Tuesday 8 September 2015

MAKONGORO NYERERE AZIDI KUTOA DOZI KWA LOWASSA



NA SOLOMON MWANSELE, KYELA

MJUMBE wa Kamati ya Kampeni ya CCM Taifa, Makongoro Nyerere, amesema hakuna kiwanda kinachoweza kutengeneza sabuni ya kumsaficha mgombea Urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, kwani ni mchafu na hastahili kuwania nafasi hiyo.

Alisema anawaonea huruma CHADEMA na UKAWA kwa jumla, kwani Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond ni fisadi, mchafu na mchonganishi na ndio maana CCM ilimkataa kwa kumwambia wazi kuwa hawezi kufaa kuwania Urais.

“CCM imethubutu kuwaumbua hawa wezi, mafisadi na wala rushwa wakiwemo Lowassa na Sumaye na wameamua kupeleka UKAWA. Leo hii Lowassa kawafumba mdomo viongozi wa CHADEMA, hawana jeuri ya kuzungumza kuhusu ufisadi,” alisema Makongoro.

Aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM jimbo la Kyela, ambapo aliwanadi mgombea ubunge Dk. Harrison Mwakyembe na wagombea udiwani kwenye mkutano uliohudhuriwa na mamia ya wananchi uliofanyika Kata ya Ipinda, wilayani Kyela.

Makongoro alisema Lowassa leo hii kamwe hampi mashiko kwa sababu hata afya yake si nzuri na kuuchekesha umati wa wananchi uliohudhuria mkutano huo kuwa mtu unaweza kumuandama mgonjwa na bahati mbaya Mungu akamchukua na wewe ukaonekana umemroga.

Aliongeza kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, walimwambia wazi Lowassa na vibaka wenzake kuwa hawatachaguliwa na kweli ikawa hivyo, ambapo Lowassa akiwa CCM kuna wenyeviti wa Chama kutoka mikoa 10 walikuwa wanasikiliza na wakatishia eti asipochaguliwa ataondoka na wengi.

“Hadi leo hii ni wenyeviti wawili tu ndio waliondoka, na wale wanane waliobaki CCM hivi sasa wameanza kufuata utaratibu wa Chama… CCM hakitoki madarakani kwa sababu ni urithi wetu, hivyo Watanzania wataendelea kuichagua,” alisema Makongoro na kushangiliwa.

Alisema CCM ni Chama cha wanyonge yaani wakulima na wafanyakazi ambao ndio wengi na kuwashangaa baadhi ya wanasiasa wanaodai kuwa wanataka kuikomboa Tanzania wakati wanatambua fika nchi hii tayari ilikwisha kombolewa.

Makongoro aliongeza kuwa leo hii shauri ya watu wachache wasiozidi 20 wameifikisha CCM mahali ilipo kiasi cha wanachama wengi wamekuwa wanaambiwa ni wala rushwa na mafisadi wakati hilo si sahihi hata kidogo.

Kwa mujibu wa Makongoro, viongozi walioaminiwa na wana-CCM na kupewa uongozi wametumia nafasi hizo kukidhalilisha Chama na wanachama wake, na kuwaomba wananchi wa Kyela na Watanzania kwa jumla kuirudishia CCM heshima yake kwa kumchagua mgombea Urais Dk. John Magufuli, mbunge Dk. Mwakyembe na wagombea udiwani wote.

Aliongeza CCM ina nidhamu na ndiyo maana wakiwa ndani ya vikao vya Chama huwa wanasemana na kuwa ameishwahi kumueleza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kwamba Lowassa na Rostam Aziz ni wachafu na wanakichafua Chama.

Makongoro alisema CCM ilikuwa inafanya makosa ya kiufundi, na hilo lilitokana na uwepo wa kundi la mafisadi ndani yake, wakiwemo hao watatu aliowataja na ndio maana akiwa katika mchakato wa kuwania Urais ndani ya CCM, alisema umefika wakati wa watu wachache wakirudishe Chama kwa wenye nachon yaani wakulima na wafanyakazi.

“CCM ndio kimbilio la Watanzania walio wengi, hivyo kamwe hatuwezi kukiacha, hawa mafisadi wameanza kutugawa na kutufitinisha Watanzania…nilichukua fomu za kuomba Urais ndani ya CCM ili niweze kusema mawili, matatu kwa Watanzania. Niliwaeleza watu hawa waturudishie Chama,” alisema.

Makongoro ambaye ni mmoja wa wajumbe wa timu ya makada 32 ya kampeni kitaifa, alisema wale wote waliokuwa wanakichafua Chama kwa tuhuma za ufisadi na kutaka kukisambaratisha leo hii wameondoka, hivyo ni vyema Watanzania wakamchagua Dk.Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM.

Aliongeza tangu Lowassa ahamie CHADEMA, amewafunga midomo kina Freeman Mbowe, kuzungumzia ufisadi na waliobaki wakizungumzia kuhusu ubaya wa ufisadi kwa maendeleo ya taifa ni Dk. Magufuli, Dk. Mwakyembe na yeye.

“Lowassa ni kiboko tangu aingie CHADEMA,  Mbowe na wenzake waliokuwa vinara wa kuuchukia ufisadi, wanashindwa kufungua midomo kumueleza Lowassa kuhusu ufisadi wake. CCM kulikuwa na maradhi, lakini sasa yamehamia CHADEMA na UKAWA na sasa wataipata vizuri,” alisema Makongoro.

POLISI YATAWANYA CHADEMA
Polisi wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA waliowafanya vurugu kwenye uzinduzi wa mkutano wa kampeni za CCM jimbo la Kyela.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi wana-CCM, wananchi, wapenzi na mashabiki wa Chama ulifanyika katika Kata ya Ipinda, wilayani humo.

Hata hivyo, polisi walilazimika kupiga bomu moja la kutoa machozi baada ya vijana wanaodaiwa ni wafuasi wa CHADEMA kuanza kuwafanyia fujo wanaCCM waliokuwa wanaenda kushiriki kwenye uzinduzi huo, ambao mgeni rasmi alikuwa Makongoro Nyerere.

Wakati wa upigaji wa mabomu hayo ya kutoa machozi, Mwenyekiti wa Chama wilayani humo, Dk.Hunter Mwakifuna, Katibu Eva Degeleki, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk. Harrison Mwakyembe na Makongoro, walikuwa hawajafika viwanjani hapo.

Wakati burudani zikiendelea kutumbuiza ghafla kijana mmoja aliyekuwa amevaa picha ya mgombea wa CHADEMA alivamia mkutano huo na kujikuta katika wakati mgumu baada ya kuzungukwa na wana-CCM waliomhoji sababu ya kuvamia mkutano wao.
“Nyie jana mmefanya uzinduzi wenu na sisi hatukuwafanyia vurugu yoyote sio kwamba tunashindwa, lakini tulitii maagizo ya viongozi wetu akiwemo Dk. Makyembe hivyo kimewauma mnataka kutuchokoza, ngoja tukupe dawa ukawasimulie na wenzako,” alisema mmoja wa watu waliokuwepo.

Kuona hivyo kijana huyo alifanya purukushani na kufanikiwa kuchomoka kutoka kwenye kundi hilo na kutimua mbio huku akifukuzwa na vijana wa CCM na ndipo ghafla ilipotokeza gari ya polisi aina ya Land Rover na askari kuamua kutumia mabomu ya machozi ili kuwatanya.

Baada ya hali ya hewa kutulia, lori aina ya Fuso likiwa limejaza wafuasi wa CHADEMA huku ndani yake wakiwa wamewabeba watoto wadogo likiwa limefungwa bendera lilipita kwenye mkutano huo huku vijana hao wakiimba nyimbo za chama hicho.

Kuona hivyo, gari la polisi lililokuwa linafanya doria liliwahi gari hilo na kusimama mbele yake hali iliyomfanya dereva asimamishe, hivyo kufanya vijana wa CCM na wanachama waliokuwa kwenye mkutano huo kuamua kutaka kuwavamia.

Polisi baada ya kuona hali hiyo walilazimika kufyatua mabomu ya machozi ili kuwatanya wafuasi wa vyama vyote hali iliyoleta mtafuruku mkubwa huku watu wakikimbia ovyo na kulifanya eneo hilo kuwa na taharuki.

Akizungumza na wana-CCM na wananchi hao Dk. Mwakyembe alisema huo si utamaduni wa wananchi wa jimbo la Kyela na kuonya kuwa siasa za aina hiyo ambazo hazina mashiko hazitakiwi kuachwa kuota mizizi wilayani humo.

“Nilizungumza na wana-CCM jana na kuwasihi wasikatize kwenye mkutano wa CHADEMA wakiwa wamevaa sare za Chama, lakini wanaweza kwenda kusikiliza…sasa nashangaa wenyewe leo kinawauma na wamevamia mkutano wetu,” alisema Dk. Mwakyembe.

No comments:

Post a Comment