Thursday, 24 March 2016

SABABU ZA ONGEZEKO LA JOTO ZATAJWA




ELNINO iliyojitokeza mwaka 2015 na kuendelea hadi mwaka huu,  ndicho chanzo kikuu cha ongezeko kubwa la joto hapa nchini.

Viwango vya joto vilivyorekodiwa hivi karibuni na Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania (TMA), vilifikia hadi nyuzi joto 36, hususan katika maeneo ya Ukanda wa Pwani  na yale ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki,  kiwango ambacho ni cha juu ya wastani kwa takribani nyuzi joto  1.7 hadi  2.0.

Tofauti hiyo ya hali ya joto ni kubwa, ikilinganishwa na viwango
vilivyowahi kupimwa katika miaka mingi iliyopita katika kipindi
hicho, ambapo kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO), ongezeko la joto limejitokeza katika maeneo
mengine duniani.

Dk. Agnes Kijazi, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA, aliyasema hayo jana, jijini Dar es Salaam, wakati wa upandaji miti kwenye eneo linalotarajiwa kujengwa makao makuu ya mamlaka hiyo, Sinza, kama moja ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hali ya Hewa.

Alisema katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa
mwaka huu, TMA ilitumia fursa hiyo kuuhamasisha umma
kutembelea vituo vya hali ya hewa vilivyogawanywa kwa kanda
nane nchi nzima, ili kufahamu huduma zitolewazo na mamlaka
hiyo.

Aidha, alisema kwa kutembelea vituo hivyo, wananchi watajifunza na kuona namna watakavyoweza kufaidika na huduma za hali ya hewa katika maisha yao na shughuli za kila siku kwa maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania.

Mkurugenzi huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwataka watumishi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, kupanda miti katika siku hiyo
maalumu, inayoadhimishwa kukumbuka kuzaliwa kwa Shirika la
Hali ya Hewa Duniani (WMO), miaka 66 iliyopita.

Alisema wamepanda miti hiyo iliyotolewa kwa hisani ya Wakala
wa Misitu Tanzania (TFS), katika maeneo mbalimbali nchini yenye ofisi za TMA, ili kuonyesha umma juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kama njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko yajayo ya hali ya hewa.

“Hali ya hewa itaendelea kubadilika kwa miongo ijayo kwa kadri,
ambavyo shughuli za kibinadamu zitaendelea kufanyika na
kusababisha ongezeko la gesi joto katika anga, hususan kwa
kukata miti,” alisema.

Aidha, alisema kwa miongo kadhaa iliyopita, joto la wastani la
kila mwaka, limekuwa likiongezeka zaidi, ikilinganishwa na
mwaka uliotangulia na hiyo ni kutokana na taarifa za nchi
mbalimbali, ikiwemo Tanzania, ambazo zimekuwa zikirekodi
ongezeko la viwango vya juu na vya chini vya joto.

Alisema matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile ukame na
mafuriko, yamekuwa yakitokea katika sehemu mbalimbali duniani na kwamba, mabadiliko haya ya hali ya hewa yamekuwa yakibadilisha mifumo ya asili ya misimu na ongezeko la ukubwa  wa matukio ya hali mbaya ya hewa. 

“Joto kali, ukame na mvua nyingi ni mabadiliko ya hali ya hewa,
ambayo yanatarajiwa kuendelea kuchangia kuwepo kwa joto kali, ukame, mafuriko katika nyakati zijazo, hivyo kupanda miti ni
suluhusho zuri,” alisema.

No comments:

Post a Comment