Tuesday 8 September 2015

JK; WANAWAKE WANA MASLAHI MAPANA NA UCHAGUZI MKUU




NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete amesema wanawake nchini wana maslahi maalumu na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa sababu kwa mara ya kwanza wanaweza kutoa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, amesema wanawake wana maslahi makubwa katika uchaguzi kwa sababu safari ya Tanzania kupata rais mwanamke imeanza kwa chama kimoja cha siasa kuteua mgombea mwenza mwanamke.
Rais Kikwete pia amesema wanawake wa Tanzania wanastahili kuwa na maslahi yasiyokuwa ya kawaida katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa sababu uchaguzi huo unaweza kuamua kama Tanzania inaendelea kuwa ya amani na utulivu ama inaingia katika machafuko kulingana na matokeo ya uchaguzi.
Alisema hali ya machafuko itawaathiri zaidi wanawake na watoto.
Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema hayo alipokuwa akizungumza na makatibu wa mikoa na wilaya wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).
Hafla hiyo ilihudhuriwa na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli.
Alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Chama kimemteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza na kwamba ni mara ya kwanza kwa CCM kumteua mwanamke kuwa mgombea mwenza.
Rais Kikwete alisema wanawake wote wa Tanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa, wanastahili kuwa na maslahi maalumu na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa sababu kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, wanawake wanaweza kupata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Tanzania mwanamke.
“Nyie kinamama wa CCM na kwa hakika wanawake wote wa Tanzania mnastahili kuwa na maslahi maalumu na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa sababu katika historia ya nchi yetu, nchi hii ya Tanzania inaweza kupata Makamu wa Rais mwanamke. Imekuwa safari ndefu na yenye changamoto nyingi,” alisema Rais Kikwete.
“Kuteuliwa kwa Samia Sululu Hassan ni ishara kuwa safari ya Tanzania kuwa na Rais mwanamke imeiva, iwezesheni safari hiyo ifanikiwe katika nchi yetu nyie kinamama.
“Na wala uteuzi wa Samia haukuwa wa bahati mbaya. Mgombea Urais wa CCM, Dk. Magufuli alitaka mwanamke awe ndiye mgombea mwenza,” alisisitiza.  
Rais Kikwete alisema uteuzi wa Samia hakuwa wa bahati mbaya kwa sababu tokea mwanzo CCM ilitaka kuwa na mgombea mwenza mwanamke.
Alisema hakukuwa na jina la mwanaume lililojadiliwa katika vikao vya uteuzi.
“Huu ulikuwa mwendelezo wa sera zetu kwa kina mama. Mtakumbuka kwa mara ya kwanza katika mchakato wetu wa kutafuta mgombea urais, kina mama wawili waliingia katika tano bora kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na wawili hatimaye wakaingia katika tatu bora kwenye mkutano mkuu kabla ya kuteuliwa Dk. Magufuli,” alisema.
Alisema: “Hata kwenye Katiba Inayopendekezwa, CCM ilipigia na imepata asilimia 50-50 ndani ya Bunge kati ya wanawake na wanaume. Haya mnayoyaona siyo ya bahati mbaya hata kidogo. Ni sera za makusudi za kumwinua mwanamke wa Tanzania.”
Kuhusu hali ya baadaye ya Tanzania baada ya uchaguzi, Rais Kikwete alisema lugha za vyama vinavyowania kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu huo zinaonyesha kuwa wanawake wa Tanzania lazima wachague kati ya amani na utulivu ama machafuko na umwagaji damu.
“Mnasikia wenyewe, sisi siku zote tunahubiri amani na utulivu kama msingi mkuu wa maendeleo ya nchi yetu, wenzetu wale wanahubiri habari ya nchi hii itamwaga damu, wanajiandaa kumwaga damu ya Watanzania, lakini kama nilivyopata kusema huko nyuma huu ni moto wa mabua.
“Mwanzoni walidhani kuwa nchi haina wenyewe, nadhani sasa wameanza kugundua kuwa nchi hii ina wenyewe, nyie wananchi wa Tanzania,” alisema Rais Kikwete.

No comments:

Post a Comment