Wednesday 9 September 2015

JOGOO LA KITAIFA NI MAGUFULI, WENGINE WASINDIKIZAJI-CHENGE




NA PETER KATULANDA, BARIADI

MGOMBEA ubunge wa Bariadi Mashariki, Andrew ChengE, amemponda mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, kuwa si chochote na kuwa jogoo la kitaifa linalowika ni Dk. John Magufuli, wengine wasindikizaji.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa uzinduzi wa kampeni za CCM mkoani Simiyu uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM, juzi, Chenge aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na waziri katika wizara mbalimbali alisema sera za CCM ni za uhakika na zinatekelezeka.
Chenge alisema: "Ndugu zangu mmepata msuluhishi kwa matatizo na mambo yote ambaye ni Dk. Magufuli, fungueni bongo zenu."
“Jogoo  la kitaifa linalowika Tanzania nzima ni Dk. Magufuli, CCM oyeeee, si huyo mwingine……..” alikatishwa na wananchi waliompokea kwa shangwe na kuanza kuselebuka baada ya kibao cha CCM mbele kwa mbele kusherehesha.
Mbunge huyo alisema akichaguliwa tena kushika kiti hicho atapigana kufa na kupona mji wa Bariadi upate maji kutoka Ziwa Vitoria, mpango wa mradi mkubwa wa kufikisha maji Bariadi kutoka Nyashimo wilayani Busega kupitia vijiji vya Lugangabilili, Kisesa na Mwanuzi hadi Mwanuzi Meatu, upo mbioni kukamilika.
Vipaumbele vyake vingine alivitaja kuwa ni kuendelea kuboresha elimu na kuondoa tatizo la madawati, kuboresha na kujenga zahanati, vituo vya afya na barabara za vijijini na kusambaza mbegu za alizeti ili liwe zao mbadala wa pamba ambayo soko lake halina uhakika.
“Pamba ni zao zuri sana tukifuata utaratibu wa kilimo chake na kutumia mbegu bora za kisasa, lakini nataka tuanze kulima zao la ziada ambalo ni alizeti, zao hilo linaiva kwa miezi mitatu tu, litakuwa mkombozi badala ya kutegemea pamba tu,” alieleza Chenge.
Mgombea ubunge wa jimbo la Itilima, Njalu Silanga, alifanikiwa kuteka nyoyo za maelfu ya wananchi na hasa vijana aliposalimia wananchi na kudai yeye ni mbunge wa Simiyu ambaye atakuwa pampu ya kumsukuma Chenge kwa kusaidia maendeleo ya mkoa huo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha vijana iwapo atachaguliwa kuwa mbunge.
Silanga alisema, wana Simiyu wakidanganyika na kumchagua Lowassa aliyewafanya wakose baadhi ya huduma za kijamii kutokana na kutafuna fedha za Richmond, watakuwa wamejiloga wenyewe na wasiisingizie CCM kuwa imesabisha wakose maendeleo, CCM imemtosa fisadi inataka tingatinga (Dk. Magufuli) liwatengenezee maendeleo.

No comments:

Post a Comment