Thursday, 11 August 2016

JPM: HAKUNA CHAKULA CHA BURE



Rais John Magufuli amesema serikali haitatoa chakula cha bure kwa kuwa haina shamba na kuwataka wananchi, hasa vijana wafanye kazi kwa juhudi na kuzalisha mavuno ya kutosha ili nchi iondokane na baa la njaa.

Pia, ameziagiza halmashauri zote nchini, kufuta sheria ndogondogo zisizo rafiki kwa wakulima.

Alitoa kauli hiyo jana, wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani, ulioko mji mdogo wa Sengerema wilayani hapa.

“Lazima tujifunze kufanya kazi na siyo kusubiri serikali iletee chakula.Nataka watanzania waelewe hivyo. Hata Chato ninakotoka, sitapeleka chakula, lazima tufike mahali tuambizane ukweli. Asiyefanya kazi asile,” alisisitiza Dk. Magufuli na kuwataka vijana wasikalie kucheza pool na kuwaachia wazazi kazi ya kilimo.

“Mmezoea maneno ya kisiasa, hakuna atakayekufa na njaa, mie nawaambia  watakaokufa kwa njaa Tanzania ni wasiofanya kazi,” alisema na kuwaagiza wakuu wa wilaya na mikoa yote wasimamie watu kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha chakula cha ziada.

Alieleza kuwa serikali ya Magufuli ni ya kujenga barabara, kupeleka dawa  bure hospitalini na kulipa ada ili watoto wa masikini wasome.

"Haiwezekani serikali iwaletee magunia ya chakula. Mkalime kweli kweli. Ukilima, kajenge nyumba ya bati maana mlinichagua kufanya kazi,” aliwaeleza wananchi.

Rais Dk.Magufuli aliziagiza halmashauri zote nchini kufuta sheria ndogo za ushuru wa mazao zisizo rafiki kwa wakulima na kumtaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuondoa matuta yote barabarani .

Magufuli alitoa agizo hilo kwa TANROADS  wakati akiwasalimia wananchi wa Kasamwa wilayani Geita.

Alisema kuwa wananchi wanakerwa na kutozwa ushuru wa ovyo ovyo kwenye mazao yao, hivyo kuanzia sasa hakuna kuwatoza, badala yake utafutwe ushuru kwenye mazao makubwa kwenye maroli na sio gunia moja, mawili hadi kumi.

“Madiwani mko hapa mnanisikia, naagiza kwenye halmashauri zote nchini, mkafute sheria ndogo ndogo zinazohusu ushuru wa mazao kwa wananchi wanyonge. Wananchi wanapoteza nguvu zao nyingi, waacheni tujenge uchumi kwa sababu wameitikia wito wa hapa kazi tu,” alisema na kuwataka watendaji wasibadilishe maagizo hayo.

Akizungumzia  suala la wachimbaji wadogo, Rais Magufuli alisema anakusudia kutoa maamuzi ya kutowaondoa wachimbaji wadogo kwenye maeneo watakayovumbua madini.

Alisema anataka wananchi hao wasiondolewe katika maeneo hayo, badala yake wawezeshwe na kumilikishwa ili watengeneze faida, badala ya kuwaondoa na kuwapa wachimbaji wakubwa au wawekezaji wa kigeni.

Rais Magufuli pia aliwaeleza wananchi wa majimbo ya Sengerema na Buchosa kuwa, barabara ya Kamanga-Sengerema yenye urefu wa kilometa 35, itajengwa kwa kiwango lami na tayari upembuzi yakinifu unafanyika kwa ajili ya kazi hiyo, ambapo aliahidi kujenga barabara ya Sengerema-Nyehunge kwa kiwango cha lami baada ya fedha kupatikana.

Kuhusu daraja la Kigongo -Misungwi-Busisi Sengerema, alisema katika bajeti ya mwaka huu, fedha zimetengwa sh.milioni 600 na serikali imetoa kazi ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu, ukimalizika nalo litajengwa na kuunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema.

Dk. Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alisema serikali yake itatekeleza ununuzi wa meli kubwa itakayofanya kazi katika Ziwa Victoria, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,000 na tani 1,000 za mizigo.

Alisema mbali na meli, tayari ndege mbili zimenunuliwa huku serikali ikatarajia kununua ndege nyingine ya tatu, itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 .

Akizungumzia sakata la kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo (machinga) katika maeneo wasiyotakiwa kufanya biashara jijini hapa, aliondoa agizo la kuwaondoa ifikapo Agosti 30, mwaka huu, hadi watakapoandaliwa maeneo ya kupelekwa.

Aliaagiza serikali ya mkoa na uongozi wa jiji la Mwanza, wakutane na wafanyabiashara hao na kuwapa muda wa miezi miwili hadi mitatu, wakati wakiandaa miundombinu ya maeneo watakayowapeleka.

No comments:

Post a Comment