Wananchi wakimsikiliza mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli alipowahutubia kwenye viwanja vya Tangamano |
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni mgombea Ubunge wa Jimbo la Bumbuli Mhe. January Makamba akihutubia wakazi wa mji wa Tanga kwenye mkutano wa kampeni za CCM |
Naibu Waziri wa Fedha na mgombea ubunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akihutubia wakazi wa Tanga mjini kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Tangamano |
Umati wa wananchi (picha ya juu na chini) uliofurika kumsikiliza Dk Magufuli alipokuwa akiwahutubia mjini Tanga juzi |
NA SELINA WILSON,
TANGA
MGOMBEA urais wa CCM, Dk.
John Magufuli, amesema akipata ridhaa ya wananchi atarejesha heshima ya Jiji la
Tanga kwa kufufua na kujenga viwanda ili kufungua fursa za kiuchumi.
Amesema miaka iliyopita
watu wa mikoa mbalimbali walikua wanakimbilia Tanga kutafuta ajira kutokana na
kuwepo viwanda vingi vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Dk. Magufuli alisema
hayo jana kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu
aliyoifanya katika Wilaya za Muheza, Pangani na Tanga Mjini katika mkutano
mkubwa uliofanyika Uwanja wa Tangamano.
Alisema serikali yake
itajenga viwanda vya samaki katika maeneo ya ukanda wa Pwani ili kuhakikisha
rasimali hiyo inawanufaisha Watanzania hususan wananchi wa maeneo hayo.
“Tutajenga viwanda ili
tudhibiti hata wezi wanaokuja kwenye bahari yetu kuvua samaki. Tutashusha bei
ya vifaa vya uvuvi ili wanaofanya shughuli hizo wanufaike na rasilimali za nchi
yao,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli aliwataka
wanaotaka kuja kuwekeza hapa nchini wajitokeze kwa kuwa milango ipo wazi kwa
ajili ya viwanda ikwemo vya matunda vitakavyowezesha wananchi kusafirisha juisi
kwenda kwenye masoko badala ya kusafirisha machungwa.
“Tutavifufua viwanda
vyote vilivyofungwa ili vifanye kazi ya uzalishaji na Watanzania hususan vijana
wapate ajira. Tanzania ni nchi tajiri, tutatumia utajiri huo kuwanufaisha
Watanzania wote,”alisema Dk. Magufuli.
Akiwa Pangani, Dk.
Magufuli alisema serikali yake kuanzia mwakani itaanza ujenzi wa Daraja ya Mto
Pangani ili kuhakikisha wananchi wanarahisishiwa usafiri kati ya Pangani na
wilaya zingine ikiwemo Bagamoyo mkoani Pwani.
Pia, alisema serikali
itanunua kivuko kipya ambacho kitakuwa kinafanya kazi wakati wa ujenzi wa
daraja na kwamba tayari wataalamu wameshanza kufanya upembuzi yakinifu kwa
ajili ya maandalizi ya ujenzi wa daraja hilo.
“Nikiwa Waziri wa Ujenzi
nilinunua Kivuko cha MV Pangani ambacho kinaendelea kutumika mpaka sasa na
kinatumiwa na wananchi wote bila kujali itikadi zao, hivyo nawaomba wananchi mniamini
ili niwatumikie,” alisema.
Dk. Magufuli aliahidi
ujenzi wa barabara ya lami kilometa 178 kutoka Tanga/Pangani/Saadan hadi
Bagamoyo.
Katika hatua nyingine,
alisema chini ya utawala wake wazee hawatalipa nauli kwenye Kivuko cha MV.
Pangani kwa kuwa ni watu wazima wanaohitaji kuendelea na shughuli zao bila
kuhangaika.
Dk. Magufuli alisema
watu wanaweza kuona ni siasa, lakini msimamo wake ni kutekeleza miradi yote na
kwamba fedha zipo isipokuwa kuna mafisadi ambao wanatumia fedha za serikali
vibaya na kuwa akiingia Ikulu atapambana nao na kufikisha huduma kwa wananchi.
Akiwa Muheza, Dk.
Magufuli alisema ana dhamira ya kutatua tatizo la muda mrefu la maji katika mji
huo na kwamba atatatua kero hiyo katika kipindi kifupi baada ya kuingia
madarakani.
Akimnadi, Mgombea
ubunge wa jimbo hilo , Balozi Adadi Rajabu, Dk. Magufuli alisema anamfahamu ni
mtu mfuatiliaji ambaye atahakikisha anafanya naye kazi bega kwa bega.
“Adadi ni rafiki yangu
ambaye ninakwenda kwake usiku na mchana…ni mfuatiliaji wa mambo kama
mimi…alikuwa mchapakazi hodari alipokuwa katika majeshi na hata kama balozi,”
alisema Dk. Magufuli na kuwa CCM imefanya jambo jema kuteua jembe hilo.
Awali, akizungumza
katika mkutano wa kampeni wa Muheza, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba,
alisema Dk. Magufuli ni mgombea mwenye sifa kuzidi wagombea wote wanaowania
urais mwaka huu.
Makamba alisema , Dk.
Magufuli ana sifa za elimu, anao uwezo wa kuongoza nchi kwa kuwa ni mchapa kazi
na hana kashfa katika utendaji wake.
Akizungumza katika
mkutano wa hadhara, Mgombea Ubunge wa Viti Maalumu na Mujumbe wa Baraza Kuu la
UWT, Ummy Mwalimu, alisema Wanawake wa Mkoa wa Tanga wana kila sababu ya
kumpigia kura Dk. Magufuli kwa kuwa ni
muadilifu na mchapa kazi.
“Wanawake tunafahamu
unao uwezo wa kutuvusha Watanzania. Kubwa zaidi ni kwamba umetupa heshima
wanawake kwa kumteua Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza na kuandika historia ya
Tanzania kupata Makamu wa Rais mwanamke,” alisema.
Katika mikutano ya
kampeni, Dk. Magufuli aliwapokea wanachama zaidi 20 kutoka CHADEMA walioamua
kukihama chama hicho huku wakieleza kukerwa na utaratibu wa kuwatumia vijana
bila kuwanufaisha.
Akizungumza mjini
Muheza kwa niaba ya wenzake, kijana maarufu, Rashid Nassor Rashid , alisema
alikuwa mpiga debe maarufu wa CHADEMA na ana kundi kubwa la vijana wenzake
wameamua kuhama kwa kuwa wanahitaji mabadiliko ya kiuchumi ambayo wanaamini
watayapata kwa Dk. Magufuli.
Kabla ya kuhutubia
mikutano ya Muheza, Pangani na Tanga Mjini, Dk. Magufuli akitokea Handeni alilazimika
kusiamama na kuzungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkata, Kabuku, Michungwani, Hale, kutokana na
hamasa ya wananchi kutaka kumsikiliza.
No comments:
Post a Comment