SAKATA la ufisadi
katika ujenzi na uendeshaji wa soko la wafanyabiashara wadogo, Dar es
Salaam, maarufu kama Machinga Complex,
limezidi kuchukua sura mpya baada ya kubainika kwamba, deni la
ujenzi wa jengo hilo limefikia
sh. bilioni 36 kutoka sh. bilioni 12.
Gharama hizo zinatokana
na uzembe mkubwa uliofanywa na baadhi ya watendaji katika ujenzi na uendeshaji wa soko hilo, tangu
lilipoanza kujengwa mwaka 2010, ambapo mkopo
halisi ambao Jiji la Dar es
Salaam, iliupata kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ulikuwa
sh. bilioni 12.7, ambazo ilitakiwa zilipwe baada ya jengo hilo kuanza
kufanyakazi.
Lakini kutokana na wasimamizi wa jengo hilo kuzembea, riba ya deni, ikijumuishwa na deni halisi, limefikia
sh. bilioni 36, ambazo ni mara tatu ya gharama za ujenzi.
Kufuatia kuongezeka kwa gharama hizo maradufu, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, jana, alitanga kuunda tume ndogo ya kuchunguza mkataba wa ujenzi wa jengo hilo.
Makonda alitoa tamko hilo baada ya kuongoza Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Dar es Salaam, kukagua
jengo hilo, akiwa na baadhi ya wajumbe
wake, ambao ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro,
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema,
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi na
Ofisa wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam (RIO), John Msumule.
Alisema kama kuna ufisadi mkubwa uliofanyika hapa
nchini, mmojawapo ni ufisadi wa jengo la Machinga Complex, ambapo aliahidi kula
sahani moja na wahusika wote watakaobainika kwa namna moja au nyingine kuhusika.
Makonda alisema baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Utumishi na
Utawala Bora, George Simbachawene, kutangaza kuvunja bodi ya soko la Machinga
Complex, hivi karibuni na kulikabidhi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ilikaa kikao cha kulitafutia
ufumbuzi suala hilo.
Alisema iliundwa kamati ndogo, ambayo jukumu lake la kwanza litakuwa ni kuuchunguza
na kuupitia mkataba wa ujenzi wa jengo kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko
mkubwa.
Alisema lengo la kuundwa kwa kamati hiyo ni kupata
uhalali wa mkataba wote wa ujenzi, ambapo kamati hiyo ndogo itachunguza kwa
kina mkataba huo na wahusika.
“Tulikopeshwa shilingi bilioni 12.7, kwa ajili ya ujenzi
wa soko hili, lakini mpaka sasa tunadaiwa shilingi bilioni 36. Fedha hizi
mnatakiwa kulipa nyie wafanyabishara mliopanga hapa,”alisema Makonda.
Alisema kamati hiyo ikishapata uhalali wa ujenzi huo,
ndipo itajulikana nani wa kuwajibika.
“Rais wetu Dk. John Magufuli anafanya kila jitihada kutetea haki za wanyonge. Sisi kama wasaidizi wake ni
lazima tuhakikishe tunatekeleza wajibu
huo.
“Lakini sifa ya mnyonge ni lazima awe mkwel, katika
kutoa taarifa sahihi na sifa ya pili ni
lazima achukie rushwa. Hivyo tunawaomba
wafanyabishara na mtu yeyote, ambaye anazo taarifa za jengo hili, atoe
ushirikiano kwa kutueleza ukweli,”alisema.
Alibainisha kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa kila mtu
aliyehusika katika kutoa au kupokea rushwa katika jengo hilo, awe
mfanyabiashara au kiongozi.
Alisema baada ya kujiridhisha na uhalali wa jengo, ndipo wataanza kuangalia utaratibu wa
kupangisha wafanyabishara kwa kujali
zaidi maslahi yao kwani serikali
iliwajengea jengo hilo ikiwa na nia njema ya kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment