NA MWANDISHI MAALUMU, MOROGORO
SERIKALI imewaasa watumishi wa umma na wa sekta binafsi, kujiepusha
na vitendo vya rushwa na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria,
kanuni, miongozo na taratibu zilizowekwa.
Imeonya kuwa mkono wa serikali hautamwacha mtu
anayejihusisha na vitendo hivyo bila ya kujali hadhi yake.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan,
wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, uliofanyika jana, katika Uwanja
wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Makamu wa Rais alisema mpaka sasa jumla ya kesi 596 za
rushwa zinaendelea mahakamani na jumla ya shilingi bilioni 6.5 tayari
zimeokolewa.
Samia alisema falsafa ya Mwenge wa Uhuru inahitajika zaidi hivi
sasa kuliko wakati wowote ule ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza za
kitaifa na kimataifa.
Alisema tangu kuanzishwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 1964
na kukimbizwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umekuwa kichocheo kikubwa
katika kuhamasisha maendeleo, umoja, mshikamano na kudumisha amani ambayo ni
tunu pekee ndani ya taifa
Makamu wa Rais alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni
kuanza kujengeka hali ya kudharauliana ndani ya jamii, kuchukiana na
kukatishana tamaa.
Samia alisema kuna haja ya kuzikabili changamoto hizo kwa
ujasiri wa hali ya juu, kwa malengo yale yale ya kudumisha amani, upendo, umoja
na mshikamano kupitia mbio za mwenge huo.
"Hilo ndilo tunalolifanya viongozi wenu wa serikali
kitaifa. Hatua zote tunazozichukua za kutumbua majipu ni kurudisha heshima na
kurudisha matumaini kwa wale waliokata tama. Serikali yenu inaendeleza falsafa
hii, naomba nanyi mtuunge mkono," alisema Makamu wa Rais.
Akizungumzia ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu
wa ‘Vijana ni Nguvu Kazi ya Taifa, Washirikishwe na Wawezeshwe,’ Samia alisema
mbali na kuhitaji kupatiwa elimu na ujuzi wa stadi za kazi, wakuu wa mikoa na wilaya nchini wanapaswa kutenga
maeneo rasmi kwa vijana ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Alisema wakati taratibu za kutafuta maeneo rasmi zinafanywa,
viongozi hao watenge maeneo maalumu kwa siku za Jumapili na kuwataka vijana
walipe ushuru, waimarishe usafi na waweke ulinzi wakati wakiendesha shughuli
zao.
Samia pia alitumia fursa hiyo kuelezea azma ya serikali ya
kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi kwa lengo la kudhibiti
mianya ya upotevu wa mapato ya serikali na kuboresha uwajibikaji katika
usimamizi wa rasilimali na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, alisema serikali inaendelea kupambana na malaria, ukimwi
pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, hatua ambayo itawafanya wananchi kuwa
wenye afya bora, nguvu na ari ya kufanya kazi,hivyo kuongeza tija kwa Taifa na
kutokomeza maadui umaskini, ujinga na maradhi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama,
alisema mwenge huo utakimbizwa kwa siku
179, katika mikoa na halmashauri zote nchini.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo
mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya kutoka Tanzania Bara
na Visiwani.
No comments:
Post a Comment