Wednesday 9 September 2015

SHAKA AKOSOA WANAOFIKIRI KUHUSU CCM KUSHINDWA



Na Mwandishi Wetu, Mafinga

KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Shaka Hamdu Shaka, amesema vyama vya upinzani vinavyofikiri CCM itashindwa katika uchaguzi wa mwaka huu kama ilivyotokea kwa vyama vingine  vilivyopigania ukombozi Afrika, hawajui ukweli wa historia na harakati za kisiasa.

Vyama hivyo ni KANU (Kenya) UNIP (Zambia) MCT (Malawi) na UPC (Uganda).

Shaka aliyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa CCM na jumuia zake kwenye mkutano uliofanyika katika ofisi za CCM Wilaya ya  Mufindi mkoani Iringa.

Alisema kuanguka kwa vyama  hivyo hakuwezi kuwa kigezo cha kuiondoa CCM kwa kuwa imejijenga na kuwa taasisi yenye sera na mfumo imara unaofahamika na kuheshimika .

Alisema mara zote tangu enzi za TANU na ASP hadi CCM, Chama kimekuwa kikijali na kuthamani umuhimu wa dhana ya  maendeleo ya wananchi, kuimarisha huduma za jamii na kutanua wigo wa demokrasia jambo ambalo huenda lilichangia kudondoshwa kwa vyama hivyo licha ya kazi kubwa vilivyofanya katika kupiginia uhuru na ukombozi kusini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa Shaka, katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM itaibuka na  ushindi mkubwa kuliko ilioupatikana  mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 kwa kuwa katika vipindi vyote  sera za CCM zimeleta manufaa kiuchumi na kijamii , msukumo wa maendeleo, umoja na kudumisha  amani na utulivu.

“Wanaofikiri CCM itaanguka madarakani kama ilivyotokea kwa vyama vingine vya ukombozi wanatwanga maji kwenye kinu, Chama chetu wakati wote kimekuwa karibu na wananchi, kikijali na kuthamini utu wa kila mmoja na kuleta maendeleo yanayoonekana,” alisema Shaka.

Aidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete , CCM imeleta mageuzi ya msingi ya kiuchumi, kidemorasia na kijamii huku sera za CCM zikionyesha dhamira ya kujenga usawa, haki na kuendeleza utawala wa sheria bila kutumia itikadi za ukabila, udini au ubaguzi na kukandamiza wananchi.

Shaka alisema tangu awamu ya kwanza hadi ya nne, CCM na serikali zake licha ya kupigania na kushiriki harakati za ukombozi kusini mwa Afrika,  haikupuuzia  kuwaunganisha wananchi na kuwajenga kiitikadi kwa kuamini kuwa binadamu wote ni sawa na Afrika  ni moja.

“Tanzania imeshiriki ukombozi Kusini mwa Afrika, imeijenga misingi ya haki, usawa, maendeleo na demokrasia. Vyama vya upinzani vimeshindwa kuja na sera mbadala, hivyo havina ubavu wa kuishinda CCM kwa sasa na wakati mwingine wowote,” alisema Shaka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi, Jimson Mhagama, alisema wana-CCM wilayani humo wameendelea kuwa wamoja na kwamba hiyo ni dalili njema ya kufanikisha ushindi wa kishindo.

“Katika uchaguzi wa serikali za mitaa tumeshinda kwa zaidi ya asilimia 99.5, hizo zilikuwa ni salamu kwa uchaguzi mkuu, tunaamini wimbi hilo litaendelea na hakuna chama cha upinzani kinachoweza kutuzuia,” alisema.

Alisema CCM imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza ahadi zake kwa wana-Mafinga ikiwemo kuimarisha huduma za afya, mawasiliano, miundombinu na elimu.

“Mgombea urais wa CHADEMA Edward Lowassa na mpambe wake Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye watafute maneno mapya yatakayowasaidia kupata kura, lakini si kwa kutoa ahadi ambazo tayari serikali ya CCM inaendelea kuzifanyia kazi kwa kasi kubwa na kuleta tija kiuchumi na kijamii,” alisema Mhagama.

Shaka amemaliza ziara yake mkoani Iringa ambapo jana alitarajiwa kwenda Mkoa wa Njombe.

No comments:

Post a Comment