KAMATI ya Bunge ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC) , imesitisha kujadili suala la Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na Kiwanda cha Nyama cha
East Afrika Meat (EAMEATCO), baada ya Makamu Mwenyekiti wa awali, Kangi Lugola kutokuwepo
kwenye kikao.
Lugora ni miongoni mwa wabunge
walioondolewa kwenye kamati hiyo, wakisubiri uchunguzi wa tuhuma za rushwa
zinazozikabili kamati mbalimbali za Bunge .
Pia, hoja hizo zimeshindwa
kujadiliwa kutokana na ugeni wa Meya wa
Jiji, aliyechaguliwa juzi, hivyo hajui chochote kuhusu sakata hilo.
Akizungumza jana, Dar es
Salam, Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Abdallah Chikota, alisema kutokana na
unyeti wa suala hilo, kamati yake haitaweza kuendelea kusikiliza hoja kuhusiana
na miradi hiyo muhimu kwa jamii.
Mbali na kuahirisha kikao hicho,
Chikota, ambaye ni mbunge wa jimbo la Nanyamba, alisema kamati hiyo imeazimia
kutoa maagizo mawili kwa serikali, ikiwemo kurejesha kiwanda cha nyama kwa Halmashauri
ya Jiji la Dar es Salaam, ili iwe mali yake na kuacha kujadili hoja yoyote ili
wajumbe wapate taarifa za kutosha.
“Ni lazima tupange siku maalumu,
hata kama ni Jumamosi ili suala la kiwanda cha nyama na UDA lifike mwisho kwani
limekuwa bughudha katika kamati,”alisema Chikota.
Kwa upande wake, Waziri
wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-
TAMISEMI), George Simbachawene, aliipongeza kamati kwa uamuzi huo kwa kuwa
utaleta maslahi kwa jamii.
Alisema muda walioutoa utasaidia
wajumbe hao kutoa taarifa za kina kutokana na unyeti wa suala hilo, hasa kiwanda
cha nyama.
“Sisi wenyewe tumechoshwa na hizi
hoja, tunahitaji kufahamu kwa kina suala hili kwa sababu lina wadau wengi. Ifike
wakati tuite wadau wote ili kila mmoja aelezee mtazamo wake na athari zake, kwa
kuwa zinagusa maisha ya kila mmoja na hisa za wawekezaji,”alisema
Simbachawene.
Aliongeza kuwa ana imani kwa mfumo
huo, watalitekeleza suala hilo kwa usahihi bila kuleta athari yoyote.
Naye Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
Isaya Mwita, alisema hana chochote anachokifahamu kuhusiana na mjadala uliopo
mbele ya kamati hiyo na kwamba, hatakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
No comments:
Post a Comment