Monday 9 November 2015

TPF-MASHUJAA CHAPATA USAJILI WA MUDA





Na Mwandishi Wetu
MSAJILI wa Vyama  vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ametoa  cheti cha usajili wa muda kwa Chama cha Tanzania Patriotic Front (TPF Mashujaa).
PTF-Mashujaa ni chama cha 23, katika orodha ya vyama vya siasa vilivyosajiliwa nchini, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana, Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisema cheti hicho kwa mujibu wa sheria ni cha siku 180, ambapo chama hicho kitatakiwa kutafuta wanachama 200, katika mikoa 10 ya Tanzania Bara  na miwili  ya Zanzibar.
Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho,  Deonatus Mutani alisema  lengo lake ni kulinda, kutetea na kudumisha uhuru, haki, amani na ustawi wa nchi na raia wote.
"Malengo mengine ni kupambana kisiasa ili kulinda fedha, rasilimali za nchi na urithi  wa asili wa nchi visiporwe, visidhudumiwe au kitumiwa vibaya na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya kikundi chochote cha watu kitakachopanga kuiba, kuhamisha, kuhujumu, kutumia vibaya fedha na rasilimali za nchi," alisema.
Alisema walifanya utafiti kwa muda mrefu na kuzingatia hali ya kisiasa  na vyama vilivyopo na kubaini kuwa, hakuna mahitaji mengi ya kisiasa yanayohitaji majibu kwa kupitia chama cha siasa kilichojipanga vyema.
"Tunahitaji chama  kinachowatumikia na kumilikiwa na wananchi badala ya wananchi kukitumikia chama na kitakachowakwamua wananchi katika mfumo, ambao siasa inachukuliwa kama jambo la mpito, hasa wakati wa uchaguzi na mijadala bungeni," alisema Mutani.
Aliongeza kuwa wamepitia katiba za vyama mbalimbali na kuona mapungufu ambayo hayawezi kushabiliana na ushujaa wanaotaka kujenga katika vyama vyote, mwanachama anayekosoa sera za chama hadharani na kutofautiana na misimamo ya viongozi wenzake.
Mutani alisema wameheshimu na kuruhusu demokrasia ya kweli ndani ya chama, viongozi wakuu wa chama na wale wanaogombea nafasi za uongozi katika dora watajadiliwa katika matawi na kutoa tamko huru la madai.
"Binadamu wote wanastahili kuheshimiwa, kuthaminiwa, kutendewa haki, kumiliki mali binafsi na kushiriki kataka maendeleo ya nchi bila kijali tofauti zilizopo miongoni mwao, ndio maana tumeamua kuanzisha chama cha kawaida, kwa ajili ya watu wa  kawaida na maisha ya kila siku kwani siasa ni maisha," alisema Mutani.
Alisema chama hicho hakina udini wala ukabila, isipokuwa kazi yake kubwa ni kutangaza sera za chama hicho kwa maendeleo ya jamii.

No comments:

Post a Comment