikiwe ndani ya siku 90 ili kufuata  utaratibu  sahihi.
Akizungumzia mipango yake  katika  uongozi, Makonda alisema ni pamoja na kuhakikisha  Dar es Salaam, inakuwa na  eneo maalamu  la kupaki magari na  gereji  kwa lengo la kuweka jiji katika mpangilio  unaoeleweka.
Pia, aliwataka wenyeviti wa mtaa kuhakikisha wanakuwa na orodha sahihi ya watu wanaowaongoza katika mitaa yao ili  kushiriki kwenye shughuli za maendeleo bila kukosa.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Sheikh  wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Alhad  Mussa Salum, alisema  kamati  yake itahakikisha inafanya kazi kwa karibu na serikali bila kuhusisha masuala ya kisiasa.
Sheikh Alhad alitumia fursa hiyo kuwapa  zawadi wakuu hao wa mikoa  kwa lengo la kuwapongeza na kuahidi kushirikiana nao  vyema katika majukumu ya kujenga taifa.
 Miongoni mwa zawadi alizowazawadia  ni  pamoja na msahafu  wa  digitali na mbuzi wawili, aliopewa  Sadiki  kwa lengo la  kuanzia maisha mapya mkoani Kilimanjaro na  kumkumbuka Mungu katika kila  kazi aifanyayo.
 Makonda alikabidhiwa biblia na fagio kwa lengo la kumtaka  kufagia uchafu wote uliopo Dar es Salaam, ukiwemo ufisadi, uhuni na ubadhilifu ili aende na kasi ya Rais  Dk. John Magufuli.
Mbunge wa  Bunge  la Afrika  Mashariki , Abdula  Mwinyi alisema  mifarakano katika uongozi  hupunguza na kuchelewesha maendeleo nchini.
Aliyataja baadhi ya mambo yanayoleta mifarakano kuwa ni    tofauti za kidini,  kipato duni cha wananchi na  uhaba wa rasilimali.
Alimtaka Makonda kutoangalia umri wake  mdogo, badala yake awashirikishe na  kuwasikiliza  wananchi  juu ya changamoto zao na kuzitatua kwa wakati ili malengo yake yaweze kutimia.
 Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo , Mchungaji  Christopher  Kalata ,  alimuahidi Makonda kuwa pamoja naye  na  kuhakikisha wanakuwa wabunifu kwa lengo la  kuiendeleza jamii.
“Tuna imani na  Makonda na tuko pamoja na serikali  kuhakikisha  jamii inapata mahitaji yanayotakiwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment