Wednesday 7 October 2015

KINGUNGE KUNA KITU ALICHOKISAHAU CCM?





NICHUKUE fursa hii kumpongeza Mzee Kingunge Ngombale Mwiru   kwa kutekeleza azma yake ya miaka mingi ya kukisaliti chama kilichomlea cha CCM.
Nafurahi kuona kuwa Kingunge ameamua kukubaliana na ukweli kwamba  CCM ya sasa inaendeshwa na  watu makini  tena wenye damu inayochemka. Watu ambao  kasi yao asingeweza  kuimudu hata kidogo kwa sababu umri wake umekwenda.
Wahenga walisema ‘Uzee ni kisima cha busara,’ lakini ninampongeza  Kingunge kwamba baada ya kubaini kisima chake  hicho kimekauka busara zilizomfanya kuheshimika mpaka sasa  katika taifa hili, aliona hana budi kukifukia kabisa.
Ninampongeza kwa kujitathimini  na kujikosoa kwamba hawezi tena kutoa ushauri  kuendana na kasi hiyo  na CCM ya sasa siyo saizi yake hivyo kuamua kujiweka pembeni.
Haya ni maamuzi ya msingi kabisa ambayo kama kuna wengine wako ndani ya CCM wanaamini kuwa hawawezi kuendana na kasi ya mabadiliko yanayoendelea, ni bora wajiondoe mapema.
CCM haiundwi na watu wanaohitaji huruma ya kusikilizwa hata kama wanachoshauri hakifai. CCM ya sasa haiendeshwi kwa kauli ya ‘Zidumu fikra za mwenyekiti’. CCM  ya sasa haiendeshwi kwa  watu wanaotegemea hisani ya  kubebwa na fulani kama kina Kingunge walivyokuwa wakibebwa na Mwalimu Nyerere kwa sababu ya busara zake.
Hii ni  CCM  mpya. CCM makini ya watu makini na  wenye maono  thabiti.  Wengi watashindwa  kasi yake. Watashuka katika gari kubwa na kuwaacha wenye CCM yao waendelee na safari ya mabadiliko ya kweli.
CCM ya sasa inaendeshwa na wenye moyo wa dhati wa kuleta mabadiliko. Kingunge ameshindwa kasi hiyo na ndiyo maana ninampongeza kwa kujipima na  kufanya maamuzi hayo  kisha kubaini kuwa hafai kuendelea na safari ya mabadiliko  ndani ya chama.
Ujana wake wote  amekula ndani ya CCM, eti leo hii uzee wake anaumalizia upinzani. Kuna nini hapo?
Bila shaka ni tama. Kingunge ameingiwa na tamaa kiasi  cha kumsaliti swahiba wake  Hayati Mwalimu Nyerere. Ameingiwa na tamaa mbaya. 
Lakini hii ni tamaa ya nini kwa umri alionao? Tamaa ya uongozi? Tamaa ya umaarufu? Tamaa ya  fedha? Tamaa ya kutafuta sifa ? Anahangaikia nini? Anahitaji nini mzee huyu?
Swali ni kwamba,  kwa uzito wa Kingunge, ni mzee gani anayefanana naye au anayemzidi kwa umri, ambaye alikwenda kumshauri   ili achukue uamuzi huo wa kusaliti Chama? 
Itanishangaza kuona kuwa,  Kingunge alishawishiwa kuchukua uamuzi huo na kama hakushawishiwa, basi inasikitisha  kama utakuwa ni uamuzi  uliotoka ndani ya kichwa chake mwenyewe.
Simfahamu vema Kingunge. Huu ndiyo ukweli. Nakiri hivyo  kwa sababu uwepo wake serikalini nimeanza kuusikia  baada ya kuzaliwa na kupata ufahamu.
Baada ya hapo nilianza kufuatilia sifa zake kwamba alikuwepo hata enzi za babu wa babu wa baba yangu  na alikuwa kiongozi katika taifa hili katika ngazi mbalimbali.
Ameishi maisha marefu ndani ya CCM. Hata nyumba aliyoishi ni ya CCM. Nashangaa eti Kingunge anaihama CCM leo hii mwaka 2015, wakati alikuwepo tokea  hamsini kweusi. Mbona amechelewa sana?
Nasema hivyo kwa sababu ninakumbuka sana kuwa,  katika nyadhifa nyingi alizowahi kupewa na Mwalimu Nyerere, alikuwa akivuliwa baada ya kusaliti. Hata  ukamanda wa vijana wa CCM (UVCCM) alivuliwa na ndiyo wadhifa wa mwisho.
Ndiyo maana nasema amechelewa kwa sababu alikuwa na chembechembe za usaliti tokea enzi za Mwalimu Nyerere.
Mwalimu alikuwa ni mtu mwenye huruma, hivyo alikuwa akimsamehe. Kingunge ameishi hivyo na kukua hivyo kwa kuonewa huruma na kubebwabebwa. Ameishi kwa kutegemea huruma ya Mwalimu. Kama si Mwalimu basi Kingunge huyu angefanya usaliti kama huu uzeeni? Asingeweza.
Hapa ndipo ninapokumbuka nukuu  anayopenda kuitumia Mwenyekiti wa  NCCR –Mageuzi, James Mbatia, mara nyingi. Amekuwa akinukuu kifungu cha Biblia kinachosema, “Heri kijana  masikini, kuliko mfalme mzee mpumbavu, ambaye hasikii tena maonyo.”
Nenda  Kingunge. Kama kuna kitu umesahau ndani ya CCM, tutakuletea.

No comments:

Post a Comment