Monday, 15 August 2016
JPM: ACHENI KUITUMIA CCM KUNUFAISHA MATUMBO YENU
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli amesema anataka viongozi wa Chama wawatumikie wananchi na sio kukitumia kunufaisha matumbo yao.
Ameonya kuwa yeyote atakayebainika kutoa hongo ili achaguliwe wakati wa uchaguzi mkuu wa Chama, utakaoanyika Novemba, mwakani, hatapitishwa kugombea nafasi atakayoomba.
Dk. Magufuli alisema hayo juzi, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Busisi, wilayani Sengerema mkoani Mwanza, wakiwemo viongozi mbalimbali wa CCM wa wilaya hiyo, waliokuwa wamevalia sare za Chama.
“Wana-CCM jipangeni vizuri uchaguzi wa mwakani usiwe wa rushwa, yeyote atakayehonga sitampitisha. Nataka Chama cha wanyonge, maskini na siyo cha rushwa,” alieleza na kuongeza kuwa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ungefanywa kwa rushwa, asingekuwa rais.
“Hata mie sikutoa rushwa, lakini mlinichagua. Nataka viongozi wanaotumikia watu, sio wanaochumia matumbo yao,” alieleza.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema serikali itamsambaratisha kwa nguvu zote, mtu yeyote atakayethubutu kuvuruga amani ya nchi na kuwataka watu waachane na siasa za ‘mapambo’.
Amesema siasa hizo hazifai kwa nchi kama Tanzania, ambayo inaweza kuongoza duniani kwa kuwa na watumishi hewa, waliokuwa wakiishi kwa kunyonya wanyonge.
Rais Magufuli alitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kigongo na Usagara, wilayani Misungwi na jijini hapa juzi, wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza barabarani kumpokea wakati akitokea wilayani Sengerema.
“Tunaweza kuongoza duniani kwa wafanyakazi hewa, ambao wamefikia 12,500. Walikuwa wakilipwa mishahara bure bila kufanya kazi, hivyo nitaendelea kutumbua majipu hadi rasilimali za watanzania ziwashukie wa chini,” alieleza Rais Magufuli.
Alisema kama ilivyo wajibu wa kila mmoja kutunza rasilimali hizo, ndivyo ilivyo katika jukumu la kulinda na kudumisha amani ya nchi na kuwaagiza polisi, wawahenyeshe wahalifu na watu watakaochezea amani.
“Nawapongeza polisi, akiwemo RPC wa Mwanza, pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama Mwanza. Endeleeni kudhibiti wahalifu na anayetaka kuchezea amani, acheze yeye kwanza kabla ya kuichezea,” alionya Rais Magufuli wakati akizungumza na wananchi wa Kigongo Feri.
Alisisitiza tena umuhimu wa kutochezea amani wakati akizungumza na wananchi wa Usagara na Nyegezi Stendi, ambapo alisema: “Tuacheni siasa za mapambo. Amani ikisambaratika, hakuna atakayekaa kufanya kazi na kutembea barabarani. Atakayechezea amani nitamsambaratisha kwa nguvu zangu zote.”
Huku akiwauliza wananchi hao ni wangapi wanataka amani na kumtaka aendelee kutumbua majipu, Dk. Magufuli alisema siasa uchwara, ukabila na udini viwekwe kando na kutanguliza utaifa mbele ili wajenge taifa jipya la viwanda na kuzalisha ajira nyingi kwa vijana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment