Wednesday 9 September 2015

WATENDAJI WAASWA WASIANZE KUJENGA HOFU KWA MAGUFULI


Na Angela Sebastian, Missenyi
WATENDAJI wa serikali na taasisi mbalimbali  nchiniwametakiwa kuacha woga dhidi ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli.

Badala yake wampe kura za ndiyo ili aweze  kupata nafasi hiyo na kufanya jitihada za kurekebisha mambo ikiwemo  kuongeza kasi katika utendaji.

Rai hiyo ilitolewa jana Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye, wakati wa uzinduzi wa kampeini za mgombea ubunge wa Jimbo la Nkenge, Balozi Dk. Diodorus Kamala.

Uzinduzi  huo uliofanyika kiwilaya katika Kata ya  Ishozi, Tarafa ya Kiziba, uliwajumuhisha wagombea wote wa viti vya udiwani kutoka kata 20 zilizo ndani ya wilaya hiyo.

Costansia alisisitiza kuwa chama cha mapinduzi kina imani kubwa na mgombea wake Dk. Magufuli kutokana na uadilifu, uchapakazi na uwajibikaji, sifa ambazo zinatosha kwa kiongozi anayepaswa kuliongoza taifa la Watanzania.

Alisema baadhi ya watumishi na watendaji katika idara nyingi za umma wameonyesha kujawa na woga juu ya ukali wa kiongozi huyo (Dk.Magufuli) pindi atakapochukua madaraka na wengi wakiwa na hofu juu ya nafasi zao za kazi kutokana na uzembe katika utendaji wa kazi za umma

“Nawaomba kuondokana na hofu badala yake jirekebisheni na mfanye kazi kwa umakini na uadilifu mkubwa kama wewe ulikuwa unaenda kinyume na maadili ya kazi yako, anza sasa kubadilika ili uweze kwenda na kazi ya kiongozi huyu,”aliwashauri  Costansia.

Aliongeza kuwa Dk. Magufuli ni kiongozi anayejali maslahi ya watumishi wa serikali, haki za raia wote wakulima na wafugaji na chama kina imani kubwa kuwa Ilani ya CCM mwaka 2015/2020 itatekelezwa kwa asilimia kubwa, kwani mgombea huyo anakubalika na anatosha kwa kiwango kikubwa kwa Watanzania wanaohitaji mabadiliko ya kweli.

Kwa upande wake, Dk. Kamala, aliwahakikishia wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kampeini hizo kumpa kura  mgombea urais wa CCM kwani ni mtu wa vitendo na mchapa kazi asiyetiliwa mashaka.

Balozi Kamala alisema tayari ameisoma vyema ilani ya uchaguzi ya CCM  na ana imani kubwa ataitekeleza iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo na kuwaomba wananchi jimboni humo kuwa na imani nae na kuwachagua madiwani wote 20 wanaotokana na CCM.

Aidha, pamoja na kueleza kuwa ameisoma ilani hiyo, tayari ameibani kuwepo baadhi ya mambo ambayo anaweza kuyatekeleza nje ya mipango ya serikali kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje  ya nchi,lengo kuu likiwa kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wa jimbo la Nkenge.

Katika kuhakikisha anatekeleza ilani hiyo, Dk.Kamala,alibainisha baadhi ya mambo muhimu atakayoanza nayo mara atakapokuwa amechaguliwa ambayo ni kupambana na umasikini kwa vitendo, hasa kuhakikisha sh. milioni 50 inayoelezwa kutolewa kwa kila kijiji ili kupunguza umasikini inapatikana kwa muda mwafaka.

Pia,  alieleza dhamira yake ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi katika shughuli za mikono kwa kutumia umeme ambao tayari umekuwepo vijijini, jambo ambalo litaongeza kasi ya vijana kujipatia ajira kirahisi baada ya kupata ujuzi.

No comments:

Post a Comment