Thursday, 24 March 2016

MAJALIWA KUKABIDHIWA RIPOTI YA VIKUNDI HATARISHI




KAMATI ya Maadili ya Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini Tanzania, inatarajia kumkabidhi Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,  ripoti yenye orodha inayotaja vikundi na maeneo hatarishi kwa taifa vinavyotumia mgongo wa dini.
Wakizungmza Dar es Salaam, jana, viongozi wa kamati hiyo walisema ripoti hiyo inalenga kupiga vita aina yoyote ya uchochezi na vikundi hatarishi, vinavyo jaribu kuingiza chokochoko nchini kwa mgongo wa dini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo,  Askofu  William  Mwamalanga, alisema ripoti hiyo imeainisha mikoa  hatari zaidi ya 13, nyumba za ibada na vikundi vya uchochezi.
Alisema wamefikia uamuzi wa kuikabidhi ripoti hiyo kwa Waziri Mkuu, baada ya kukusanya ushahidi  mzito,  ambao  hawana shaka nao  juu ya vitendo hivyo.
 “Kuna  baadhi ya waumini, viongozi wa dini na vikundi, vinatumia mgongo wa dini kufanya mambo, ambayo  hayafai. Na kuna mikoa, ambayo kiukweli uchunguzi wetu umebaini kuwepo kwa mazingira hatari zaidi. Kama kamati ya maadili, hili halivumiliki kwa sababu linaweza kuwa hatari kwa ustawi wa taifa,”alisema askofu huyo.
Aidha, alisema orodha hiyo itahusisha nyumba za ibada zinazoongoza kwa uchochezi,  taasisi, mashirika, vikundi na viongozi wa dini ili  washughulikiwe kikamilifu.
Alisema  kamati hiyo imebaini  bila shaka yoyote,  kuwepo kwa viongozi na vikundi hatari, ambavyo vinajaribu kuchimba amani iliyopo kwa kutaka kufanya uchochezi na kuibua mifarakano.
“Vikundi hivi vimeanza pia kueneza uchochezi huo kwa njia ya mitandao na  tunaiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuchukua tahadhari juu ya taarifa zozote za kidini kuingizwa mitandaoni, waziondoe haraka,”alionya askofu huyo.
Alisema Tanzania ni nchi isiyofuata tofauti za kidini na misingi  ya serikali yake haifuati tofauti hiyo, bali inaongozwa kwa  kufuata katiba.
“Tunashukuru tumempata Rais Dk. John Magufuli, ambaye uongozi wake haufuati mambo hayo wala  tofauti ya itikadi za kisiasa, hivyo niwaombe Watanzania, hususan vijana, kutokubali kutumika katika njama ovu, hasa kwa njia za kidini.  Tuendelee kulinda amani kwa umoja wetu,”alisema Askofu Mwamalanga.
Alibainisha kwamba ripoti hiyo pia itagusia kwa undani  hali ilivyo katika visiwa vya Zanzibar.
“Kama kamati inayoundwa na madhehebu ya kidini, wajibu wetu si kuhubiri tu, bali kufanyakazi kwa vitendo  kwa maslahi ya jamii nzima,”alieleza.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo imeitaka serikali kuendesha  zoezi la usalimishaji silaha nchi nzima, badala ya Dar es Salaam pekee, huku ikitaka taasisi za kidini zihusishwe kikamilifu katika uchunguzi.
“Tunaamini kuna  mambo yamejificha katika nyumba zetu za ibada, ambayo tunahitaji yawe yanafuatiliwa kwa karibu. Zoezi hili liendane na uchunguzi  huo katika taasisi zetu, ambazo baadhi zimeanza kupoteza mwelekeo wa kutekeleza malengo yake na kujihusisha katika uchochezi na upangaji wa  mambo hatari kwa taifa,”alisisitiza Mwamalanga.

No comments:

Post a Comment