Tuesday 8 September 2015

MWIGULU: IKULU HAPALEKWI MTU KUJAZA NAFASI


NA ANITA BOMA,IRINGA

WANANCHI wa Manispaa ya Iringa mkoani Iringa, wametakiwa kumchagua mgombea urais atakayekwenda Ikulu kwa ajili ya kufanyakazi za kuwatumikia wananchi na sio kujaza nafasi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akizindua kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), za kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Iringa Mjini.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya sekondari Mwembetogwa na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, Mwigulu alimnadi mgombea huyo, Frederick Mwakalebela na kuwataka wananchi kumpigia kura kwa wingi ili akawawakilishe bungeni.

Mwigulu, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, kabla ya kujiuzulu ili agombee urais, alisema wananchi wa Iringa Mjini wanapaswa kutafakari mambo matatu muhimu, wapi walikotoka, walipo sasa na wanapokwenda kabla ya kumchagua mbunge wao.

Alisema ushabiki unaofanywa sasa na vijana hauzingatii mambo hayo na ipo hatari ya kuwachagua wabunge na madiwani wasiokuwa na sifa na uwezo wa kuwawakilisha bungeni.

Mwigulu alisema pia kuwa, huu si wakati wa wananchi kumchagua mgombea urais kwa kigezo cha mahaba, badala yake wazingatie rekodi, sifa na uwezo wake.

Alisema Oktoba 25, mwaka huu, sio siku ya kuendekeza ushabiki wa vyama vya siasa, badala yake wananchi wanatakiwa kuchagua wagombea watakaowasaidia kuwaletea maendeleo.

"Hii ni siku ambayo wananchi mnatakiwa kumchagua mgombea urais atakayekwenda Ikulu kufanyakazi usiku na mchana kwa ajili ya kuwaletea maendeleo. Urais sio nafasi ya kimzahamzaha, ni nafasi anayostahili kupewa mtu makini, mwadilifu na mchapakazi,"alisema.

Mwigulu alisema hakuna mgombea urais mwenye uwezo wa kupambana na yule wa CCM, Dk. John Magufuli katika kuwania urais mwaka huu, kwa vile anazo sifa zote zinazostahili kwa nafasi hiyo.

Alisema wananchi wameshawasikiliza na kuwaelewa vya kutosha wagombea wote wanaowania urais katika uchaguzi huo mwaka huu na kwamba hakuna anayeweza kufananishwa na Dk. Magufuli.

Aliwaonya wananchi kuepuka kupokea rushwa ili kuwafanyia kampeni na kuwachagua wagombea wasiokuwa na sifa kwa kuwa kufanya hivyo ni kujirudisha nyuma kimaendeleo.

Alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa mabingwa wa kuifananisha Tanzania na nchi zingine zilizoendelea bila kujua kuwa nchi hizo hufanya maamuzi yake kwa umakini na kuwaweka madarakani watu wenye sifa na uwezo.

Mwigulu alisema CCM iliamua kumteua Dk. Magufuli kugombea nafasi hiyo kwa vile alikidhi vigezo vyote vilivyotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuwa na rekodi nzuri ya uchapakazi.

“Kati ya wagombea urais wa vyama vyote vya siasa hapa nchini na wale waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ndani ya CCM, hakuna hata mmoja anayemfikia Dk. Magufuli kwa uadilifu na uchapakazi pamoja na ufuatiliaji wa mambo na kuchukua hatua kwa wakati. Pia hajazungukwa na watu wa dili wala mtandao wa wakwepa kodi,"alisema Mwigulu huku akishangiliwa na wananchi.

Aliongeza kuwa wingi wa watu katika mikutano ya kampeni ya uchaguzi sio kigezo cha wagombea wa vyama hivyo kukubalika, bali wananchi wanataka kusikiliza ilani na sera za wagombea.

Mwigulu alisema mgombea urais aliyesimamishwa na UKAWA, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, alianza kugombea nafasi hiyo tangu mwaka 1995, lakini alikuwa akikatwa kutokana na kutokuwa na sifa.

"Huyu mgombea wa upande wa pili, tangu enzi za Mwalimu Nyerere, alikuwa mtu wa kupiga dili tu, hana sifa za kwenda Ikulu na haiwezekani tumpeleke Ikulu kwa kuwa sehemu ile ni mahali patakatifu,"alisema.

Alisema katika kudhihirisha kutokubalika kwake, mgombea huyo amekuwa akitumia vibaya hotuba za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere katika mikutano yake ya kampeni ili kuwashawishi wananchi wamchague.

“Ni kweli Baba wa Taifa alituasa kwa kusema kuwa Watanzania wasipopata mabadiliko ndani  ya CCM, watayapata nje ya CCM, lakini hawaimalizii hotuba hiyo hadi mwisho alipozungumzia masuala ya rushwa na ufisaidi,"alisema.

Alisema Lowassa si mwadilifu na hata Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na viongozi wenzake wa chama hicho walikuwa wakimwita fisadi wakati alipokuwa CCM, hivyo inashangaza kuona kwa sasa wamemkumbatia na kumwita mtu safi.

Mwigulu alisema jitihada zinazofanywa na viongozi wa UKAWA kumsafisha Lowassa haziwezi kufanikiwa kwa kuwa mwanasiasa huyo hawezi kusafishika.

Akimnadi mgombea ubunge wa Iringa Mjini, Mwakalebela, Mwigulu alisema ndiye pekee atakayeweza kuwaletea maendeleo, badala ya mbunge aliyemaliza muda wake, Mchungaji Msigwa.

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano, ambacho Mchungaji Msigwa alikuwa mbunge wa jimbo hilo, ameshindwa kuwaletea maendeleo yoyote zaidi ya kupinga mambo mazuri yaliyokuwa yakifanywa na serikali ya CCM.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwakalebela alisema yeye ni mtoto aliyezaliwa na kukulia mkoa wa Iringa, hivyo anayafahamu matatizo na changamoto zote zinazowakabili wakazi wa mji huo.

Aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutompa kura Mchungaji Msigwa kwa vile katika kipindi chote cha miaka mitano alichowatumikia, alikuwa muhamasishaji mkubwa wa maandamano badala ya maendeleo.

Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisema Chama kimejipanga vyema kuhakikisha kinashinda majimbo yote katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

"Wananchi msisumbuke kupoteza kura zenu kwa Mchungaji Msigwa, ninalo faili la kila kata na kiasi cha pesa za mfuko wa jimbo, ambazo zingepaswa kufanyakazi ya jimbo, lakini zilikuwa zikiishia mfukoni mwake,"alisema.

Alisema ni vyema wakazi wa Iringa Mjini wamuhoji mbunge huyo fedha hizo zilivyotumika na kwamba iwapo atashindwa kutoa maelezo, wasimpe kura zao.

No comments:

Post a Comment