BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatarajia kuanza kutumia utaratibu mpya kuwasajili wabunge kwa kuwachukua alama za vidole, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi na usalama na pia kuwatambua wabunge watoro.
Utaratibu huo pia utahusisha wafanyakazi wa bunge pamoja na waandishi wa habari wanaofika bungeni kwa ajili ya kuripoti habari za bunge.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Bunge, Didas Wambura, mbele ya Naibu Spika wa Bunge Tulia Akson.
Awali, Naibu Spika alikagua ukumbi wa bunge uliokuwa ukifanyiwa matengenezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubadilisha paa, kufunga viti vipya na kuweka mitambo mbalimbali, ikiwemo ya kuchukua alama za vidole.
Kwa mujibu wa Wambura, wabunge wote watafanya usajili kwa kuchukuliwa alama za vidole na kwamba, kwa siku ya kwanza, zitachukuliwa alama za vidole vyote kumi ili kama itatokea tatizo katika kidole kimoja, vingine viweze kutumika.
"Mchakato huo utaanza kesho (leo) na unatarajiwa kuchukua siku mbili hadi tatu na baadaye wataanza kusajiliwa kwa vidole gumba vya mikono yote miwili,"alisema.
Akifafanua zaidi kuhusu utaratibu huo, Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila, alisema lengo la kutumia mitambo hiyo ya kuchukua alama za vidole ni kuweka vizuri mahudhurio ya wabunge.
Aidha, alisema waandishi wa habari, wafanyakazi na wageni wote wanaoingia bungeni, nao watalazimika kusajiliwa kwa kutumia utaratibu huo kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama.
"Katika utaratibu huu, si wabunge peke yao watakaochukuliwa alama hizo, bali ni kwa watu wote ili iwe rahisi kuwatambua wanaiongia na kutoka,"alisema.
Alisema mchakato wa kuchukua alama za vidole una faida nyingi kutokana na ukweli kwamba, watu wanaoingia bungeni kwa siku wanafika 1,000 hadi 2,000, idadi ambayo alidai ni kubwa sana.
"Nanyi waandishi pia mtachukuliwa alama za vidole pamoja na wafanyakazi wote, lengo ni kutambua muda wanaoingia na kutoka wafanyakazi," alisema Dk. Kashilila.
Pia, alisema ofisi ya bunge ipo kwenye mchakato wa kufunga 'tablet' kwenye ukumbi wa bunge ili kuwarahisishia wabunge kupata taarifa mbalimbali, zikiwemo matangazo ya shughuli za bunge.
Alisema mchakato wa zabuni unaendelea na kwamba, hiyo itasaidia wabunge kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi.
Katibu huyo wa bunge alisema kwa sasa wanatumia simu za mkononi kutoa matangazo mbalimbali ya shughuli za bunge, lakini kuna kipindi kitafika hakutakuwa na haja ya kutumia makaratasi bungeni.
Dk. Kashilila alisema samani zilizowekwa ndani ya ukumbi huo ni imara na kwamba, hata ikitokea vurugu, hakuna mbunge anayeweza kung'oa kiti wala meza katika ukumbi huo.
Kwa mujibu wa Dk. Kashilila, kuanzia leo bunge litaanza kutumia studio yake binafsi, ambapo vituo vingine vyote vya televisheni havitafunga mitambo yao na kurusha moja kwa moja matukio ya bunge kama ilivyokuwa awali.
Badala yake, alisema vituo hivyo vitalazimika kuchukua (kunyonya) matangazo kutoka kwenye studio hiyo.
Alisema studio hiyo tayari imeshakamilika na 'screen' nne zimeshafungwa kwa ajili ya kupokea matangazo kutoka kwenye studio ya bunge.
Akifanya majumuisho ya ziara hiyo, Naibu Spika Tulia alisema, ameridhishwa na ukarabati uliofanywa, ingawa bado haujakamilika na kusisitiza kuwa, vitu ambavyo havijakamilika haviwezi kuathiri shughuli za Bunge.
Mkutano wa tatu wa bunge la 11, unatarajiwa kuanza leo katika kikao chake cha kwanza, ambapo pamoja na mambo mengine, utapitisha miswada miwili ya serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, miswada itakayopitishwa ni wa Sheria ya Matumizi ya mwaka 2016, na Muswada wa Sheria wa Fedha wa mwaka 2016.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, katika kikao hicho serikali inategemea kuwasilisha bungeni miswada ya sheria kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa bungeni baada ya shughuli za kupitisha bajeti kukamilika.
Pia, ilisema kutakuwa na uchaguzi wa mwenyekiti mmoja wa bunge ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kufanya mabadiliko ya wajumbe wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge.
Sambamba na hilo, taarifa hiyo ilieleza kuwa katika mkutano huo, bunge linatarajia kujadili na kupitisha Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano 2015/16-2020/2021 kwa muda wa siku tatu.
Baada ya kukamlika kwa mpango huo, taarifa hiyo ilisema bunge litapokea na kujadili utekelezaji wa bajeti kwa wizara zote kwa mwaka wa fedha 2015/16 na makadirio ya matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, kazi itakayofanyika kuanzia Aprili 22 hadi Juni 2, mwaka huu.
Juni 9, mwaka huu, saa nne asubuhi, waziri anayeshughulika na mipango atawasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa nchi, ikifuatiwa na hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, itakayosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philipo Mpango, kuanzia saa 10 jioni.
"Mjadala wa kuhusu Bajeti ya Serikali utafanyika kuanzia Juni 13 hadi Juni 21, mwaka huu,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika mkutano huo, pia kutakuwa na hati za kuwasilishwa mezani, ambapo bunge litapokea Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15, pamoja na majibu ya serikali kuhusu hoja zilizotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu za mwaka wa Fedha 2014/15.
Pamoja na shughuli hizo, jumla ya maswali 465 yataulizwa na kujibiwa na serikali bungeni, ambapo kila Alhamisi yataulizwa maswali kwa Waziri Mkuu, ambapo jumla ya maswali 88 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa.
Kikao cha leo kitaanza kwa wabunge
wapya watatu wa viti maalumu, kula kiapo cha uaminifu. Wabunge hao ni
Ritha Kabati (CCM), Lucy Owenya
(CHADEMA) na Oliver Semguruka (CCM).
No comments:
Post a Comment