Wednesday 9 September 2015

SAMIA: SERIKALI KUJENGA VIWANDA VIDOGO NYASA



 Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia Suluhu akishuka kwenye ndege baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege mjini Songea kuanza kampeni za CCM
 Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Mama Samia akisalimia baadhi ya viongozi baada ya kuwasili mjini Songea
Mama Samia akihutubia mkutano mdogo wa kampeni uliofanyika Kingerikiti wilayani Nyasa mkoani Ruvuma
 Mama Samia akimnadi mgombea Ubunge Injinia Stela Manyanya katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kingerikiti wilayani Nyasa mkoani Ruvuma
Wananchi wakishangilia katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kingerikiti wiayani Nyasa mkoani Ruvuma
 NA ABDALLAH MWERI, NYASA

SERIKALI inatarajia kujenga viwanda vidogo kwa wakazi wa Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma ili kuwaokomboa wananchi kiuchumi baada ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Kauli hiyo ilitolewa jana na mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, alipozungumza katika mkutano wa hadhara na wakazi wa Kijiji cha Tingi, Wilaya ya Nyasa.

Samia, alisema serikali ya awamu ya tano ikiingia madarakani, itajenga viwanda vidogo vya kahawa na kukoboa mahindi, ambavyo vitakuwa na ustawi kwa wakazi wa Nyasa.

Alisema serikali ya awamu ya tano inatarajia kutoa sh. milioni 50 katika kila kijiji na viwanda hivyo vitajengwa kupitia fedha hizo kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya wakazi wa Kijiji cha Tingi, kilichoko Kata ya Tingi, Tarafa ya Tingi.

Samia, aliwataka wakazi wa Tingi kumchagua Dk. John Magufuli kuwa rais wa awamu ya tano katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema ana matumaini makubwa fedha hizo zitakuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa wakazi wa Tingi, ambao watajikomboa kupitia viwanda vidogo vya kahawa na kokoboa mahindi.

"Jamani wakazi wa Tingi msifanye kosa katika uchaguzi mkuu ujao, nawaombeni sana mpeni kura Dk. Magufuli afanye kazi. Ni mchapakazi hodari, ambaye mnajua uwezo wake katika wizara mbalimbali," alisema Samia huku akishangiliwa.

Pia, aliwataka wakazi wa Tingi kupuuza kauli za wapinzani ambao wamejipanga kutoa fedha sh. 1,500 kununua shahada za kupigia kura baada ya kuona wameshindwa kutoa ushawishi kwa wananchi.

Samia aliwataka wakazi wa Nyasa kutunza shahada hizo hadi tarehe ya uchaguzi, na wakapige kura kwa kumchagua Dk. Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM katika uchaguzi huo.

"Msikubali kuhadaika na baadhi ya watu wanaojipitisha kuwadanganya kununua shahada zenu, msikubali kamwe na muwapuuze, nawaomba sana tunzeni shahada zenu na mchague CCM katika uchaguzi mkuu," alisema Samia.

Aidha, alisema kituo cha afya cha Tingi kitapandishwa hadhi na kuwa hospitali, ambayo itakuwa na vifaa bora, madawa na wafanyakazi wa kutosha, ambao wataleta tija na ustawi kwa wakazi wa Tingi.

Pia, alisema serikali ya awamu ya tano itandeleza ujenzi wa barabara zikiwemo za Wilaya Nyasa ili kuwakomboa kiuchumi wakazi wa Tingi na vitongoji vyake.

Samia aliwataka wakazi wa Tingi kumchagua Injinia Stella Manyanya kuwa mbunge wa Nyasa kwa sababu ni mtendaji hodari na amefanya naye kazi kwa muda mrefu, hivyo anatambua uwezo wake.

Mgombea mwenza alitembelea vijiji mbalimbali vikiwemo vya Kingerikiti, ambapo msafara wake ulikuwa ukisimamishwa mara kwa mara na wakazi wake kwa lengo la kuwasalimia. Samia leo anatarajia kufanya kampeni katika vijiji vya Lusewa, Magazini, Nalasi, Mbesa na Tunduru Mjini.

No comments:

Post a Comment