RAIS Dk. John Magufuli
ameandika historia nyingine ya aina yake katika uongozi wake, baada ya
kuamua kula chakula cha mchana katika moja ya migahawa iliyoko pembeni ya
uwanja wa ndege wa Mwanza.
Tukio hilo lilitokea jana mchana, wakati Rais Magufuli
na mkewe, Janet Magufuli, walipotua kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, akiwa njiani
kwenda nyumbani kwake Chato kwa mapumziko.
Rais Magufuli alipokewa na viongozi mbalimbali wa
serikali wa mkoa wa Mwanza, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, Meya
wa Jiji la Mwanza, Mstahiki James Bwire, Meya wa Ilemela, Mstahiki Renatus
Mulunga na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa, Anthony Diallo.
Akizungumza na viongozi hao pamoja
na waandishi wa habari na viongozi wa dini, Rais Magufuli aliagiza kufunguliwa
kwa barabara ya Airpot-Igombe hadi Kayenze, iliyofungwa tangu mwaka 2014,
kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa kisasa wa Mwanza.
Kufungwa kwa barabara hiyo yenye
urefu wa kilomita saba, kumesababisha usumbufu kwa wananchi wa jiji la Mwanza
na vitongoji vyake, vikiwemo vya wilaya ya Ilemela na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakiitumia.
Rais Magufuli alisema kufungwa kwa
barabara hiyo kumeleta adha kubwa kwa wananchi wa jiji hilo la kibiashara.
“Natambua lipo suala linalowaumiza
wananchi la kufungwa kwa barabara hii ya Airpot-Igombe. Sasa naagiza mkuu wa
mkoa kuanzia leo, barabara hii ifunguliwe ili wananchi waitumie ili kuondoa
usumbufu wa kuzunguka kupitia Nyakato hadi maeneo ya TX Kata ya Bugogwa, Igombe
hadi Kayenze katika kata ya Sangabuye,” alisema.
Rais Magufuli alieleza kuwa serikali
itaangalia uwezekano wa kupanua uwanja huo kuelekea mashariki ili barabara hiyo
inayopita pembezoni mwa Ziwa Victoria na uwanja wa ndege, iboreshwe kwa kiwango
cha lami na kuharakisha maendeleo ya wananchi wa maeneo hayo.
“Katika bajeti ya fedha ya mwaka
2016/2017, tumepanga kutoa fedha kwa lengo la kuhakikisha ujenzi wa uwanja huu
unaoboreshwa kuwa wa kisasa na ukamilike ili kuwezesha ndege kubwa kutua kwa
wingi na pia kutumiwa kimataifa na nchi za Maziwa Makuu kama tulivyoahidi
wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015,” alisema.
Alisisitiza kuwa kamwe hataki
kusikia tena uwanja huo umefungwa na kuuagiza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege nchini (TAA), kuupanua zaidi kwenda mashariki, ambapo kuna nafasi ya
kutosha kuliko kulazimisha kufunga barabara muhimu kwa matumizi ya wananchi.
Hii ni mara ya tatu kwa Rais
Magufuli kutoa agizo la kufunguliwa kwa barabara hiyo, ambapo mara ya kwanza ilikuwa
alipokuwa Waziri wa Ujenzi na mara ya pili, alipofika ofisi ya CCM mkoani
Mwanza kusaka wadhamini wakati wa kuwania kuteuliwa kugombea urais ndani ya
CCM.
Wakati wa mchakato wa kuwania urais,
alimueleza Katibu wa CCM mkoani hapa, Miraji Mtaturu kuwa, akichaguliwa kuwa rais,
atahakikisha barabara hiyo inafunguliwa na kuboreshwa kwa kiwango cha lami ili
kuwaondolea adha wananchi wanaoitumia.
Awali, Rais Magufuli aliyetua
uwanjani hapo saa 5:15 asubuhi, alikwenda eneo walipokuwa wamesimama watumishi
wa uwanjani hapo na kuwasalimia kwa kushikana nao mikono.
Wakati akiongozwa na maofisa wa
Idara ya Usalama kwenda chumba cha VIP, alikatiza ghafla na kwenda kwenye
mlango wa chumba cha kupumzikia abiria, ambao ulikuwa umefungwa na kuomba
ufunguliwe, ambapo alipata fursa ya kusalimiana na abiria.
Kabla ya kuanza safari ya kwenda Chato, Rais Magufuli na
mkewe waliamua kupata chakula cha mchana kwenye mgahawa wa Victoria, tukio
lililopokelewa kwa mshangao mkubwa na wananchi waliofika uwanjani hapo kumlaki.
Wakati Rais Magufuli, mkewe na viongozi hao wa serikali
wakiwa wanapata chakula kwenye mgahawa huo, wananchi hao pamoja na baadhi ya
wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, walisimama pembeni ya mgahawa huo
wakimpungia mikono.
Mbali na kupata msosi kwenye mgahawa huo, Rais Magufuli
aliamua kutoa sh. 100,000 na kuwanunulia soda wananchi waliokuwepo kwenye
mgahawa huo pamoja na waandishi wa habari.
Mmoja wa wasimamizi wa mghahawa,
ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alieleza kufurahishwa kwake na
kitendo hicho cha Rais Magufuli, na kuahidi kubadilisha jina la mgahawa wake na
kuuita ‘Dk Magufuli Café’ ili kuenzi kufika kwake na kula chakula hapo,
ikizingatiwa kuwa ni kiongozi mkubwa wa nchi.
Mara baada ya Rais Magufuli kuondoka uwanja wa ndege wa Mwanza kuelekea Chato, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema agizo hilo la Rais litatekelezwa mara moja.
“Mimi na Kamati ya Ulizi na Usalama
ya mkoa, wilaya pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Meneja wa Tanroads mkoa wa Mwanza na viongozi
wa CCM wilaya ya Ilemela, tunaongozana muda huu kwenda TX Kata ya Bugogwa ili kufikisha ujumbe
uliotolewa na Rais Dk Magufuli ili wananchi watumie barabara hii kuanzia sasa,”
alisema.
Rais Magufuli alipita Mwanza, akiwa njiani kwenda
nyumbani kwake Chato, kwa mapumziko ya siku tano. Baada ya mapumziko hayo, Rais
Magufuli anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi Jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment