Monday, 15 August 2016

WALIOIFILISI NYANZA KITANZINI


RAIS Dk. John Magufuli ameagiza mali za Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Mwanza, Nyanza (NCU 1984 Ltd), zilizouzwa kwa bei chee, zirudishwe mikononi mwa wanaushirika huo.

Pia, ameagiza nyavu haramu zinazoingizwa nchini zikamatwe na magari yanayoziingiza yataifishwe, huku akimtaka Waziri wa Kilimo, Ushirika, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba, aongeze kasi ya kukamata na kuchoma zana haramu.

Dk. Magufuli alitoa maagizo hayo jana, wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa jiji la Mwanza na vitongoji vyake, kwenye uwanja wa Furahisha, Kirumba.

Alisema haiwezekani mali za wanyonge zichezewe bila hatua kuchukuliwa na kuvitaka vyombo vya dola na serikali ya mkoa wa Mwanza, chini ya uongozi wa John Mongella (mkuu wa mkoa), kuchukua hatua za kurudisha mali hizo haraka.

“Polisi na mkuu wa mkoa mpo hapa, haiwezekani mali za wanyonge zikawa zinachezewa, lazima zirudi, ushirika wa Nyanza ulikuwa na Ginnery nyingi, lakini sasa zimekufa,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa, aliyenunua kiwanda cha New Era kwa bei chee ya sh. milioni 30, badala ya zaidi ya sh. bilioni moja, hakitumii kama kiwanda cha mafuta.

Alifafanua kuwa, kilimo cha pamba kimeshuka na kinaelekea kufa kwa sababu ya kutoweka kwa Nyanza na kutafuna mali zake kwa maslahi ya matumbo ya watu binafsi, hali inayosababisha wakulima wa zao hilo kuteseka na kukata tamaa.

“Mkuu wa mkoa, tunalipwa mishahara, tujipange kwa majukumu ya wananchi hawa, tusipofanya hivyo tutahukumiwa siku moja, kama siyo hapa basi mbinguni. Mali za Nyanza zirudi mikononi mwa wenyewe,” alisisitiza na kuzitaja baadhi ya Ginnery za ushirika huo zinazomsikitisha kutokana na kufa kwake kuwa ni pamoja na Manawa, Kasamwa, Buchosa na Nassa.

Akizungumzia kukithiri kwa uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, Dk. Magufuli alisema lazima ziwa hilo lilindwe kwa nguvu zote na kumtaka Waziri Tizeba, aige mfano wake wa kukamata na kuchoma zana haramu kama alivyokuwa akifanya wakati akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

“Tunataka kiwanda cha ngozi cha Mwanza, kiwanda cha nguo na viwanda vya samaki Mwanza vifufuliwe. Viongozi wa serikali kuna baadhi ya nyavu haramu zinapita mipakani, zishikeni ikiwezekana mtaifishe na magari yanayoziingiza,” aliagiza.

Akisisitiza suala la machinga kutohamishwa bila kuandaliwa mazingira mazuri ya kufanyia biashara, Dk. Magufuli alisema waandaliwe maeneo rafiki yaliyoko mjini, badala ya kuwapeleka milimani kusikokuwa na biashara.

Alishauri uwekwe utaratibu wa kufunga baadhi ya mitaa siku za wikiendi (Jumamosi na Jumapili), kama inavyofanywa hata katika baadhi ya miji ya Ulaya ili wafanyabiashara hao wapate riziki, kwani alipokuwa akiomba kura, aliahidi kuwasaidia maskini, wakiwemo machinga na mama lishe.

Akizungumzia upanuzi wa barabara ya Mwanza kwenda uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa na njia nne na ujenzi wa kivuko cha watembea kwa miguu, Rais Magufuli alisema kuwa ni moja ya utekelezaji wa ahadi zake na shauku yake kubwa ni kuifanya Mwanza kuwa kiungo cha nchi za maziwa makuu na jiji la kibiashara.

“Lazima tutengeneze Mwanza mpya. Daraja hilo ni kubwa kuliko la Mabatini na mkandarasi anatakiwa kulikabidhi mwezi Desemba.
Nataka pasiwepo kisingizio chochote ili ikiwezekana siku ya Krismasi  watu wafungie ndoa kwenye daraja hilo,” alisema na kuwafanya wananchi waangue vicheko.

Akizungumzia ujenzi na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Dk. Magufuli aliagiza mkandarasi aendelee na ujenzi mara moja na kwamba, fedha anazodai ni ndogo na zitalipwa, hivyo aache visingizio kuwa anadai fedha nyingi.

Aidha, Rais Magufuli alisema yeye ni mtumishi wa Watanzania wote waliomchagua kwa kuwa wao ndio taasisi nzima ya urais kwake.

Pia, alisema anamuomba Mwenyezi Mungu, urais alionao usimpe kiburi na majivuno ili aweze kuwatumikia Watanzania wote kwa uadilifu mkubwa.

“Nitawatumikia Watanzania wote ili kila mmoja aweze kunufaika na maendeleo yaliyopo na sintawaangusha," alisema.

No comments:

Post a Comment