WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amewataka wanaoomba hifadhi kutoka nchi ya Burundi, kuacha kuanzisha kambi za kujifunza ugaidi wawapo kwenye kambi za hifadhi.
Amesema zipo taarifa kuwa baadhi ya waomba hifadhi wamekuwa na tabia ya kufanya mafunzo ya kigaidi kwa lengo la kwenda kufanya ugaidi watakaporudi nchini mwao.
Mwigulu alisema hayo jana, wakati akizungumza na baadhi ya waomba hifadhi katika kituo cha kuwapokelea kilichopo Manyovu, wilaya ya Buhigwe na waomba hifadhi walioko katika kambi ya Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani hapa.
Waziri huyo alisema mkimbizi yeyote atakayegundulika anajihusisha na mafunzo ya kigaidi, atachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema waomba hifadhi wote wanatakiwa kuishi kwa kufuata sheria na utaratibu wa nchi na kuachana na vitendo vya kujifunza ugaidi pindi wawapo kambini, hali inayosababisha kuongezeka kwa matendo ya kihalifu.
Aliwataka waomba hifadhi kuhakikisha wanafuata sheria na utaratibu wanaopewa pindi wawapo kambini na kuishi kwa undugu bila ubaguzi na kwa kufuata tamaduni walizozikuta nchini, huku akiwataka kuacha ubaguzi wenye lengo la kuwatenganisha raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na wale wa kutoka Burundi.
Pia, aliwaomba kuhakikisha usalama unaendelea kuimarika na kuacha vitendo vya uhalifu na kujihusisha na ugaidi, lengo likiwa ni kwenda kufanya vurugu nchini mwao wanaporejea huko.
Waziri Mwigulu alisema Tanzania sio nchi inayotoa mafunzo ya ugaidi,
hivyo yeyote atakayegundulika anafanya hivyo, atachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani bila kujali ni raia au amepewa hifadhi.
Mbali na hilo, aliziomba kamati za ulinzi na usalama mkoani Kigoma, kuhakikisha zinadhibiti wahamiaji haramu na uingizwaji wa silaha, mambo yanayosababisha kuongezeka kwa matukio ya uhalifu.
No comments:
Post a Comment