Thursday, 24 March 2016

MHASIBU WA WAFUGAJI ATUPWA JELA MIAKA 23




MHASIBU Mkuu  wa Baraza la Wafugaji Wilaya ya Ngorongoro, Loserian  Laizer, amehukumiwa kwenda jela miaka 23, baada ya kupatikana na hatia ya kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya sh.milioni 4.3.

Hasara hiyo ilitokana na kuandaa orodha hewa  za majina ya wanafunzi wanaoidhinishwa na baraza hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha,  Juventus Baitu, alisema  mhasibu huyo alihukumiwa Machi 18, mwaka huu, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Ngorongoro, Dimitrio Nyakunga.

Kwa mujibu wa Baitu, mtuhumiwa huyo alitiwa hatiani kwa makosa manne ya matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, ambapo kila kosa alihukumiwa kifungo cha miaka minne na  kwa kosa la kuisababishia hasara serikali, alihukumiwa  kwenda jela miaka saba.

Baitu alisema mtuhumiwa alikuwa mhasibu wa baraza hilo,  ambalo liko chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na alifikishwa mahakamani  kwa mara ya kwanza na TAKUKURU, mkoa wa Arusha, kupitia wilaya ya Ngorongoro, Juni 6, 2013.

Shauri hilo lilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Ngorongoro na kusajiliwa kwa ECC. Na. 4 ya mwaka 2013, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya, Dimitrio Nyakunga.

Baitu alisema jumla ya makosa aliyoshitakiwa ni matano, ambapo kati ya hayo, manne  yalihusiana na matumizi ya nyaraka zenye maelezo ya uongo, kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007.

Baitu alisema kosa la tano lilihusiana na kuisababishia hasara
serikali kinyume  na aya ya 10 (i) kifungu cha 57 (1) na 62 (2)  cha sheria ya uhujumu uchumi, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Alisema mtuhumiwa akiwa kazini, alitayarisha nyaraka za uongo, akiwa mhasibu wa baraza hilo kwa kuandaa orodha ya majina ya wanafunzi wanaodhaminiwa na Baraza la Wafugaji na kuwalipia  ada na posho za kujikimu, wakati ni hewa.

Baitu amewaasa watumishi wa umma na wananchi kutojihusisha na vitendovya rushwa kwa kukataa kutoa wala kupokea rushwa.

No comments:

Post a Comment